Meneja wa sera na ushirikishaji wa TANGO, Zaa Twalangeti, akizungumza na Modewjiblog
kwenye mahojiano maalum yaliyofanyika katika ofisi za TANGO jijini Dar
es Salaam. Kulia ni Mratibu wa kitaifa wa Mtandao wa Asasi zisizo za
kiserikali za haki za binadamu kusini mwa Afrika(SAHRINGON), Bi. Martina
Kabisama.
Na Mwandishi wetu
ASASI
isiyokuwa ya kiserikali ya TANGO imezindua kampeni kubwa ya kuelimisha
umma wa Tanzania kuhusu malengo 17 ya maendeleo endelevu kwa lengo la
kuyafanya kumilikiwa na wananchi ili yapigane kuondoa umaskini na kuleta
ustawi wa jamii.
Uzinduzi huo ulifanyika mjini Dar es salaam.
Aidha
katika uzinduzi huo wamesema kwamba ili kutoa nafasi ya sauti za
wananchi kusikika na kufikishwa kwa viongozi wa kimataifa ambao
watakutana baadae mwaka huu, asasi zisizokuwa za kiserikali zitaitisha
mkutano mkubwa ambapo watu wa kawaida wataambiwa wasema wanachohitaji,
shughuli itakayofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja Januari 15 mwaka huu
kuanzia saa tatu asubuhi.
Kwa
mujibu wa Meneja wa sera na ushirikishaji wa TANGO, Zaa
Twalangeti,kuanzishwa kwa kampeni hiyo kabla ya kuanza kwa utekelezaji
wake mwakani kwa miaka 15 kumefanyika baada ya kutambua kasoro
zilizojitokeza katika kampeni ya malengo ya milenia (MDG) ambayo
ushiriki wa wananchi haukulengwa na matokeo yake kuna kasoro katika
utekelezaji.
Alisema
ingawa malengo ya milenia yalikuwa manane, kasoro iliyoijitokeza ambayo
inasababisha utekelezaji wake kuwa wa chini ni hali ya kuwatumia
viongozi kuyazungumza na kuyatekeleza kiasi cha kufanya wananchi wasione
kama ni mali yao.
Alisema
haja ya kupata mafanikio katika malengo yaliyofikiriwa sasa ambayo ni
17 inatokana na kutaka wananchi kuyajua, na pia kusema wao katika
malengo hayo 17, ambayo yatafanyiwa kazi na Umoja wa Mataifa Oktoba
mwaka huu kabla ya kuanikwa wazi kwa jamii ya kimataifa, yapi wanayataka
na kipaumbele chao nini.
Aidha
alisema kwamba malengo hayo ni muongozo wa dunia wa kupunguza umaskini
na kwamba wakati mataifa mengine yamefurahisha ushiriki wa wananchi
kuanzia ngazi za chini hadi juu , watanzania wamejikuta hawajui wala
kufikiria kuyatekeleza kutokana na ukweli kuwa hawakushirikishwa na
hivyo malengo hayo hayakuwa yao bali ya viongozi.
Alisema
kiukweli muongozo huo wa awali wa kukabili umaskini (MDGs) haukuweza
kufikiwa na watanzania kwani hata upunguzaji wa umaskini umefanyika kwa
asilimia 3 tu, huku tatizo la vifo vya wajawazito na watoto likiwa
tatizo na elimu kubaki kuwa ya kubabia kutokana na matatizo lukuki
yaliyozunguka elimu kufuatia kukosekana kwa tathmini.
Mratibu
wa kitaifa wa Mtandao wa Asasi zisizo za kiserikali za haki za binadamu
kusini mwa Afrika(SAHRINGON), Bi. Martina Kabisama akifafanua jambo kwa
mwandishi wa Modewjiblog wakati wa mahojiano maalum katika ofisi za TANGO jijini Dar es Salaam.
“umefikia
lengo la kuandikisha, lakini mbona unazalisha watu wasiojua kuandika,
kusoma na kuhesabu;mbona mdondoko ni mkubwa” alisema.
Alisema
kampeni ya kuelewa malengo hayo ambayo wameiita Action 2015 yamelenga
kuhakikisha kwamba malengo ya sasa ni vyema yakamilikiwa na wanananchi
ili watafute dawa ya changamoto zinazowakabili.
Tawalangeti
alisema kufikisha ujumbe kwa wananchi watatumia mikutano,makongamano,
majadiliano, vipindi vya mazungumzo katika radio, televisheni na
mitandao ya kijamii.
Sisi
kama watanzania lazima tuupige vita umaskini, tunaupigaje vita? unasema
pato limekua. limekuaje kama pengo kati ya matajiri na maskini linazidi
kuongezeka? alisema Martina Kabisama ambaye aliongeza kwamba hata maisha
yanaonesha kuongezeka kwa umaskini kwa sababu sasa kuna majengo ya bati
vijijini lakini hakuna chakula.
Alisema
zamani unakuta nyumba mbaya lakini kuna kuku , kuna maziwa kuna chakula
cha kutosha tukasema kuna umaskini ulikithiri leo hii unaenda hukohuko
vijijini kuna nyumba nzuri lakini nyumba hiyo haina mifugo wala akiba ya
chakula.
Aidha
kuonesha kutopea kwa umaskini pia alitolea mfano wa elimu ambapo
alisema wakati zamani wakubwa wenye hela na viongozi walikuwa wakifanya
kila hila kuhakikisha watoto wao wanaenda shule za serikali, siku hizi
hawahangaiki kwa kuwa wanatumia uwezo wao kupeleka watoto katika shule
za kulipia wakiacha shule za serikali magofu.
Meneja wa sera na ushirikishaji wa TANGO, Zaa Twalangeti akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na mtandao wa habari wa Modewjiblog jijini Dar es Salaam.
Martina
Kabisama, ambaye ni mratibu wa kitaifa wa Mtandao wa Asasi zisizo za
kiserikali za haki za binadamu kusini mwa Afrika (SAHRINGON) alisema
kampeni imelenga kuweka msingi imara wa mambo yanayotakiwa kufanywa huku
wananchi wakiyaelewa.
Alisema
miaka 15 ya malengo ya maendeleo endelevu kuanzia mwakani hadi mwaka
2030 bila kuwa na mipango madhubuti na wananchi kukumbatia malengo
yenyewe kwa kuyafanya yao na kufuatilia utekelezaji wake kwa namna
wanavyohitaji hasa kutokana na ukweli kuwa mwaka huu Tanzania imepata
bahati ya kuwa na matukio mawili makubwa yanayoashiria maamuzi mazuri
kusaidia msingi wa maendeleo.
Mambo hayo mawili ni katiba pendekezwa na pia uchaguzi mkuu.
Alisema
matukio hayo mawili yatasaidia sana kujua nani wanawekwa madarakani ili
kama maamuzi yalikuwa mazuri inakuwa rahisi kudai utekelezaji wa
malengo hayo kama yalivyoeleweka.
Alisema
ni muhimu kuelewa malengo endelevu ya maendeleo kwa kuwa hatima ya
Watanzania ipo mikononi mwa watanzania wenyewe pamoja na maelekezo ya
jumuiya ya kimataifa na viongozi waliopo nchini.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mwishoni mwa mwaka
huu viongozi wa kimataifa watakutana kujadili malengo ya maendeleo
endelevu (SDGs) baada ya kukamilisha malengo ya milenia ambayo hata
hivyo bado kuna mataifa yanahitaji kuendelea kutoka pale yalipoishia.
TANGO
wamesema moja ya mambo muhimu ambayo wanafikiria yanastahili kufanyiwa
kazi ni kuendelezwa kwa MDG1 ya kuondoa umaskini uliokithiri na njaa na
MDG8 ya namna ya utekelezaji. Alisema malengo hayo, bado yapo kizani na
ikizingatiwa kwamba malengo ya maendeleo endelevu yanatakiwa
kushirikisha wananchi.
Pamoja
na ushirikishaji wa wananchi TANGO imesema kwamba malengo ya SDGs
yanahitaji serikali kuwa na dhamira ya kukabiliana na umaskini kwa
kushirikisha wadau wote, huku bunge ambalo husimamia sera na utekelezaji
wa sheria likiwezeshwa kutekekeza wajibu huo.
No comments:
Post a Comment