Umoja
wa katiba ya wananchi Ukawa umelitaka bunge lijalo liiwajibishe
serikali kwa kutoku tekeleza kikamilifu maazimio ya bunge huku
wakitishia kuandamana nchi nzima endapo waliohusishwa na tuhuma za
ufisadi wa Escrow hawatachukuliwa hatua za kisheria.
Mwenyekiti wa chama cha wananchi CUF Prof Ibrahim Lipumba ameyasema
hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha umoja huo ambapo amesema
sheria ya maadili inatakiwa itungwe upya na utaratibu wa viongozi
kutangaza mali zao uwe wa wawazi kwa wananchi na kuongeza kuwa
maandamano hayo yana lengo la kulaani ufisadi wa Escrow pamoja na
kushinikiza utekelezaji wa maazimio yote ya bunge.
Kwa upande wake katibu mkuu wa Chadema Dk Willbroad Silaa
akizungumza katika kikao hicho amesema kuwajibika peke yake haitoshi
badala yake hatua za kisheria zinatakiwa zichukuliwe ili kukomesha
vitendo hivyo ambavyo vimeonekana kujirudia mara kwa mara kutokana na
watu kutenda makosa na kuishia kujiuzulu ili hali kuna hasara ambazo
taifa limeingia.
Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi Mh James Mbatia ni miongoni mwa viongozi
wa Ukawa walioshiriki kikao hicho ambapo ametumia fursa hiyo kuwasihi
viongozi wa dini na viongozi wastaafu waliotumikia taifa kutumia siku
kuu ya Noel kupaza sauti zao katika kuhakikisha serikali inasimamia haki
na kwamba taifa lolote lenye migogoro haliwezi kupata ustawi wa jamii.
No comments:
Post a Comment