Tunachukua
fursa hii kurekebisha taarifa tuliyoitoa jana katika tovuti yetu yenye
kichwa cha habari "Wahisani wafurahishwa na hotuba ya JK".
Kimsingi,
katika mawasiliano yake na Idhaa ya Kiswahili ya BBC kwa njia ya barua
pepe, Balozi wa Finland nchini Tanzania, Sinikka Antila, ambaye pia ni
mwenyekiti wa Wahisani wanaochangia bajeti ya Tanzania (Budget Support
Development Partners) alieleza kuwa wamekuwa wakifuatilia hatua
zinazochukuliwa kuhusiana na madai ya "uchotwaji" wa fedha kutoka akauti
ya Tegeta Escrow.
"Wahisani walipokea hatua ya kuwasilishwa
ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (PCCB) Bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC), kuwasilishwa kwa ripoti ya PAC Bungeni,
mjadala uliofuatia, maazimio yaliyopitishwa na Bunge", Balozi Anitila
aliifahamisha BBC.
Washirika wa maendeleo (DPs) wanaamini kuwa
mifumo ya uwajibikaji ya Tanzania itamudu kushughulikia swala hili
kikamilifu na tunatazamia kupatikana kwa majibu ya uhakika kutoka
serikalini.Balozi Antila alifafanua kuwa wamefuatilia maelezo aliyoyatoa
Rais Kikwete katika hotuba yake kwa taifa.
"Wahisani wamepokea
taarifa aliyoitoa Rais tarehe 22 Disemba, 2014, akitambua maazimio
yaliyopitishwa na Bunge na kuthibitisha baadhi ya hatua na uchunguzi
zaidi. Wakati bado tunatathimini hali ya mambo, wahisani bado
wanaendelea na mashauriano na Wizara ya Fedha, na uamuzi wowote wa
kuruhusu fedha zitolewe utafanyika kwa mawasiliano na Waziri
anayehusika”, alieleza Balozi Antila.
Pia alisema mpaka sasa,
kiasi cha dola za kimarekani milioni 84, au takriban asilimia 15 ya
fedha zilizoahidiwa kusaidia bajeti (Budget Support funds) kwa mwaka
2014/15 zilikwishatolewa, lakini fedha hizo hazina uhusiano na hatua
zinazochukuliwa sasa. Bali ni jumla ya fedha ambazo zimetolewa kwa nyati
tofauti.
Tunaomba radhi kwa Balozi Sinikka Antila wa Finland na pia wasomaji wa tovuti ya bbcswahili.com kwa usumbufu uliojitokeza
No comments:
Post a Comment