Mbunge
wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter msigwa (Chadema) amewataka viongozi
walioshinda uchaguzi wa serikali za mitaa kupitia vuguvugu la Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutolipiza visasi dhidi ya wenzao wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) walioshindwa.
Alisema hatua yoyote ya kulipiza visasi inaweza kupoteza
imani ya wananchi dhidi ya Ukawa hasa katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa
Oktoba mwaka huu.
Mchungaji Msigwa, aliyasema hayo wakati akihutubia wananchi
katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Ruanda Nzovwe
jijini Mbeya.
Mkutano huo ulilenga kuwashukuru wakazi wa jijini humo
kuwachagua wagombea wengi wa upinzani kwenye uchaguzi wa serikali za
mitaa uliofanyika Desemba 14, mwaka jana.
“Mlioaminiwa na wananchi mkachaguliwa kupitia Ukawa, hamna
sababu ya kulipiza visasi kwa yale yote mliyofanyiwa na viongozi wa CCM,
badala yake elekezeni nguvu zenu katika kuleta maendeleo ya wananchi,”
alisema na kuongeza:
“Kama mkijielekeza kwenye visasi, wananchi watapoteza imani
na nyie, hivyo malengo yetu ya kuing’oa CCM madarakani hayatafanikiwa.”
Alisema kuwa licha ya upinzani kupitia Ukawa kupata ushindi
huo, kila chama cha upinzani hususani Chadema na Watanzania, wana kazi
nzito ya kuhakikisha wanafanya mabadaliko ndani ya taifa kwa kuiondoa
CCM madarakani.
Asema kuwa bila mabadaliko ya kiutawala, taifa litaangamia
hivyo akawataka watanzania kuikabidhi nchi kwa wapinzani ili walete
mabadiliko katika elimu, afya, uchumi na kurejesha heshima kwa usalama
wa taifa.
Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina
la Sugu, alisema chanzo cha vurugu na migomo inayoibuka katika maeneo
mbalimbali hususani kwenye majiji ni askari Polisi na mgambo kutumiwa
vibaya na watawala.
Alisema, Chadema ikishinda na kupata madiwani wengi kwenye
Uchaguzi Mkuu ujao itavunja kitengo cha mgambo ili wananchi waishi kwa
amani ndani ya jiji hilo.
“Chadema tukishika halmashauri ya Mbeya, kitu cha kwanza
kukiondoa kitengo cha mgambo wa jiji kwani wanatumika vibaya na ndio
chanzo cha vurugu kati yao, machinga na mama ntilie,’ alisema.
Kwa upande wake, Mwanamuziki wa muziki wa kizazi kipya ambaye
pia ni kada wa Chadema, Joseph Haule maarufu kwa jina la ‘Professa
Jay’, pamoja na kushiriki harakati za kupigania haki za raia kupitia
muziki, sasa amejikita katika akiwa siasa mwanachama wa Chadema.
“Mimi ni mkazi wa pale Mikumi Morogoro, nimeingia kwenye
siasa ili kupigania haki kwa watanzania wote, nimetangaza nia ya
Ubunge….. na pale Mikumi ilikuwa kichaka cha CCM lakini sasa
tumekisambaratisha na kuizika kabisa CCM,” alisema.
No comments:
Post a Comment