Na Mwandishi Wetu
OFISA Habari Umoja wa Mataifa
(UN), Bi. Usia Nkhoma Ledama amesema bado lengo la kupunguza kiwango cha
umasiki lililokuwa katika malengo ya milenia yaliyomalizika mwakani
litaendelea kuwa changamoto kwa nchi mbalimbali kutokana na hali ya
utekelezaji wake. Bi. Nkhoma ametoa ufafanuzi huo Uwanja wa Mnazi Mmoja
jijini Dar es Salaam katika Uzinduzi wa Kampeni ya Chukua Hatua Dhidi ya
Umasikini 2015 zilizozinduliwa leo Dar es Salaam.
Alisema jitihada zinafanyika na
nchi mbalimbali zipo katika viwango tofauti katika kulitimiza lengo
hilo. “…Kwanza lazima tukubali kuwa ni lengo ambalo linachangamoto kubwa
kiutekelezaji karibia nchi nyingi, hivyo litaendelea kupewa uhimizaji
kiutelekezaji hata katika malengo yajayo,” alisema Bi. Nkhoma.
Hata hivyo akizungumzia suala la
kupunguza maambukizi ya Ukimwi alisema bado ni lengo ambalo
linachangamoto kubwa licha ya kwamba maambukizi mapya bado yapo lakini
nguvu kubwa imewekwa katika kupunguza hayo maambukizi mapya. “…Tupunguze
maambukizi mapya na tusiwe tena na watu wanaoendelea kufa kutokana na
maambukizi ya Ukimwi…hili bado ni lengo ambalo linaendelea kufanyiwa
kazi kwa nguvu kubwa pia linahitaji msukumo na jitihada za mtu mmoja
mmoja, lakini pia kama nchi, kama taifa na jumuiya za kimataifa katika
kupambana nalo,” alisema.
Alisema lengo la kupunguza vifo
vya watoto wachanga na wajawazito bado ni lengo lenye changamoto, hii ni
kutokana na suala hili utekelezaji wake unahitaji rasilimali ya kutosha
kuhakiisha tuna hospitali, vituo vya afya na klinii za kutosha
kuhakikisha tuna sehemu za kutolea huduma kwa akina mama na watoto.
Hospitali zetu kuwa na vifaa na wahudumu wa afya waliosomea na kubobea
kwenye huduma hizo.
“Bado kuna changamoto lakini
tutatumia changamoto zilizokuwa katika utekelezaji kwa miaka iliyopita
kutatua changamoto za sasa kimaboresho zaidi. Kupunguza umasikini sio
suala la sera bali ushiriki wa wananchi mmoja mmoja oale alipo, pia hili
ni suala mtambuka kutokana na kutegemeana na sekta nyingine. Mfano
mkulima hawezi kupunguza umasikini kama hana pembejeo, kama hana
miundombinu imara ya kusafirisha mazao yake kutoka shambani hadi sokoni
na pia kupata soko la uhakika anapoingiza mazao yake sokoni.”
Alisema ili kupambana na hili
inabidi kujengwa mazingira kuhakikisha kila mmoja anashiriki kupambana
na malengo hayo, mfano fursa za ajira na fursa za kujiajiri haiwezekani
kila mtu kuajiriwa so inabidi kuandaliwa wengine kujiajiri wenyewe.
“…Sio lazima kila mtu aajiriwe kila mtu anakipaji chake katika
uzalishaji kinaweza kutumika kwa kuendelezwa na kujikuta anafanya
vizuri,” alisema.
Kampeni ya Chukua Hatua Dhidi ya
Umasikini 2015 zimezinduliwa rasmi leo jijini Dar es Salaam na
kushiriisha makundi mbalimbali, wazee, vijana, wanafunzi wa Msingi na
Sekondari, watu wenye ulemavu na makundi mengine husika.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment