(Picha na: Genofeva Matemu – Maelezo, Dodoma)
…………………………………………………………………………………..
Na: Genofeva Matemu
Vijana kutoka kikundi cha Iringa
Promise Keepers chenye wanachama 6 wanaojishughulisha na ufundi Selemala
wameishukuru Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaosimamiwa
na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuwapatia mkopo wa
shilingi laki tatu mwaka 2007 ambao umeinua na kusababisha mradi wa
kikundi kupanuka na kuwa mkubwa.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti
wa kikundi hicho Bw. Rashid Magule walipotembelewa na wawezeshaji
kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na maafisa
kutoka ofisi ya Mkoa wa Dodoma kukagua miradi ya vijana leo Mkoani
Dodoma.
“Kikundi cha Iringa Promise
Keepers kinaishukuru Serikali kwa kutufaidisha na mkopo wa shilingi laki
tatu kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Vijana tuliopatiwa mwaka 2007 ambao
ulikua kama mtaji katika kikundi chetu hivyo kupanuka na kuwa na mtaji
wa shilingi milioni nne unaotuwezesha wanakikundi kupata kipato cha
kuweza kuendesha maisha yetu” alisema Bw. Magule.
Hata hivyo Bw. Magule ameiomba
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
kuendelea kukipatia mkopo kikundi chake kwani bado wanakikundi
wanahitaji kujiendeleza zaidi na kuwaendelezo vijana wenzao wanaohitaji
utaalamu kutoka kwao hivyo kuomba kupatiwa mkopo wa shilingi milioni
mbili kwa ajili ya maendeleo ya kikundi hicho.
Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha
Vijana Sasanda Mbeya kilichopo chini ya Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo Bw. Laurean Masele amewapongeza wanakikundi kwa
jitihada kubwa walizozifanya na kuweza kutumia mpoko mdogo waliopata
kusimamia na kuendeleza mradi wao kwa kushirikiana.
Bw. Masele amewashauri wanakikundi
kufanya kazi kwa ushirikiano huo huo huku wakisimamia malengo
waliyokusudia kwa kutumia ujuzi walionao kwani vijana wakiwezeshwa
wanaweza.
Naye Afisa Maendeleo ya Vijana
Mkoa wa Dodoma Bw. Tumsifu Mwasamale amewapongeza wanakikundi wa Iringa
Promise Keepers kwa maendeleo waliyonayo na kuwataka kutafuta eneo lao
binafsi kwa ajili ya shughuli zao kwani mradi wao unahitaji nafasi kubwa
na ya wazi itakayosaidia kuonyesha bidhaa wanazozalisha katika jamii.
No comments:
Post a Comment