HOTUBA YA MWENYEKITI WA CCM TAIFA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO
KIKWETE, KATIKA SHEREHE ZA KUTIMIZA MIAKA 38 YA CCM, KWENYE UWANJA WA MAJIMAJI,
SONGEA - RUVUMA,
TAREHE 01 FEBRUARI, 2015
Mwenyekiti wa CCM Rais Kikwete akihutubia umati wa wananachi
Ndugu
Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM;
Mheshimiwa
Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu na mjumbe wa Kamati Kuu;
Mheshimiwa
Anne Makinda, Spika wa Bunge na Mjumbe wa Kamati Kuu;
Ndugu
Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;
Ndugu
Mike Mukula, Makamu Mwenyekiti wa NRM ya Uganda na ujumbe wake;
Waheshimiwa
Wajumbe wa Kamati Kuu;
Mheshimiwa Oddo
Mwisho, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma;
Waheshimiwa Wajumbe
wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa;
Wajumbe
wa Sekretarieti ya CCM;
Ndugu Verena
Shumbusho, Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma;
Wenyeviti
wa Jumuiya za CCM;
Viongozi,
wananchama na wapenzi wa CCM;
Naomba nianze kwa kuwashukuru na
kuwapongeza wenyeji wetu kwa mapokezi
mazuri, hususan napenda kuwatambua wananchi, viongozi na wana-CCM wa
Mkoa wa Ruvuma wakiongozwa na Mwenyekiti wao ndugu Oddo Mwisho, Katibu wa Mkoa
Mama Verena Shumbusho, Mkuu wa Mkoa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa Ndugu Said
Mwambungu. Nawapongeza kwa maandalizi mazuri ya sherehe hizi. Hakika zimefana
sana. Hii ni mara ya pili sherehe hizi kuadhimishwa
mkoani hapa. Mara ya kwanza ilikuwa
mwaka 1991 wakati wa kuazimisha miaka 14 ya CCM.
Tunatambua kuwa mmefanya kazi kubwa ya maandalizi mpaka mmeweza kufanikisha shughuli ya leo kwa
kiwango cha juu. Waswahili wanasema “Usione vinaelea Vimeundwa”. Napenda
kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa Katibu Mkuu Abdulrahman Kinana kwa
uongozi wake makini uliowezesha mambo kuwa mazuri kiasi hiki. Hongera sana kwa hili na kwa kazi nyingi
nzuri unazofanya kwa maslahi ya Chama chetu na nchi yetu.
Leo ni siku ya furaha kwangu na kwa viongozi na
wanachama wenzangu wa CCM kote nchini ya kusherehekea na kuadhimisha miaka 38
ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi. Tunastahili kuisherehekea siku hii kwa
nderemo na vifijo kwa sababu ya mafanikio makubwa ambayo Chama chetu
kimeendelea kupata ndani ya Chama na katika kuliongoza taifa letu. Katika miaka
38 ya uhai wake Chama chetu kimezidi kuimarika na kimeendelea kuliongoza vyema
taifa letu: kuna amani, utulivu na maendeleo yanayoonekana.
Tumeeendelea kuaminiwa na kutumainiwa na Watanzania.
Kama ilivyothibitika na ushindi wa kishindo katika chaguzi zote tangu mfumo wa
vyama vingi uanze mwaka 1995 mpaka sasa.
Hata mwaka huu itakuwa hivyo hivyo. Dalili ya mvua ni mawingu: ushindi mnono
tulioupata kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni dalili tosha kwamba Oktoba,
2015 watani zetu hawana chao.
Ninaposema hivyo nawaomba wana CCM wenzangu tusibweteke
tukadhani kwamba ndiyo tumekwishafika. Bado safari ndiyo kwanza tumeianza na
inaweza kuwa na changamoto zake. Lazima
tufanye kazi tena kazi kubwa sana ndipo tutakapojihakikishia ushindi. Nguvu ya ushindi inaanzia kwenye Chama. Huu ni mwaka ambao kazi ya Chama ndani ya
Chama na kazi ya Chama ndani ya umma inatakiwa ifanyike kwa nguvu zaidi na kwa
ari kubwa zaidi. Lazima tuhakikishe tunao
umoja wa dhati na kwamba wanachama wetu
wanakuwa na mwamko wa hali ya juu wa kukipigania Chama katika kutafuta na kupata
ushindi kwa Udiwani, Ubunge, Uwakilishi, Urais wa Zanzibar na Urais wa
Muungano.
Huu ni mwaka ambao wanachama na viongozi
wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanakutana mara kwa mara kwa mujibu wa Katiba na
hata zaidi kuzungumzia mikakati ya kupata ushindi na kuitekeleza. Huu ni mwaka ambao lazima tuhakikishe kuwa
tunazo rasilimali na nyenzo za kutuwezesha kufanya kazi ya Chama ndani ya umma
na kuwapatia ushindi wagombea wa Chama chetu.
Huu ni mwaka ambao kazi ya Jumuiya za Chama ya kukiwezesha
Chama kuungwa mkono na jamii pana ya Watanzania walio vijana, wanawake na
wazazi inafanyika kwa umahiri na ufanisi wa hali ya juu.
Bila ya shaka, ndugu zangu mtayakumbuka maneno
niliyoyasema kwa kuyarudia kuwa “Mwisho wa uchaguzi mmoja ndiyo mwanzo wa
uchaguzi mwingine”. Najua baadhi yenu mmezingatia na kuchukua hatua za
kufanya maandalizi mapema ya uchaguzi wa mwaka huu mara baada ya
kumaliza uchaguzi wa mwaka 2010. Hao nawapongeza. Lakini wapo viongozi na wanachama ambao
hawajafanya chochote. Hawa, wananisikitisha
kwa athari mbaya na hatari ya kupoteza ushindi wanayokiletea Chama chetu.
Naomba kila mmoja wetu ajipime yupo fungu gani.
Kama upo kwenye kundi la kwanza lililokwishaanza maandalizi natoa pongezi
nyingi. Nawaomba muendelee kukamilisha
ipasavyo. Kwa wale ambao wapo kundi la wale ambao maandalizi yao ni ya kiwango
kidogo au hawajaanza kabisa lazima waanze na wakati ni huu. Usikawie, unatakiwa kufanya kazi kwa ari
zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi kama ilivyo kauli mbiu ya CCM. Yapo mambo
kadhaa ya kufanya ambayo tulikwishaambiana tufanye. Miongoni mwao ni lile agizo la kutaka kila
ngazi ya Chama na hasa Wilaya na Mikoa kuwa na Mfuko wa Uchaguzi. Wakati wake
ndio huu sasa wa mfuko huo kufanya kazi iliyokusudiwa. Naomba tujiulize wangapi wanayo mifuko hiyo
na wangapi hawana. Kwa wale walionayo
wahakikishe ina rasilimali za kutosha.
Kama hazitoshi waweke mikakati ya kuitunisha mifuko hiyo. Kwa wale ambao hawajaanzisha wachune bongo
kuhusu namna ya kupata fedha za kuendeshea shughuli za uchaguzi. Sina budi
kuwatahadharisha kuwa msichukue fedha ambazo zitazua matatizo.
Ndugu
viongozi na ndugu wanachama;
Huu ni mwaka wa kutambua ahadi zipi tulizotoa
zimetimizwa na zipi bado. Kwa zile
ambazo hazijakamilika wajibu wetu ni kuweka mikakati ya kuzikamilisha. Kwa zile ambazo hazitakamilika tutafute
maelezo sahihi ya kutoa kwa wadau wa huduma hiyo. Naamini hazitakuwa nyingi za kuchosha. Mwaka
huu siyo mzuri kwenda na madeni lukuki ya ahadi. Yanaweza kutupunguzia ushindi wetu.
Huu ni mwaka wa kuongeza ukubwa wa jeshi letu la
ushindi kwa kuongeza wananchama wapya. Natambua tatizo la upungufu wa kadi
lakini najua mipango thabiti iliyopo ya kuleta kadi nyingi za kutosha wale
waliopo nje. Tujiepushe na kuingiza mamluki hivyo taratibu za kuingiza
wanachama zizingatiwe ipasavyo.
Ndugu
Viongozi;
Ndugu
Wananchi;
Jambo lingine kubwa na muhimu sana kufanya mwaka
huu ni kuwatembelea wanachama na wananchi na kuzungumza nao. Hatujaifanya
vizuri sana kazi hii lakini hatujachelewa. Sina budi kutoa pongezi maalum kwa Katibu Mkuu
wa CCM kwa ufanisi mkubwa aliopata kwa jambo hili. Sote hatuna budi kuiga mfano wake mzuri. Tuache kukaa maofisini tutoke kuzungumza na
watu kuwashawishi waunge mkono na kuipigia kura CCM katika uchaguzi ujao. Kila
Ofisi ya Mkoa na kila Ofisi ya Wilaya inalo gari la kuwawezesha kufanya kazi
hiyo. Tafadhali fanyeni hivyo, kwani bila ya kufanya hivyo hakuna uhakika wa
kupata ushindi. Kilichobakia kwa upande
wetu ni kutafuta vipando kwa Ofisi za Kata na Matawi. Tusaidiane pale
inapowezekana.
Uandikishaji wa
Wapiga Kura
Ndugu wana CCM na ndugu Wananchi;
Jambo lingine muhimu katika kutafuta
ushindi ni kupatikana kwa wapiga kura.
Chama chetu kama vilivyo vyama vingine, hatuna budi kuwahimiza wanachama
wetu, wapenzi wetu na wananchi wengine wajitokeze kwa wingi kujiandikisha
kupiga kura. Mwaka huu wenye kadi mpya
za mpiga kura ndiyo watakaoruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu na katika
kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendekezwa.
Asiyejiandikisha hatapata fursa ya kushiriki kura
ya maoni na uchaguzi mkuu. Kwa sababu
hiyo nawaomba viongozi na wanachama wa CCM wawe ndiyo wa kwanza kujitokeza
kujiandisha. Pia wawe mstari wa mbele
kuwahimiza wananchi wengine kujiandikisha.
Nawaomba jambo hili mlipe uzito mkubwa kwani safari ya kutafuta na
kupata ushindi inaanzie kwenye kupata wapiga kura hususani wapiga kura wanaounga
mkono Chama chetu na wagombea wetu.
Kura ya Maoni
Ndugu
wananchi;
Kama mjuavyo, jambo kubwa lililo mbele
yetu ni kura ya maoni kuhusu Katiba Inayopendezwa itakayofanyika tarehe 30
Aprili, 2015. Maandalizi yote husika yanaendelea kufanyika ili kuwezesha kura
hiyo kutekelezwa kama ilivyopangwa. Kama nilivyokwishaeleza hivi punde
uandikishaji wa wapiga kura ni miongoni ma maandalizi hayo. Mengine ni
uchapishaji na usambazaji wa Katiba Inayopendekezwa.
Yapo mambo kadhaa ambayo nawasihi viongozi na
wanachama wenzangu mfuatilie kwa karibu ili yasiwapite. Yale tunayoyajua
tuwaambie. Miongoni mwa mambo muhimu sana ambayo Chama hakina budi kujipanga
vizuri ni kuhusu kutoa elimu kwa umma kuhusu Katiba Inayopendekezwa na kampeni
ya Kura ya Maoni. Watani zetu watatoa elimu hasi kuhusu Katiba Inayopendekezwa, sisi tutoe elimu
chanya. Wenzetu watataka Katiba Inayopendekezwa
isipite. Sisi tupige kampeni ikubalike.
Nilisema siku ile Dodoma wakati wa
kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa na narudia tena leo kwamba Katiba Inayopendekezwa imebeba maslahi mapana ya
taifa letu. Hatujawahi kuwa na Katiba kama hii Inayopendekezwa. Misingi ya historia ya nchi yetu yaani kule
tulikotoka, tulipo sasa na tuendako imezingatiwa vizuri. Katiba hiyo inatambua maslahi
ya makundi yote nchini na kuyawekea utaratibu mzuri wa kutekelezwa. Wakulima,
wafugaji, wavuvi, wanawake, vijana, wasanii, wafanyakazi, wazee na watoto wametambuliwa
kwa kina na upana zaidi kuliko Katiba ya sasa.
Katiba Inayopendekezwa imeshughulikia kero za Muungano
na kujenga mazingira bora zaidi kwa Muungano wetu kuimarika. Yale mambo
yaliyokuwa yanaikwaza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kuukwaza Muungano
yamepatiwa ufumbuzi mwafaka. Sasa Zanzibar itaendesha na kushughulikia mambo
yake kwa uhuru mkubwa zaidi.
Ndugu
wananchi;
Kwa
maoni yangu sioni sababu ya kuikataa Katiba Inayopendekezwa. Hatuna budi
kutambua kuwa tukiikataa Katiba Inayopendekezwa, Katiba ya sasa itaendelea
kutumika mpaka hapo mchakato mwingine utakapomalizika miaka mingi ijayo. Viongozi
wa vyama vinne vya siasa wamesikika wakisema watasusia kushiriki katika kura ya
maoni na kuwataka wanachama wao wasishiriki. Kauli hiyo imenisikitisha sana
ingawaje haikunishangaza hasa tukikumbuka waliyoyafanya wakati wa Bunge la
Katiba. Mimi nawaomba washiriki.
Nawasihi wananchi wasiwasikilize. Wao wakitaka
kususia waacheni wasusie lakini nyie jitokezeni kupiga kura. Nawasihi msikubali kupoteza mema mengi yaliyo
katika Katiba Inayopendekezwa ati kwa sababu tu hakuna Serikali Tatu walizokuwa
wanazitaka. Kama kweli wananchi wa Tanzania wanakereketwa na Serikali Tatu
watathibitisha hiyo kwenye kura ya maoni.
Naomba msibabaishwe wala kudanganywa na watu
wanaotaka kuturudisha nyuma kutoka katika hatua kubwa muhimu tutakazopiga kwa
kuikubali Katiba Inayopendekezwa. Tusikubali kubaki nyuma.
Uchaguzi Mkuu
Ndugu
wananchi;
Kama mjuavyo mwezi Oktoba, 2015 nchi
yetu itafanya uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge, Wawakilishi, Rais wa Zanzibar
na Rais wa Jamhuri ya Muungano. Uchaguzi wa mwaka huu ni wa kihistoria kwa nchi
yetu kwani tunachagua Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mimi nataka Rais huyo awe mwana CCM.
Sisi sote katika CCM tunataka Rais atoke katika Chama chetu kwa sababu kama alivyousia Baba Wa Taifa
Mwalimu Julius Nyerere “Rais wa nchi yetu anaweza kutoka Chama chochote lakini Rais bora
atatoka CCM”.
Huu ni usia mzito wenye maono ya mbali. Tusiupuuze wosia huu bali tuuenzi. Sisi katika Chama cha Mapinduzi tuwe mstari
wa mbele katika kuuenzi wosia huu kwa kupata mgombea aliye bora wa kupeperusha
bendera ya CCM katika uchaguzi ujao.
Mgombea ambaye wananchi wakisikia jina lake likitajwa watasema naam, hapo sawa,
hapo barabara. Lakini tukiteua mgombea
ambaye watu wataguna na kusema hata huyu? Tutakuwa tumemuangusha Muasisi wa Chama chetu na taifa letu katika wosia
wake. Bila shaka laana yake tutaipata. Na hilo likitokea itakuwa hasara kubwa
kwa taifa letu na msiba kwa CCM. Nchi
itayumba.
Lazima tuhakikishe kuwa hatutafika huko. Watu wazuri wapo wa kutosha katika CCM na naamini
tunawajua. Kama hawajajitokeza
tuwashawishi wafanye hivyo. Ndugu zangu, tusifanye ajizi katika jambo hili
kubwa na la msingi kwa Chama chetu.
Kushinda chaguzi za dola katika sehemu zetu mbili za Muungano ndiyo
madhumuni makuu ya kuundwa na kuwepo kwa CCM.
Napenda kuwahakikishia wanachama wa
CCM na wananchi kuwa, Chama cha Mapinduzi ni Chama kilichokomaa, kilicho makini
na imara. Tunao utaratibu unaoeleweka na
kutabirika wa kuwapata wagombea. Inazo kanuni na vigezo vya wazi vya kuwapata
viongozi walio bora, na tunavyo vikao rasmi vya kuchuja na kuteua wagombea kwa
kuzingatia kanuni, taratibu na maadili ya Chama chetu. Hivyo basi, hapataharibika
jambo.
Naomba niwahakikishie kwamba CCM itawapatia
Watanzania wagombea bora ambao hawatawapa wananchi mashaka wala kigugumizi cha
kuwachagua. Tutafanya hivyo kwa nafasi
ya Rais wa Muungano, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani. Nawaomba
wagombea wazingatie na kuheshimu masharti ya Katiba ya Chama, Kanuni na Madili
ya uteuzi kwa wanaotaka kuteuliwa kugombea nafasi katika chaguzi za dola.
Asiyezingatia hayo asije akakilaumu Chama bali ajilaumu mwenyewe kwa makosa
aliyoyafanya.
Utekelezaji wa Ilani
ya Uchaguzi wa CCM
Ndugu
wananchi;
Miezi minne iliyopita nilifanya ziara
ya mkoa huu wa Ruvuma kukagua shughuli za maendeleo. Nimefurahishwa sana na jitihada za kujiletea
maendeleo zinazofanywa na wananchi wa mkoa huu na mafanikio mnayoendelea
kuyapata. Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na mipango mbalimbali ya
serikali unakwenda vizuri, kiasi cha kuwastajabisha hata wale waliokuwa na
mashaka na wasio tutakia mema.
Yako mambo mengi tuliyoahidi kufanya ambayo
tumeyakamilisha na mengine utekelezaji wake unaendelea vizuri. Kilio cha miaka
mingi cha wananchi wa mkoa huu kuhusu barabara kimefanyiwa kazi vya kutosha.
Ujenzi wa barabara ya Namtumbo – Songea
na Peramiho - Mbinga kwa kiwango cha
lami umekamilika. Tunaendelea na ujenzi wa barabara ya Namtumbo – Tunduru na Tunduru
– Mangaka ili kuunganisha mkoa wa Mtwara na Ruvuma kwa barabara za lami.
Aidha, mipango ya kujenga barabara ya Mbinga
– Mbambabay kwa mkopo wa Benki ya Maendeleo ya Afrika imefikia mahali
pazuri. Kwa upande wa usafiri katika
Ziwa Nyasa hivi sasa mchakato wa ujenzi wa chelezo cha kujengea meli ya ziwa
hilo kule kwenye bandari ya Itungi, Kyela unaendelea vizuri. Ujenzi wa chelezo
ukishakamilika ujenzi wa meli utaanza.
Kwa upande wa umeme tunaendelea na ujenzi wa njia
ya umeme ya msongo wa Kv 220 kutoka Makambako kuja Songea na hadi Mbinga na
Namtumbo. Ujenzi wa njia hii ya umeme
utakapokamilika utawahakikishia wakazi wa mji wa Songea na mkoa wa Ruvuma umeme
wa uhakika. Tumechelewa kidogo kwa sababu ya kubadilisha ukubwa wa njia kutoka
msongo wa Kv 132 tuliyotaka kujenga awali hadi Kv 220. Aidha, usambazaji wa
umeme vijijini unaendelea kwa kasi katika maeneo yote nchini. Tunataka ifikapo
June, 2015 zaidi ya vijiji 5,336 viwe
vimepatiwa umeme. Kati ya vijiji hivyo zaidi ya vijiji 300 ni vya mkoa wa Ruvuma. Haya ni mafanikio makubwa na ya kutia
moyo.
Kuhusu sekta ya Afya nako pia tumepata mafanikio
makubwa katika utoaji wa huduma ya afya kwa Watanzania. Kwa hapa Songea
nimekwishatoa maelekezo kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuanza mchakato
wa ujenzi wa hospitali mpya ya Mkoa wa Ruvuma na hii iliyopo sasa iwe ni hospitali
ya Manispaa ya Mji wa Songea. Halmashauri ya Manispaa ya Songea iharakishe kutenga
eneo la kutosha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ya mkoa ambayo itakuwa ni
ya rufaa kwa yale ambayo hospitali za Wilaya zitashindwa kumudu.
Haya ni maeneo machache tu ambayo yanaonyesha
hatua kubwa tuliyopiga katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na maendeleo ya
mkoa huu. Ukweli ni kwamba Ruvuma ya miaka 10 iliyopita siyo Ruvuma ya leo.
Ninyi nyote ni mashahidi wa mambo haya. Mwenye macho haambiwi tazama.
Ndugu
wananchi;
Jambo la mwisho ambalo napenda kulizungumzia
ambalo nilishalizungumzia kwenye hotuba yangu ya mwaka mpya inahusu ununuzi wa
mazao ya wakulima. Nilieleza siku ile kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA) ilikuwa bado haijalipa shilingi
bilioni 89 kwa wakulima kwa mazao yao iliyonunua. Nilielezea kutokufurahishwa
kwangu na hali hiyo na kuagiza Wakala
kulipa deni hilo.
Nimeambiwa kuwa tayari shilingi bilioni 15 zimeshatolewa na hapa Ruvuma mmepata shilingi bilioni 8. Hivi karibuni shilingi bilioni 36 zitatolewa na kubaki shilingi bilioni 38 ambazo zitalipwa mwezi Machi.
Jambo lingine ambalo tunaendelea nalo kulishughuikia
katika Serikali ni kupata masoko mengine kwa mazao ya wakulima. Kama nilivyosema NFRA haiwezi kununua mazao
yote ya wakulima nchini. Uwezo wake ni kuhifadhi tani 240,000 wakati uzalishaji wa mahindi hapa Ruvuma ni tani 993,350. Hata kama NFRA ingeamua kununua mahindi yote
kutoka mkoa wa Ruvuma peke yake isingeweza kuyamaliza.
Nimewaagiza viongozi wa mkoa wa Ruvuma na mikoa yote nchini washirikiane na Wizara ya
Kilimo, Chakula na Ushirika na Wizara ya Viwanda na Biashara kutafuta masoko mengi
kwa ajili ya mahindi, mpunga na mtama wa wakulima ndani na nje ya nchi.
Tunakokwenda
Ndugu
wana CCM;
Mafanikio
ya miaka 38 ya Chama chetu yasitufanye tubweteke. Bado tunayo kazi kubwa mbele
yetu. Ili tuendelee kuongoza dola hatuna
budi tuendelee kuwa tumaini na kimbilio la wananchi wetu. Inatupasa kuwa
waaminifu kwa ahadi zetu na watiifu kwa matakwa yao. Kubwa sana, tunatakiwa tuwe tayari wakati
wote kubadilika na kwenda na wakati. Tunaweza kufanya hivyo ikiwa tutaendelea
kukuza Demokrasia ndani ya Chama chetu na kuruhusu na kuvumilia tofauti za
mitazamo. Hiyo ndiyo siri ya uhai wa CCM
ambayo hatuna budi kuendeleza.
Tunapoanza safari ya kuelekea mwaka wa
39, hatuna budi sasa kuelekeza nguvu zetu kwenye kuondoa utegemezi wa kifedha
kutoka kwenye ruzuku na michango ya wafanyabiashara. Kutegemea misaada na michango si mambo endelevu
na huo hauwezi kuwa ni mkakati wa kutumainiwa wa kuimarisha Chama chetu. Wakati mwingine michango hii imetugharimu
ndani ya Chama chetu. Lazima tuwe
wabunifu katika kutafuta vyanzo vya mapato ikiwa ni pamoja na rasilimali zetu nyingi
tulizonazo ili kuwezesha Chama kujitegemea. Tayari yako mawazo yaliyoibuliwa
kutokana na kazi nzuri ya Kamati iliyoongozwa na Mjumbe wa Kamati Kuu na Mweka
Hazina wetu Mheshimiwa Zakhia Meghji tumeagiza yatekelezwe. Naomba mtimize
ipasavyo wajibu wenu.
Hitimisho
Ndugu
wana CCM;
Leo ni siku ya furaha kwetu sote.
Wakati tukisherehekea mafanikio yetu tuwakumbuke pia waasisi wetu Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, aliyekuwa Mwenyeti wa TANU na Ndugu Sheikh Aboud
Jumbe aliyekuwa Mwenyekiti wa ASP kwa busara, hekima na uamuzi wao uliotukuka
uliowezesha kuzaliwa kwa CCM.
Tunawakumbuka pia wale wote waliotangulia mbele ya haki ambao walijitoa
maisha yao kujenga CCM. Hatuna budi
kuwaenzi kwa kutoa mchango mkubwa zaidi
mwaka ujao na miaka mingi ijayo. Tuhakikishe kuwa tunaimarisha Chama chetu na kutenda
mema kwa ajili ya nchi yetu na watu wake. Hili linawezekana ikiwa kila mtu
atatimiza wajibu wake. Kidumu Chama cha Mapinduzi!
Asanteni
sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment