Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limeizuia timu ya Polisi Mara kutumia Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma kwa mechi zake za Ligi Daraja la
Kwanza (FDL) kuanzia leo mpaka hapo itakapotangazwa vinginevyo.
Uamuzi huo umechukuliwa kutokana
na matukio ya vurugu na uvunjifu wa amani ambayo yamekuwa yakitokea
kwenye mechi za FDL zinazochezwa kwenye uwanja huo, ikiwemo ile ya
Jumamosi iliyopita dhidi ya Mwadui ya Shinyanga ambapo waamuzi
walipigwa.
Kamati zinazohusika zitakutakana
hivi karibuni kupitia matukio yote ya utovu wa nidhamu kwenye FDL, na
hatua kali zitachukuliwa kwa wahusika ikiwemo na viwanja ambavyo
vimekuwa na sifa ya vurugu.
Vyama vya mpira wa miguu vya mikoa vina wajibu wa kutoa ulinzi wa kutosha viwanjani wakati wa mechi.
RAUNDI YA PILI TAIFA CUP WANAWAKE JUMAMOSI
Mechi za kwanza za raundi ya pili
ya mashindano ya Taifa ya mpira wa miguu kwa wanawake (Taifa Cup
Wanawake) zinachezwa wikiendi hii (Januari 17 mwaka huu) kwenye miji
minane tofauti nchini.
Timu tisa zilizofuzu kutoka raundi
ya kwanza baada ya mechi za nyumbani na ugenini akiwemo mshindwa bora
(best loser) zitaungana na Ilala, Kinondoni na Temeke kucheza raundi ya
pili. Mechi za marudiano za raundi hiyo zitachezwa Januari 21 mwaka huu.
Hatua ya robo fainali
itakayochezwa Januari 26 na 27 mwaka huu pamoja na nusu fainali na
fainali ya michuano hiyo inayodhaminiwa na Proin Promotions itafanyikia
jijini Dar es Salaam.
KOCHA NOOIJ KUTAJA STARS MABORESHO
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart
Nooij anatarajia kutaja kikosi cha Maboresho kitakachoingia kambini
Januari 18 mwaka huu kujiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Rwanda
itakayofanyika Januari 22 mwaka huu jijini Mwanza.
Nooij atataja kikosi hicho kwenye
mkutano na waandishi wa habari utakaofanyika kesho (Januari 15 mwaka
huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF), Uwanja wa Karume.
RAMBIRAMBI MSIBA WA STEPHEN NSOLO
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa ya msiba wa Katibu Mkuu
wa zamani wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Shinyanga (SHIREFA)
uliotokea jana (Januari 13 mwaka huu) jijini Mwanza.
Msiba huo ni pigo kwa wadau wa
mpira wa mpira wa miguu kwani wakati wa uhai wake, Nsolo alitoa mchango
mkubwa akiwa kiongozi. Aliongoza SHIREFA akiwa Katibu kuanzia mwaka 1975
hadi 1994.
Kabla ya hapo alikuwa Katibu wa
Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Shinyanga kwa kipindi cha miaka kumi.
Pia aliwahi kuwa mwamuzi wa daraja la kwanza na kamishna wa mpira wa
miguu kwa muda mrefu.
TFF inatoa salamu za rambirambi
kwa familia ya marehemu, SHIREFA na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu
Tanzania (FRAT) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi
hiki kigumu kwa msiba huo.
Marehemu anatarajiwa kuzikwa leo
(Januari 14 mwaka huu) katika makaburi ya Shinyanga Mjini. Bwana alitoa,
Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.
No comments:
Post a Comment