Mkurugenzi
Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar
Karsan akionyesha gazeti la “Tuwasiliane” linalochapishwa na UTPC na
kusambazwa kwa wadau na maeneo mbalimbali ya jijini Mwanza kwa Mratibu
Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez
aliyetembelea makao ya ofisi hizo kwa ajili ya mazungumzo na kuboresha
ushirikiano baina ya Umoja wa Mataifa Umoja huo wa vilabu vya waandishi
wa habari nchini.
Na Mwandishi Wetu
WIMBI
kubwa la kuwa na vijana wasiokuwa na kazi limeelezwa kuwa tatizo
duniani kote na serikali mbalimbali zinatakiwa kuliangalia hilo kwa
undani na kulitatua.
Kauli
hiyo imetolewa na Mratibu wa Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa
nchini na Mwakilishi wa shirika la maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP),
Alvaro Rodriguez.
Mratibu huyo alisema hayo katika mazungumzo yake na Mkurugenzi Mtendaji
wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC) Abubakar Karsan.
Alisema
ukosefu wa kazi kwa sasa ni tatizo la kijamii na kwamba, shauri hilo
lisipoangaliwa kwa makini linaweza kuwa chanzo cha matatizo makubwa ya
usalama na amani katika taifa.
Alvaro Rodriguez ambaye alifika katika ofisi za UTPC kuangalia mambo
yanayofanyika katika ofisi hiyo wakati akiwa ziarani Mwanza wiki
iliyopita, alisema kama tatizo la ajira litaendelea kuwapo, vijana
wanaoathirika wanaweza kufikiria njia nyingine isiyo ya kistaarabu
kufanikisha mambo yao.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC), Abubakar
Karsan akizungumza na Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na
mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini,
Alvaro Rodriguez (kushoto) aliyeambatana na Mshauri wa masuala ya haki
za binadamu kutoka ofisi ya mratibu mkazi wa UN Tanzania, Bi. Chitra
Massey (kulia) alipotembelea makao makuu ya ofisi hizo jijini Mwanza.
Alisema
Umoja wa Mataifa unaendelea kushirikiana na serikali mbalimbali
kuhakikisha kwamba tatizo la ajira kwa vijana linamalizwa ili jamii
isiingie katika mtafaruku utakaokosesha amani na usalama na hivyo
kusimamisha maendeleo yaliyofikiwa katika jamii.
Bila
kutaja makundi ya kigaidi yanayotikisa dunia kwa sasa kama Al – Qaeda na
washirika wake Boko Haram, Al – Shabab, Islamic State of Iraq na Levant
(ISIL) alisema makundi mengi ya kigaidi duniani yanatokana na vijana
kutojua wafanye nini na mazingira waliyonayo na hivyo kuwa rahisi
kushawishika.
Alisema
makundi ya hatari mara nyingi ni ya vijana ambao wanashindwa kupata
riziki au hawajui wafanye nini kupata riziki na serikali zimewaacha bila
kuwaangalia.
Aidha
alisema Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia kuhakikisha kwamba masuala
muhimu yanayowezesha maendeleo kama demokrasia yanazingatiwa ili
kuiwezesha jamii kufanya maamuzi sahihi ya vile wanavyotaka kupanga
maendeleo yao.
Mtaalam
wa Mahusiano na Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa (UN) Tanzania, Hoyce
Temu (kulia) akichangia jambo wakati wa mazungumzo na Mkurugenzi
Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari (UTPC) Abubakar
Karsan makao makuu ya ofisi za umoja huo jijini Mwanza.
Alisema
Demokrasia huwezesha wananchi kujua namna wanavyoweza kutengeneza
mustakabali wao katika masuala ya ustawi wa jamii na maendeleo huku haki
zao za msingi zikilindwa.
Mapema
Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC, Bw. Karsan alimwambia mratibu huyo mambo
ambayo yamefanywa na umoja huo na changamoto walizokumbana nazo kwa
kuzingatia mpango mkakati wake wa mwaka 2011-2013.
Umoja
huo ambao ulianzishwa mwaka 1996 na kusajili na wizara ya mambo ya
ndani kama taasisi isiyokuwa ya kiserikali (NGO) mwaka uliofuata,
umefanikiwa kuanzisha mfuko wa kusaidia vyombo vya habari kwa jina la
Daudi Mwangosi, aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari wa
Iringa (IPC).
Mratibu
Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez
akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa
Habari (UTPC), Abubakar Karsan wakati wa mazungumzo ya kuboresha
mahusiano baina ya mashirika ya umoja wa mataifa na umoja wa vilabu vya
waandishi wa habari nchini Tanzania.
Aidha
alimwambia kwamba wamefanikisha mafunzo ya kuongeza umahiri wa uandishi
wa habari na pia kuwaelezea umma juu ya uhuru wa vyombo vya habari.
Pia
alielezea mafanikio yaliyopatikana katika kampeni za kuelimisha umma na
kuelewana miongoni mwa wadau mbalimbali wa sekta ya habari.
Alisema
hata hivyo bado wanaendelea na kampeni yao kutaka mabadiliko ya malipo
kwa waandishi wa habari wanaojitegemea ambao ndio wanatoa mchango wa
asilimia 75 hadi 80 za habari zinazotangazwa au kuchapishwa.
Aidha
wanaendelea kutoa mafunzo ya kanuni na maadili kwa waandishi wa habari
na kuendelea kukabiliana na tatizo la usalama katika mpango mkakati wa
mwaka 2015 – 2019.
Katika
ziara hiyo ya kanda ya Ziwa, mratibu huyo aliambatana na mshauri
mwandamizi wa masuala ya haki za binadamu Dk Chitralekha Massey na
Mtaalamu wa mawasiliano wa umoja huo hapa nchini HoyceTemu.
No comments:
Post a Comment