Siku moja baada ya kufukuzwa uwaziri, Mbunge wa Muleba Kusini
(CCM), Profesa Anna Tibaijuka amewasili jimboni kwake na kusema, “Bwana
alitoa na Bwana ametwaa.”
Profesa Tibaijuka alivuliwa uwaziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Rais Jakaya Kikwete juzi kutokana na
kuhusika kupokea fedha katika akaunti binafsi.
Baada ya kuwasili na kupokewa kwa maandamano,
Profesa Tibaijuka aliwaomba wananchi kukaa kimya kwa dakika moja ili
kumkumbuka katibu wake wa jimbo aliyefariki dunia wakati sakata hilo
likijadiliwa bungeni.
Profesa Tibaijuka aliyepokewa kwa msafara wa
magari kutoka Uwanja wa Ndege wa Bukoba, aliwaeleza wananchi kuwa
ilikuwa ni lazima kutafuta msaada kwa watu wengi ili aweze kuwasomesha
watoto anaowasaidia kielimu.
“Kuna suala la escrow, zamani kulikuwa na aspro
ambayo ilikuwa ni dawa ya kweli, sasa suala hili limefikia tamati
hamkunichagua ili nikawe waziri, ni sawa na kusema Bwana alitoa na Bwana
ametwaa,” alisema Profesa Tibaijuka.
Aliambatana na mtoto wa kike akisema ni mmoja wapo
wa wanafunzi wasio na uwezo anaowasomesha katika Shule ya Babro
Johanson, inayotajwa kuwa ndiyo iliyopokea Sh1.6 bilioni alizoingiziwa
katika akaunti yake binafsi, katika Benki ya Mkombozi.
Profesa Tibaijuka alitumia muda mfupi kuelezea
suala la kuhusishwa katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow akisema
Taifa lina changamoto ya kupata elimu bora na wapo viongozi wachache
kama yeye wenye moyo wa kusaidia masuala ya elimu.
“Teknolojia sasa imekua, naamini mlikuwa
mnafuatilia mambo yalivyokuwa yanakwenda, yalikuwa ni mambo makubwa,
kazi ya uwaziri nisingeipata bila nyinyi wananchi. Nilikuwa na majukumu
mengi, sasa nitapata muda wa kukaa jimboni.
“Taifa bado lina changamoto ya kupata elimu bora,
hiyo shule mnayoisikia ada yake kwa mwaka ni zaidi ya Sh4 milioni, hivyo
lazima nitafute mtu wa kunisaidia. Hakuna mtoto wangu hata mmoja
anayesoma kwenye shule hizo,” alisema Tibaijuka.
Huku hotuba yake ikikatizwa na watu waliokuwa
wakishangilia, Profesa Tibaijuka aliwaonya wanaotaka kulinyemelea jimbo
hilo kuwa yuko ‘fiti’ na anawasubiri kukutana nao ulingoni.
Alisema atakuwa tayari kufanya kazi katika maeneo
yanayoongozwa na vyama vya upinzani jimboni kwake akiamini kuwa pia wapo
wanachama wa CCM.
>>>Mwananchi
>>>Mwananchi
No comments:
Post a Comment