Jumuiya
ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) inampongeza
Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Profesa Jakaya Mrisho Kikwete kwa hotuba yake
nzuri iliyojaa ufafanuzi bayana wa masuala makubwa ya kitaifa, likiwemo
suala la Akaunti ya Escrow ya Tegeta, yaliyoleta mkanganyiko kwa
wananchi, aliyoitoa jana katika Ukumbi wa Diamond Jubilee alipozungumza
na wazee wa jiji la Dar es salaam.
Sisi
Vijana tunampongeza kwa kubariki na kuridhia hatua iliyochukuliwa na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa, Mheshimiwa Hawa Ghasia za kuwachukulia hatua sitahiki wakurugenzi
wazembe waliovuruga Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu.
Tunahimiza
utaratibu huo uwe endelevu kwa kuendelea kuwachukulia hatua kali
wakurugenzi ambao wanapata hati chafu za Ukaguzi pamoja na wale ambao
wanashindwa kutimiza wajibu wa kisheria wa kutenga asilimia tano (5) za
mapato ya Halmashauri kwa ajili ya maendeleo ya Vijana.
Pia, Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, (Mb) Mheshimiwa Anna Kajumulo Tibaijuka.
Tunamwomba
Mheshimiwa Rais kumteua Waziri mwingine ambaye atamudu wizara hiyo
ipasavyo kwa kutatua na kumaliza kabisa migogoro ya ardhi ambayo
imeendelea kusababisha vurugu, machafuko na maafa katika maeneo
mbalimbali hapa nchini kama vile Mvomero, Maswa, Kiteto. Tunapendekeza
apatikane Waziri ambae muda wake mwingi atakuwa katika maeneo hayo
akitafuta suluhu ya kudumu kati ya wafugaji na wakulima, baina ya
wafugaji, wakulima na hifadhi, na baina ya wananchi, hifadhi na
wawekezaji.
Pia,
tunavitaka vyombo vinavyoendelea na uchunguzi, kumaliza na kukabidhi
matokeo ya uchunguzi wao katika mamlaka husika mapema ili kutoa fursa
kwa maamuzi kufanyika kwa wakati.
Tunavitaka
vyombo hivyo kufanya kazi zake kwa weledi na uaminifu mkubwa ili jambo
hili lipate maamuzi sahihi lakini pia asionewe mtu na haki itendeke.
Na
mwisho tungependa kuwakumbusha wananchi na viongozi kuheshima mgawanyo
wa madaraka, na kuheshimu nguvu na mamlaka za kila mhimili wa Taifa,
tunaiomba Mamlaka ya Bunge iendelee na utaratibu wake katika
kuwashughulikia wale walio kwenye mamlaka zake ambao wamehusika katika
kadhia hii ya ESCROW na pia kuitaka mahakama na tume zake kuchukua hatua
kulingana na taratibu na miongozo yao.
Tunawaomba
Wananchi kuwa makini na kutoruhusu mijadala inayohusu suala hili
kutawaliwa na maslahi binafsi ya wafanyabiashara na wanasiasa, ambao
wameendelea kushawishi na kushinikiza maamuzi yanayolinda maslahi yao.
No comments:
Post a Comment