Mwenyekiti wa Baraza la
Michezo Bi Sharifa Khamis akizungumza na Wanahabari kuhusu Mashindano ya
kitaifa ya Riadha yatakayofanyika Disemba 26-27 , 2014 katika Ukumbi wa
wizara ya habari Kikwajuni mjini Zanzibar. Rais Shein anatarajiwa kuwa
Mgeni Rasmi wa Mashindano hayo.
Picha na Makame Mshenga.
……………………………………………………….
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi
katika mashindano ya Kitaifa ya Riadha ya wilaya ambayo yanatarajiwa
kufanyika katika kiwanja cha Amaani Disemba 26-27 mwaka huu.
Mashindano hayo yaliyodhaminiwa na Rais Shein kwa lengo la
kukuza sekta ya michezo nchini yametayarishwa na Baraza la michezo la
Taifa Zanzibar (BMTZ) kwa kushirikiana na chama cha Riadha (ZAAA)
Hayo yameelezwa leo na Mwenyekiti wa baraza la michezo Bi
Sharifa Khamis katika ukumbi wa wizara ya habari , utamaduni, utalii na
michezo huko kikwajuni wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari.
Amesema mashindano hayo yatakayozishirikisha Wilaya zote 10 za
Unguja na Pemba yatajumuisha wanariadha 250 ambapo michezo yote ya
riadha ikiwemo kukimbia masafa ya mita 100 , 200, 400, na 1500 kwa
wanawake na wanaume itafanyika.
Aidha ameongeza kuwa jumla ya vikundi 12 kutoka Kenya , Uganda na Tanzania Bara vimealikwa kushiriki Mashindano hayo.
Amefahamisha kuwa sambamba na Riadha pia kutakuwa na michezo ya kurusha mkuki , tufe, ,na kisahani.
Amebainisha kuwa Washiriki wa mashindano hayo watapatiwa huduma
zote za michezo bure ikiwemo malazi , mavazi ya michezo , chakula,
usafiri na zawadi zote za washindi za vikombe , medali na fedha taslim.
“Lengo kuu la mashindano hayo ni kuinua mchezo wa riadha
Zanzibar kuanzia vijijini , maskulini na maeneo mengine mbali mbali kwa
nia ya kutafuta vipaji vya wanariadha kutoka katika sehemu hizo ili
kuviendeleza vipaji hivyo “ alisema Bi Sharifa.
Amesema dhamira ya Rais wa Zanzibar ni kuona Zanzibar inarejesha
hadhi yake ya asili ya ubingwa katika michezo tofauti ambayo amesema
sifa hiyo imepotea kwa kipindi kirefu ikilinganishwa katika miaka 70.
Mashindano hayo nisehemu ya utekelezaji wa sera tya michezo
Zanzibar , ambayo inasisitiza kuwa vyama vyote vya michezo Zanzibar
vifanye jitihada za makusudi za kuinua michezo ili nchi iweze kupiga
hatua kubwa katika michezo.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment