NA: VERONICA KAZIMOTO
14 JANUARI, 2015
KAMPALA.
WITO umetolewa kwa washiriki
wote wa Mkutano wa Kumi wa Maendeleo ya Takwimu Afrika kuelendelea kutoa
takwimu sahihi na kwa wakati ili kuleta maendeleo yanayokusudiwa ya
kiuchumi na kijamii barani Afrika.
Wito huo umetolewa jana na
Waziri Mkuu wa Uganda Mhe. Dkt. Ruhakana Rugunda wakati akifungua
Mkutano wa Kumi wa Maendeleo ya Takwimu Afrika uliofanyika katika Ukumbi
wa Mikutano wa Speke Munyoyo Kampala, Uganda.
Dkt. Rugunda amesema kuwa, ili
kupata maendeleo kwa haraka, ni lazima takwimu zitolewe kwa wakati na
ziwe sahihi kwa ajili ya kusaidia kupanga mipango mbalimbali ya
maendeleo.
“Ili Bara la Afrika liweze
kuendelea kwa haraka, linahitaji takwimu sahihi na zinazotolewa kwa
wakati ili takwimu hizo zisaidie katika kupanga mipango mbalimbali ya
maendeleo”, amesema Waziri Mkuu Rugunda.
Dkt. Rugunda ameongeza kuwa ili
kuweza kufanikisha hilo, kuna umuhimu kwa nchi za Afrika kusaidia
program mbalimbali za uzalishaji wa takwimu na matumizi yake kwa ajili
ya kupanga mipango ya maendeleo.
Kwa upande wa Waziri wa Fedha wa
Uganda Matia Kasaija amesema kuwa, ili kuweza kulinganisha takwimu za
nchi mbalimbali, ni vyema takwimu zinazozalishwa zikafuata mbinu bora za
uzalishaji wa takwimu.
Matia Kasaija amesema mbinu bora
za uzalishaji wa takwimu ni zile zinazofuata viwango vinavyopendekezwa
na Umoja wa Kimataifa – Kitengo cha Takwimu.
Mkutano wa Kumi wa Maendeleo ya
Takwimu Afrika umewakutanisha washiriki takribani 400 kutoka nchi
mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania. Mkutano huu ni wa siku tatu na
unatarajia kumalizika kesho tarehe 15 Januari, 2015.
No comments:
Post a Comment