Picha na Aron Msigwa- MAELEZO.
……………………………………………………………………………………….
Na.Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Abdallah Kigoda
amezindua rasmi Bodi ya Uongozi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na
kuitaka bodi hiyo kufanya kazi zake kwa kuzingatia sheria na
kushirikiana na menejimenti ya chuo hicho kuweka mikakati na mipango ya
maendeleo itakayokiwezesha chuo hicho kuendelea kutoa huduma bora kwa
wananchi.
Akizungumza na viongozi na wajumbe wa bodi hiyo leo jijini
Dar es salaam, Dkt. Kigoda amesema serikali inayo imani kubwa na
Mwenyekiti na wajumbe wa Bodi hiyo walioteuliwa na kwamba watatimiza
majukumu yao kikamilifu na kukiwezesha chuo hicho kufikia malengo na
matarajio ya watanzania ya kuendelea kuzalisha wataalam bora wa fani
za biashara.
“Ninaamini kuwa Bodi niliyoizindua leo itasimamia shughuli
za chuo hiki kwa kufuata misingi ya uadilifu,utawala bora na kuongeza
chachu ya kuleta huduma bora kwa wananchuo na umma” Amesisitiza Dkt.
Kigoda.
Amesema viongozi na wajumbe wa Bodi walioteuliwa
wanalojukumu la kusimamia ustawi wa chuo hicho wakiwa chombo cha juu cha
utoaji wa maamuzi na usimamizi wa masuala mbalimbali ya chuo hicho
ikiwemo uidhinishaji wa matumizi ya chuo yanayoendana na mapato ya chuo,
uteuzi wa Mkuu wa Chuo na watumishi wengine na uidhinishaji wa viwango
vya ada.
Akizungumzia mabadiliko ya chuo hicho toka kuanzishwa
kwake mwaka 1965 Dkt. Kigoda amesema yamehusisha mabadiliko makubwa ya
mitaala ya kufundishia ili kuwafanya wanafunzi na wahitimu waweze
kupanua ufahamu wao kwa kuwa na uwezo wa kukabiliana na ushindani wa
soko la ajira kwa kuongeza fursa za ajira katika sekta ya umma na
binafsi pamoja kuwajengea uwezo wahitimu waweze kujiajiri wenyewe.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema
akizungumza wakati wa kuwakaribisha wajumbe walioteuliwa chuo hapo
amesema kuwa wao kama viongozi wa chuo hicho wataendelea kusimamia
msingi wa kuanzishwa kwa chuo wa kuendelea kuzalisha wataalam bora
katika nyanja za biashara na sekta ya uendeshaji viwanda nchini.
Amesema kuwa wao kama menejimenti ya chuo hicho
watashirikiana na uongozi na wajumbe wa bodi iliyoteuliwa kusimamia
rasilimali na miundombinu ya chuo hicho ili kiendelee kutoa huduma bora
kwa wanafunzi na wananchi wengi Zaidi kwa wakati.
Naye Makamu mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi ya Chuo hicho
Prof. Eleuther Mwageni akizungumza kwa niaba ya uongozi na wajumbe wa
bodi iliyoteuliwa amesema kuwa Bodi iliyoteuliwa itatekeleza majukumu
yote yaliyoanishwa kwa mujibu wa sheria.
No comments:
Post a Comment