Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es
salaam, Said Meck Sadiki amewaomba wakazi wa jiji la Dar es salaam kujitokeza
kwa wingi katika mapokezi ya Rais wa Shirikisho la Ujerumani Mh.Joachim
Gauck anayetarajiwa kuwasili nchini
Tanzania leo usiku kwa ziara ya kikazi ya siku tano.
Akizungumzia ujio wa
rais huyo ofisini kwake leo jijini Dar
es salaam Mh. Meck Sadiki amesema kuwa rais Joachim Gauck na msafara wake
atawasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere majira
ya saa 2.30 usiku na kulakiwa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete.
Ameeleza kuwa mapokezi
rasmi ya rais huyo yatafanyika kesho katika viwanja vya Ikulu majira ya saa 3
asubuhi ambapo rais huyo akiwa na mwenyeji wake atapata fursa ya kukagua
gwaride maalum lililoandaliwa kwa ajili yake na Jeshi la Wananchi wa Tanzania
na kupigiwa mizinga 21.
Amesema kuwa akiwa
nchini Tanzania Rais Joachim Gauck atakuwa na mazungumzo ya faragha na Rais
Jakaya Kikwete, Ikulu jijini Dar es salaam na baadaye kufanya mazungumzo na
baadhi ya viongozi wa Vyama vya hiari, uongozi wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani pamoja na kukutana na
wafanyabiashara wa Dar es salaam.
Amefafanua kuwa
Februari 4, 2015, Rais huyo ataelekea Zanzibar ambapo atakutana na kuwa na
mazungumzo na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein na viongozi wengine wa
Serikali.
Aidha kabla ya
kuhitimisha ziara yake nchini Tanzania
Februari 6, 2015 rais huyo wa Shirikisho la Ujerumani atatembelea mbuga
ya wanyama ya Serengeti ,Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mahakama ya Kimataifa ya Haki za Binadamu
jijini Arusha.
No comments:
Post a Comment