Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imewafungia kati ya mechi tatu na nane
wachezaji Juma Nyoso wa Mbeya City na Aggrey Morris wa Azam kutokana na
makosa ya kinidhamu waliyoyafanya wakiwa uwanjani.
Nyoso ambaye alilalamikiwa na TFF
kwa kumfanyia vitendo vya udhalilishaji mshambuliaji Elias Maguri wa
Simba amefungiwa mechi nane za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL). Adhabu hiyo
imetolewa kwa kuzingatia Ibara ya 57 na Ibara ya 11 (f) ya Kanuni za
Nidhamu za TFF Toleo la 2012.
Akiwa mbele ya Kamati hiyo jana
(Februari 5 mwaka huu) jijini Dar es Salaam, Nyoso alikiri kufanya na
kujutia kosa hilo, pia amemuomba radhi mchezaji Maguri kwa kitendo
hicho.
Akisoma uamuzi huo, Makamu
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Wakili Jerome Msemwa alisema kitendo
kilichofanywa na Nyoso ni kosa kubwa, kudhalilisha utu wa mtu, na ni
mfano mbaya kwa watoto na jamii nzima ya mpira wa miguu.
Naye Morris amefungiwa mechi tatu
za VPL baada ya kutiwa hatiani kwa kumpiga mshambuliaji Emmanuel Okwi
wakati timu hizo zilipopambana kwenye mechi ya ligi iliyochezwa Januari
25 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kabla ya kusoma uamuzi, Wakili
Msemwa alisema mlalamikiwa Morris alikiri kugongana na Okwi, kwa maelezo
kuwa aliingia kwenye ‘reli’ ndiyo ukatokea mgongano huo.
Kamati baada ya kupitia malalamiko
ya klabu ya Simba, ripoti za Brain CT scan kutoka Besta Diagnostic
Centre na nyingine kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), taarifa za
madaktari zilionyesha Okwi aligongwa kichwani akiwa anacheza mpira na
kuzimia kwa dakika tano, pia mkanda wa video uliowasilishwa na TFF
imeona kulikuwa na kugongana kati ya wachezaji hao.
Hivyo, Kamati ikamtia hatiani
Morris kwa kutumia Ibara ya 48(1)(d) ya Kanuni za Nidhamu za TFF Toleo
la 2012 kwa kumfungia mechi hizo tatu na kumpa onyo kali.
Pia Kamati hiyo imemfungia miezi
sita na kumpiga faini ya sh. 200,000 Meneja Vifaa (Kit Manager) wa timu
ya Polisi Mara, Clement Kajeri kwa kuhamamisha vurugu na kuwapiga
waamuzi kwenye mechi dhidi ya Mwadui iliyochezwa Uwanja wa Karume mjini
Musoma. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 40(2) ya Ligi
Daraja la Kwanza.
Wachezaji watatu wa Friends
Rangers; Mahmoud Othman, Khalid Twahil na John Alexander wamefungia
miezi sita na faini ya sh. 500,000 kila mmoja kwa kumpiga mwamuzi kwenye
mechi ya Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Majimaji.
Licha ya wachezaji hao kuitikia
mwito wa Kamati, wachezaji hao walizuiwa na viongozi wa kuingia ukumbini
wakati malalamiko dhidi yao yalipoanza kusikilizwa. Hatua hiyo
iliifanya Kamati ifanye uamuzi baada ya kuusikiliza upande wa
walalamikaji pekee.
Shauri dhidi ya mchezaji George
Michael wa Ruvu Shooting kwa kumchezea ubabe Amisi Tambwe wa Yanga,
Kamati imeliahirisha baada ya mlalamikiwa kupata udhuru uliosababisha
asiwepo.
Pia Kamati ya Nidhamu imeelekeza
malalamiko ya timu ya Friends Rangers kupinga refa kuchezesha mechi yao
dhidi ya Majimaji kwenye mvua kubwa, kutoa maamuzi yasiyo halali na
kutokuwepo na ukweli kwenye ripoti ya Kamishna yakasikilizwe na Bodi ya
Ligi kwa vile si masuala ya kinidhamu.
No comments:
Post a Comment