Na: Genofeva Matemu
Vijana wa Mkoa wa Kilimanjaro wameziomba Halmashauri zao
kuhamasisha vijana kuanzisha Saccoss za Wilaya zitakazowawezesha vijana
kuwekeza na kuwasaidia kuomba mkopo wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana
utakaopitishiwa katika Saccoss hizo ili waweze kujiajiri wenyewe na
kuondokana na umasikini.
Hayo yamesemwa na Vijana wakati wa kufunga semina ya
uhamasishaji kwa vijana kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na kuiomba
Wizara yenye dhamana na vijana kujitolea kutoa elimu kwa vijana mara kwa
mara itakayowawezesha vijana kujitambaua na kuwajengea uwezo.
Akizungumza baada ya kufunga semina hiyo Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga Bw. Jamhuri David Willium ameishukuru
timu kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuweza kufika
katika Halmashauri yake na kuwaomba kujitolea pale Wilaya
itakapowahitaji kwa mara nyingine kwa ajili ya kuelimisha vijana wa
Mwanga.
Bw. Willium amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ipo
karibu na vijana wake, imeweza kuwaunganisha vijana kwenye vikundi
mbalimbali na kuwashirikisha vijana katika shughuli mbalimbali za
maendeleo zinazofanywa na Halmashauri hiyo hivyo kuwahaidi vijana
kushughulikia ufunguaji ya Saccoss ya vijana kwa maendeleo ya vijana wa
Mwanga.
“Vijana ni taifa la leo, sisi kama viongozi wa Halmashauri tupo
tayari kushirikiana nao kwa jitihada zote kwani umuhimu wa Saccoss ya
vijana katika Halmashauri tunaufahamu hivyo tutajitahidi kusimamia suala
la ufunguzi wa Saccoss ya vijana itakayowawezesha kujitegemea kwa
maendeleo yao na maendeleo ya Wilaya ya Mwanga”, amesema Bw. Willium.
Naye mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo Bibi. Ester Riwa ameuomba uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Mwanga kushirikiana na wadau wengine wanaojishughulisha na masuala ya
vijana kuwasaidia Vijana wa Mwanga huku wakitumia vyombo vya habari
kuelimisha vijana na kubadili fikra za vijana kuwa chanya.
No comments:
Post a Comment