Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa vijiji
vipatavyo 45 vilivyopo katika mkoa wa Mara vinatarajiwa kuunganishiwa na
huduma ya umeme kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Profesa Muhongo aliyasema hayo katika ziara yake ya siku sita
katika mkoa wa Mara lengo likiwa ni kukagua na kuzindua miradi ya umeme
vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) awamu ya pili
kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Nchini (Tanesco)
Profesa Muhongo alisema ziara yake iliyohusisha wilaya za Musoma
Vijijini, Tarime, Rorya, Bunda na Serengeti ililenga pia kubaini na
kukagua mahitaji ya umeme katika wilaya hizo ili vijiji vilivyokosa
umeme kwenye awamu ya pili viingizwe katika awamu nyingine ya umeme
vijijini.
Alieleza kuwa Wizara imekuwa ikisambaza umeme katika kila Mkoa
na Wilaya za Tanzania kwa awamu kulingana na mahitaji na idadi ya watu
katika maeneo hayo.
Alisema kwa sasa umeme unaosambazwa upo katika awamu ya pili ambapo awamu ya tatu itakuja baada awamu ya pili kumalizika.
Alisema vipaumbele vinavyotolewa katika uunganishaji wa umeme
vijijini Profesa Muhongo alitaja kuwa ni maeneo yenye huduma muhimu za
kijamii kama vile mashule, vituo vya afya, makanisa, misikiti, ofisi za
vijiji na kata, na sehemu zenye miradi ya maji.
“Lengo letu kuu kwanza ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata
huduma za jamii kwa urahisi na baada ya kuboreshwa kwa huduma hizo
tunakwenda kuwaunganishia umeme wananchi mmoja mmoja, ikiwa ni mkakati
wa kuhakikisha maisha ya wananchi yanaboreshwa kupitia nishati ya
umeme”, alisema Profesa Muhongo
Profesa Muhongo aliongeza kuwa ili nchi yoyote duniani iweze
kupiga hatua katika ukuaji wa uchumi wake, inahitaji nishati ya umeme na
kuongeza kuwa kwa kutambua hilo serikali imeanza kwa upande wa vijijini
ili wananchi hao waweze kujiingizia kipato kupitia ajira za kujiajiri.
Alifafanua kuwa wananchi wa vijijini kupitia nishati ya umeme
wanaweza kuwekeza kupitia mashine za kusaga nafaka, kukamua mafuta,
kuhifadhi vyakula vya kuuza kwenye majokofu na kujipatia fedha na
kuongeza kuwa itapunguza wimbi la watu kukimbilia mjini kutafuta ajira
Wakati huohuo Mwenyekiti wa kijiji cha Bukabwa Thomas Makwera
alisema kuwa wananchi wa kijiji chake wamekuwa wakikabiliwa na
changamoto ya kutokuunganishiwa umeme kwa muda mrefu hali inayopelekea
maendeleo ya kijiji hicho kudorora.
Hata hivyo aliongeza kuwa wakandarasi wamekuwa wakionekana
wakisimika nguzo za umeme hali inayotia hamasa kwa wananchi ya kutaka
kujua ni lini wataunganishiwa na huduma ya umeme.
Akijibu swali la Mwenyekiti huyo Profesa Muhongo alimtaka
mkandarasi anayesimamia mradi huo kutoka kampuni ya Derm Electrical
Huseni Ayubu kutoa ufafanuzi ambapo mkandarasi huyo alieleza kuwa kazi
ya kusimika nguzo pamoja na kuunganisha umeme inatarajiwa kukamilika
mapema Februari mwakani.
Naye Profesa Muhongo aliwataka wanakijiji wa Bukabwa
kuchangamkia fursa ya kuunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi
27,000. wakati mradi wa umeme ukiwa bado upo katika kijiji chao.
Alisema kuwa lengo la utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini
kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni kuhakikisha kuwa vijiji
vyote ambavyo umeme umepita lakini havijaunganishiwa vinaunganishiwa ili
kuhakikisha vijiji vyote vilivyopitiwa umeme vinapata umeme kwa kufuata
utaratibu huo.
No comments:
Post a Comment