Mtandao
wa Korea kazkazini ulizimika kwa masaa kadhaa na kuzua uvumi kwamba
huenda Marekani imeanza kulipiza kisasi kufuatia madai ya uhalifu wa
mtandaoni uliofanyiwa kampuni moja ya filamu nchini Marekani.
Kulingana
na kituo cha habari cha AFP haijulikani ni nani ama nini kilichozima
mtandao wa Pyongyang ,lakini wataalam wa mitandao wamesema kuwa mtandao
wa taifa hilo ulizima usiku kucha kutoka siku ya jumatatu hadi jumanne.
Wachanganuzi wa mtandao nchini
Marekani Dyn Research wanasema kuwa kampuni nne za mtandao za Pyongayang
zinazopata mtandao wake kutoka kwa kampuni ya mawasiliano ya Uchina,
China Unicom zilikuwa zimezimwa kwa masaa tisa na dakika 31 kabla ya
huduma kurejea siku ya jumanne.
Kampuni ya Dyn Research imesema
kuwa mitandao michache iliopo Pyongyang huenda ikaathiriwa na kukatika
kwa umeme lakini vile ilivyozimika kunazua mjadala kwamba huenda
mitandao hiyo ilizimwa kutoka nje.
Rais wa Marekani Barrack Obama
na shirika la ujasusi la FBI limeishtumu Korea Kazkazini kwa kushambulia
mitandao ya kampuni ya filamu ya Sony Pictures ambayo ilitishiwa na
kuilazimu kuahirisha maonyesho ya filamu inayomkejeli rais wa taifa hilo
Kim Jong-un.
Maafisa wa Washington wamekataa kutoa tamko kuhusu
madai kwamba kuzimwa kwa mtandao wa Korea Kazkazini ni hatua ya kwanza
ya rais Obama aliyeonya kwamba atalipiza kisasi shambulizi hilo.
No comments:
Post a Comment