Na Mwandishi Wetu,
MAKAMPUNI saba yamethibitisha
ushiriki wao katika tuzo za bodi yenye uongozi bora katika sekta ya
kibenki na bima zijulikanazo kama Best Board Leadership Awards (BBLA),
zilizopangwa kufanyika Januari 30, mwakani katika Hoteli ya Serena
jijini Dar es Salaam.
Taarifa kwa vyombo vya habari
iliyotolewa jana na Mratibu wa tuzo hizo, Bi. Neema Gerald, imezitaja
benki zilizothibitisha kushiriki katika tuzo hizo kuwa ni pamoja na
Benki ya Posta (TPB), Benki ya Exim na Benki ya CRDB.
Aliyataja makampuni ya bima
yaliyothibitisha kushiriki katika tuzo hizo kuwa ni Heritage Insurance,
Alliance Insurance Corporation, Alliance Life Assurance na Strategis
Insurance (T) Limited.
Tuzo hizo zimelenga kutambua uongozi bora wa Bodi za Wakurugenzi katika Sekta ya Kibenki na Bima.
Bi. Neema aliendelea kuzisihi
kampuni zaidi zilizopo katika sekta ya kibenki na bima kujitokeza kwa
wingi ili kujisajili katika tuzo hizo zilizoandaliwa chini ya mwamvuli
wa Chama cha Mabenki Tanzania (TBA) na Chama cha Makampuni ya Bima
Tanzania (ATI).
“Ningependa kutoa shukrani zangu
za dhati kwa makampuni yaliyoonyesha mwamko wa kushiriki kwenye tuzo
hizi katika hatua hizi za mwanzo za maandalizi,” alisema na kuongeza:
“Tuzo hizi zitatoa fursa ya
ufahamu wa jinsi gani bodi bora inaweza kusaidia taasisi kupata
mafanikio na kufikia utendaji bora hususani katika eneo walilobobea
kiutalaam. Hivyo ningependa kuziasa kampuni zaidi kujitokeza na
kushiriki,” alisema Bi. Neema.
Alibainisha kuwa zoezi hilo,
tathmini na upangaji wa mwisho wa matokeo utafanywa na jopo la majaji
waliobobea na wenye rekodi bora za kiutendaji.
Tathmini hiyo italenga zaidi
katika ufanisi wa Bodi ya Wakurugenzi katika suala la utawala wa
taasisi, usimamizi wa fedha na uwezo wa kuiongoza dira ya taasisi kwa
ujumla wake.
Maeneo mengine ni umakini wa bodi katika uwazi, uwajibikaji, utendaji, na ufuataji wa hatua madhubuti na utendaji wake.
Alitaja maeneo mengine ambayo bodi
itafanyiwa tathmini kuwa ni utoaji wa mitazamo yakinifu ya bodi katika
kusisitiza umuhimu wa utendaji wa mtaji watu katika ngazi ya bodi na
kuweka mbele vigezo vitakavyowezesha utendaji bora zaidi wa bodi,
“alisema.
Bi. Neema aliwataja wadhamini wa
tukio hilo la kipekee kuwa ni pamoja na Capital Plus Internaional
Limited, Real PR Solutions Limited, Afrimax Strategic Partnerships
Limited, Serena Hotel na IPP Media.
“Tumeona umuhimu wa kutambua na
kuthamini mchango unaotolewa na wakurugenzi wa bodi katika taasisi
zao.Tunaamini kuwa katika kila mafanikio ya taasisi ya kifedha, nyuma
yake kuna bodi ya wakurugenzi imara na makini. Sasa, sifa hizo ambazo
wajumbe wa bodi wengi wanakua nazo zinapaswa kutambuliwa na kuthaminiwa,
“alisema.
Bi. Neema alisema kuwa ni
utamaduni uliozoeleka kwa Maafisa Watendaji Wakuu na Wakurugenzi Wakuu
pekee kuthaminiwa na kutambuliwa na waajiriwa au jamii nzima kwa ujumla.
“Ni wakati muafaka sasa kwa bodi zenye utendaji bora kutambuliwa na kuzawadiwa kikamilifu kwa jitihada zao,” alisema.
Bi. Neema aliongeza kuwa tuzo hizo
zimeanzishwa kwa wakati muafaka nchini kipindi ambapo sekta za Bima na
kibenki zinapitia mabadiliko makubwa huku makampuni mengi zaidi ya bima
yakijitokeza na masoko zaidi kuongezeka ili kufikia wateja wengi katika
nyanja zote za maisha.
“Kwa mabadiliko haya yanayotokea
wakati huu, hasa katika sekta ya fedha ambapo idadi kubwa ya makampuni
ya bima na benki yamekuwa yakifungua biashara Tanzania, wateja
wanahitaji kuwa na uhakika kuwa malipo yao ya bima yako salama na
wanaweza kupatiwa kwa wakati wowote”, alisema.
No comments:
Post a Comment