Meneja
Mkuu wa Tanzania House of Talent, Mwita Mwaikenda akizungumza kuhusiana
na maadhimisho ya miaka kumi ya THT, kulia ni mwakilishi wa kampuni ya
MOSAIC, Deo Masagati ambao ndio wadhamini wa shuguli hiyo, na kushoto ni
mwanamziki Peter Msechu ambaye ndio mwongozaji wa burudani siku ya
tamasha.
Mbunifu
wa Mavazi, Ally Remtullah akiongea na waandishi kuhusu uzinduzi wa
mradi wa ubunifu na ushonaji unaonzishwa na THT. Kulia ni Peter Msechu,
na kushoto ni Lameck Ditto.
Mkuu wa Masoko wa THT, Michael Nkya akiongea na waandishi wa habari juu ya maadhimisho ya miaka kumi ya THT
………………………………………………………………
- Kufungua kampuni ya ushonaji na ubunifu wa mavazi
Kituo cha kuzalisha na kukuza
vipaji, Tanzania House of Talent, kinatarajia kuadhimisha miaka kumi
toka kuanzishwa kwake hapo tarehe 31/1/2015 Escape 1 jijini Dar es
Salaam.
THT ilianzishwa mwishoni mwa mwaka
2005 kwa lengo la kuwasaidia vijana wenye vipaji, lakini wasio na uwezo
wa kujiendeleza wenyewe, kwenye sekta ya sanaa hapa nchini, na toka
wakati huo kituo kimekuwa na mafanikio makubwa na mchango wa pekee
kwenye kukuza sanaa ya muziki nchini.
Akizungumza wakati wa kuzindua
maadhimisho hayo ambayo yatakuwa kwa mwaka mzima, Meneja Mkuu wa Kituo
hicho, Mwita Mwaikenda alisema ni heshima kubwa kuweza kusherehekea
miaka kumi toka imeanzishwa kwani wameweza kufanikisha mambo mengi
makubwa.
‘Tulianzisha kituo hiki miaka kumi
iliyopita kwa hakika tukiwa hatuna chochote zaidi ya imani yetu kwenye
vipaji vya vijana, na tulianza hatuna hata sehemu ya maana, lakini leo
miaka kumi baadaye vijana zaidi ya 3000 wamefaidika na kituo hiki kwa
namna moja au nyingine na wameweza kumudu maisha yao na familia zao
kutokea kuwa watoto wa mitaani’ alisema Mwita.
THT ikiwa imeanzishwa kama kituo
cha kusaidia watoto wa mtaani wenye vipaji, imeweza kukua kwa kipindi
cha miaka kumi, na sasa sio tu inazalisha na kukuza vipaji bali imekuwa
ikitoa huduma zote kuanzia kuratibu matamasha, kuandaa mpangilio wa
burudani, kutengeneza matangazo ya radio na televisheni pamoja na makala
na vipindi vya televisheni.
‘THT imeweza kuratibu burudani ya
matamasha mbalimbali kama FIESTA, Mkutano wa Smart Partnership, Sensa ya
mwaka 2013, Sherehe za miaka 50 ya Muungano pamoja na mikutano na
matamasha kadha wa kadha’ alisema Meneja Masoko wa THT, Michael Nkya.
THT imeendelea kukua kwa kuweza
kuanzisha studio yake ambayo imeweza kurekodi matangazo, nyimbo za
wasanii wote wa THT pamoja na wengine wengi kama Mdogomdogo na Number
One Remix ya Diamond, Me and You ya Ommy Dimpoz, Prokoto ya Victoria
Kimani na nyingine nyingi.
Kwa sasa THT inatengeneza vipindi
mbalimbali vya televisheni kama 69 Records, na vingine vingi
vinavyorushwa chaneli za nje huku pia ikijivunia kuwa na maktaba ya
nyimbo kubwa zaidi nchini.
‘Shukrani zetu za dhati kwa kweli
ni kwa serikali, hasa hasa Mheshimiwa Rais Kikwete, ambaye toka mwanzo
alikubali wazo na akaamini mziki unahitaji elimu ya peke yake, lakini
pia makampuni mbalimbali ambayo wamekuwa wakitupa kazi pamoja na vyombo
vyote vya habari kwa kutuunga mkono siku zote’ alisema Bwana Nkya.
Akielezea kuhusu mwelekeo wa kituo
baada ya miaka kumi, Mwita alisema anaamini kituo kimefanya kazi yake
tayari kwa kuweza kuchagiza sanaa ya muziki nchini, na sasa ni wakati wa
kuendelea kusaidia wadau au vituo vingine kama Mkubwa na Wanawe kufika
THT ilipofika.
‘Kimsingi mwaka huu ndio mwaka wa
mwisho kuendela kupokea wanafunzi wapya wa kuimba, na mpango wetu ni
kuendelea kukuza kituo kwa kuanzisha kampuni ya ushonaji na ubunifu wa
nguo kwa kutumia kitenge ambao tunaamini utatoa ajira kwa vijana wengi
zaidi hapa nchini’ alisisitiza Mwita.
Kampuni ya ubunifu na ushonaji kwa
kutumia vitenge, tayari ishaanza mchakato wake kwa kuhusisha wadau wa
biashara ya vitenge, na mbunifu mahiri Ally Remtullah, mwanamitindo
Flaviana Matata wakiwa ndio walezi na wasimamizi wa mradi ambao utaanza
na wabunifu wanaochipukia Neyonce pamoja na Adam Mchovu.
‘Kwa kuanza mradi utapeleka
wabunifu nchini China ili wakajifunze zaidi juu ya ubunifu na kuongeza
ubora kwenye kazi zao, wakirudi tunaamini wataweza kuwafundisha vijana
wengi zaidi, na kutimiza lengo letu la kuwasaidia vijana kujiajiri’ alimaliza Mwita.
No comments:
Post a Comment