Waziri
wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu (wa pili kushoto)
akimsikiliza kwa makini Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Saudi Arabia
Dk. Abdulrahman Al-Zamil (wa tatu kushoto) jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Wengine katika picha kutoka kulia ni Mshauri wa Ushirikiano wa
Kimataifa wa Mamlaka ya Wanyamapori ya Saudia Mohammad Sulayem; Katibu
Mkuu wa Maliasili na Utalii Dk. Adelhelm Meru na Balozi wa Tanzania
nchini Saudi Arabia Prof. Abdillah Omari.
Waziri
wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu (kushoto) katika mazungumzo
na Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Saudi Arabia Dk. Abdulrahman
Al-Zamil jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Mhe.
James Lembeli (kushoto) akikaribishwa na Mwenyekiti wa Chemba ya
Biashara ya Saudia Dk. Abdulrahman Al-Zamil jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Waziri
Kivuli wa Maliasili na Utalii Mhe. Peter Msigwa (kushoto) akikaribishwa
na Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Saudia Dk. Abdulrahman Al-Zamil
jijini Riyadh, Saudi Arabia.
Ujumbe
wa Serikali ya Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii
Mhe. Lazaro Nyalandu (wa tano kushoto) ukiwa katika picha ya pamoja na
Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara ya Saudia Dk. Abdulrahman Al- Zamil (wa
sita kushoto) mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina ya pande
mbili jijini Riyadh, Saudi Arabia. Wengine pichani kutoka kushoto ni
pamoja na Mkurugenzi wa Wanyamapori Herman Keraryo; Mkurugenzi Mkuu
TANAPA Allan Kijazi; Mhe James Lembeli; Mhe Peter Msigwa; Katibu Mkuu
Maliasili na Utalii Dk. Adelhelm Meru pamoja na maafisa kutoka Chemba ya
Biashara ya Saudia.
Na Pascal Shelutete, TANAPA
Waziri
wa Maliasili na Utalii Mhe. Lazaro Nyalandu amewakaribisha
wafanyabiashara kutoka Saudi Arabia kuwekeza katika sekta ya utalii
nchini ambayo ina fursa nyingi za uwekezaji. Nyalandu alitoa wito huo
kufuatia mazungumzo yake na Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabiashara ya
Saudi Arabia Dk. Abdulrahman Al-Zamil yaliyofanyika Riyadh, Saudi Arabia
jana.
Waziri
Nyalandu ambaye anaongoza ujumbe wa Wizara ya Maliasili na Utalii
nchini Saudia alibainisha kuwa mazingira ya uwekezaji nchini yanavutia
na kutaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na ujenzi wa hoteli na loji za
kisasa zitakazoweza kuvutia watalii wengi zaidi katika maeneo ya mijini
pamoja na ndani ya maeneo ya uhifadhi.
Alisema
kuwa utalii wa Tanzania unakua kwa kasi nzuri kutokana jitihada
zinazofanywa na serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kutangaza
vivutio vya utalii na kuwa juhudi hizo lazima ziende sambamba na
upatikanaji wa huduma bora za malazi. “Upatikanaji wa huduma nzuri za
malazi ya bei nafuu utasaidia kuvutia watalii wengi zaidi nchini na kwa
maana hiyo tunawakaribisha kuja kuzitumia fursa zilizopo ili kuweza
kukuza uchumi wa nchi yetu”, alisema Nyalandu.
Waziri
Nyalandu ambaye anaongoza ujumbe wa Wizara ya Maliasili na Utalii
nchini Saudia, alisema kuwa Tanzania ni ya pili ulimwenguni baada ya
Brazil kwa kuwa na vivutio vizuri vya asili vya utalii na kuwa
rasilimali hizi zinapaswa sasa kutumiwa vema ili kuinua uchumi na njia
pekee ni pamoja na kuvutia wawekezaji na mitaji kutoka Saudia ili
kufikia azma hiyo.
Kwa
upande wake Dk. Al-Zamil aliahidi kuwashirikisha wafanyabiashara
wenzake kutikia wito huo na kwa kuanzia timu ya wafanyabiashara pamoja
na mawakala wa utalii watafika nchini katika siku chache zijazo ili
kuona namna gani wataweza kuzitumia fursa zilizopo kikamilifu. Aidha,
katika eneo la utalii Al- Zamil alisema kuwa Chemba yake itafanya kila
liwezekanalo kubadilisha mtazamo wa Wasaudia wanaotembelea kwa wingi
maeneo mbalimbali ya utalii duniani ili waweze kuitembelea Tanzania na
kujionea vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana nchini.
Aidha,
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dk. Adelhelm Meru alisema
kuwa serikali itaandaa Kongamano Maalum la Uwekezaji nchini Saudi Arabia
ili kuweza kutangaza fursa mbalimbali zzilizopo nchini ambazo
zikitumika vema zinaweza kuinua uchumi wa taifa.
Hivi
sasa Tanzania inategemea idadi kubwa ya watalii kutoka Mataifa ya Ulaya
na Amerika na kwamba japokuwa idadi ya watalii kutoka nchi za kiarabu
haizidi 15,000 kwa mwaka, bado jitihada za utangazaji na uwekezaji
zikifanywa vizuri idadi ya watalii kutoka mataifa ya kiarabu itaweza
kuongezeka nchini.
Ujumbe
wa Tanzania unajumuisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii
Dk. Adelhelm Meru; Balozi wa Tanzania Saudi Arabia Prof. Abdillah Omari;
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira Mhe. James Lembeli, Waziri kivuli wa Maliasili na Utalii Mhe.
Mchingaji Peter Msigwa; Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa Allan Kijazi
pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Herman Keraryo
No comments:
Post a Comment