Immaculate Makilika –MAELEZO ARUSHA
Rais wa
shirikisho la Ujerumani,Jochim Gauck ameonesha kufurahishwa na
utendaji wa kazi wa Jumuiya ya afrika mashariki, EAC, na kusema ikiwa
Jumuiya hii itatimiza malengo yake iliyojiwekea basi itakua mfano bora
Afrika’.
Rais huyo
ameyasema hayo leo alipotembelea makao makuu ya jumuia ya Afrika
Mashariki EAC, mjini Arusha, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku
sita nchini na kusema kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC inafaida ya
kuwa na nchi zenye uchumi unaendelea kukua kwa asilimia 6 katika kipindi
cha miaka 10 iliyopita.
Amesema kuwa
Jumuia ya Afrika Mashariki ina watu zaidi ya milioni 145 huku wengi wao
wanazungumza lugha moja ya kiswahili pamoja na kuwa na tamaduni
tofauti, na kuongeza kuwa Jumuiya ya nchi za Ulaya EU hawana neema ya
namna hii.
Rais Gauck
ameelezea uhusiano mzuri uliopo baina ya Shirikisho la Jumuiya ya Afrika
Mashariki EAC na Shirikisho la Jumuiya ya Nchi za Ulaya EU na kusema
kuwa zinafanana kwa kiasi kikubwa hasa katika masuala ya utengamano wa
kisiasa.
Hivyo jumuiya hizo hazina budi kushirikiana pamoja katika masuala mbalimbali yenye kuleta tija.
‘Msiwaamini
wanaosema Shirikisho la Jumuiya ya Nchi za Ulaya limekufa’ alisema Rais
huyo, na kuongeza pia si kweli kwani hivi sasa Jumuiya hiyo ipo na
imeendelea kuwa na nguvu kuliko ilivyokuwa mwanzo, isipokuwa
imekabiliana na changamoto zake alisema.
Kwa upande
wake Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Harrison Mwakyembe
ameeleza kuwa, Tanzania ni Mshiriki wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na
ujio huu ni muhimu kwa kuwa Ujerumani inauzoefu katika
Masuala haya ya mtengamano.
Amesema,
Ujerumani imekua msaada mkubwa sana kwa Jumuiya hii tangu ianzishwe hadi
sasa imetoa jumla ya Euro milioni 100. Waziri Mwakyembe ameendelea kwa
kusema tuwe na imani na kuijengea Jumuiya umoja, kwani tukiungana
tutapata faida kubwa kuliko kutengana.
Aidha, Mbunge
wa Bunge la Shirikisho la Afrika Mashariki Mhe. Jesca Erio ameshukuru
ujio wa kiongozi huyo na kuahidi kuendeleleza uhusiano mzuri kati ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki na Serikali ya shirikisho la Ujerumani na
Taasisi zake kama GIZ pamoja na mashirika yanayojishughulisha na masuala
ya haki za binadamu.Baada ya wiki mbili Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete anatarajia kuwa mwenyekiti wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
No comments:
Post a Comment