Siku
ya tarehe 6 Februari, 2015; Tanzania itaungana na nchi nyingine duniani
kupinga vitendo vya ukeketaji wa wanawake na watoto wa kike unaofanywa
na baadhi ya jamii hapa nchini. Vitendo vya ukeketaji ni ukatili na
unadhalilisha utu na hadhi ya mwanawake.
Nchini Tanzania ukeketaji ni tatizo sugu na limedumu kwa muda
mrefu. Waathirika zaidi wa ukeketaji ni wasichana wenye umri kati ya
miaka 15-19 na watoto wa kike. Ukeketaji unafanywa kwa vile ni sehemu ya
mila na desturi za baadhi ya makabila. Katika jamii zenye imani hii,
ukeketaji unafanyika kwa wasichana ili waonekane kuwa wamefikia rika la
watu wazima. Aidha, kwa mangariba na wazee wa kimila kimekuwa ni
kichocheo cha vitendo hivyo dhalili kwani wanategemea mapato kutokana na
ukeketaji. Hapa nchini, mikoa yenye matukio ya ukeketaji ni pamoja na
Manyara (71%), Dodoma (64%), Arusha (59%), Singida (51%), Mara (40%),
Morogoro (21%) na Tanga (20%).
Serkali inakemea vikali vitendo vya ukeketaji sio tu kwamba vinaleta madhara makubwa kwa wanawake na watoto wa kike, bali pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Matukio haya ya ukeketaji yanasababisha madhara ya kiafya, kimwili na kisaikolojia kwa maisha ya watoto wa kike, wasichana na wanawake kwa ujumla. Mila na desturi ya ukeketaji ni tatizo katika jamii zetu kwani wanawake na watoto wengi wa kike wameendelea kufanyiwa vitendo hivyo bila ridhaa yao; vile vile, wanaumizwa, kuteseka, kutengwa, na hata kupoteza maisha kutokana na ukeketaji. Licha ya elimu inayoendelea kutolewa kwa jamii, matukio ya ukeketaji yameendelea kuwepo katika jamii zetu. Kutokana na hali hiyo, jukumu kubwa linaloikabili Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ni kuongeza nguvu katika kujenga uelewa kwa jamii kuhusu mila na desturi zenye madhara kwa wanawake na kuwa na njia mbadala wa kuziacha. Hatua zinazofikiwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ni kuendeleza juhudi za kupambana na vitendo vya ukatili ukiwemo ukeketaji kwa kuridhia Mikataba ya Kimataifa na Kikanda inayokataza ukatili. Aidha sera, sheria na mikakati mbali mbali imewekwa na kutekelezwa ili kuondokana na tatizo la ukatili huo. Pamoja na juhudi hizo, bado vitendo hivi vinaendelezwa na baadhi ya jamii zetu na kufanya kiwango cha ukeketaji kwa sasa kuwa asilimia 14.6. Imeonekana wazi kuwa ukeketaji unachangia kuongezeka kwa mimba na ndoa za utotoni hapa Tanzania kwa kuwa mtoto wa kike anapokeketwa anahesabiwa kuwa mtu mzima na anakuwa yuko tayari kuolewa. Hii inachangia watoto hawa kutokumaliza masomo yao na hivyo kuongezeka kwa watu wasioelimika nchini. Wakati dunia inaadhimisha siku maalum ya kupinga ukeketaji, Serikali inapinga hoja zinazoendeleza ukeketaji kwani sababu hizo zinamdhalilisha mwanamke na kumnyima haki mtoto wa kike kwa kisingizio cha kudumisha mila na desturi zisizo na manufaa. Wizara inaendelea kuwasisitiza wananchi wote kuunga mkono juhudi za Serikali katika kupinga ukeketaji ili kutokomeza mila zenye madhara. Aidha, Serikali na wadau itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuondokana na imani zinazoendeleza ukeketaji. Ni wazi kuwa jitihada za kupambana na ukatili wa kijinsia na mila zenye kuleta madhara hazitafanikiwa kwa kutegemea Serikali peke yake. Natoa wito kwa jamii husika na wadau wengine wote kwa pamoja kushiriki katika kuzuia ukeketaji ili kuwa na jamii salama, inayojali haki za binadamu na kuheshimu utu wa mwanamke na mtoto wa kike. ‘Kutokomeza Ukeketaji ni Jukumu letu Sote; Tekeleza sasa’.
Nuru M. Millao
Kny: KATIBU MKUU
05/02/2015
No comments:
Post a Comment