BENKI ya Posta Tanzania (TPB) Tawi
la Mbeya, imetoa semina kwa Wajasiriamali wa mkoa ikiwa na lengo la
kuwaongezea ujuzi kwenye biashara zao. Semina hiyo ya siku moja
imefanyika kwenye ukumbi wa Mtenda Sunset mjini Mbeya na kufunguliwa na
Mkuu wa Wilaya, Profesa Norman Sigallah.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa
semina hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya
Posta, Sabasaba Moshingi, Mkuu wa Wilaya alitoa wito kwa wajisiriamali
kutoogopa kukopa kwenye mabenki ili kukuza mitaji yao na hatimae
biashara zao.
Prof. Sigallah alitoa changamoto
kwa wajasiriamali kuhakikisha biashara zao zinaubora unaotakiwa ili
kuweza kujenga imani na ushindani kwenye soko. Mkuu huyo wa Wilaya
alitoa changamoto kwa benki ya Posta kuweka dawati maalum la wataalam
watakaotoa ushauri kwa wajasiriamali pindi wanapokuja kuomba mikopo.
Aliwashauri wajasiriamali kujiepusha na makundi yenye muelekeo wa kuleta
vurugu na kuvunja amani, kwani ili kukua biashara yoyote inahitaji
amani na utulivi.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji
Mkuu wa Benki ya Posta, Sabasaba Moshingi, akijibu maswali mbalimbali
yaliyoulizwa na wajasiriamali hao zaidi ya 150 waliohudhuria semina
hiyo, alisema benki yake itaendelea kuboresha huduma zake hasa upande wa
mikopo, na pia kuangalia suala la riba zinazotozwa kwa aina tofauti ya
biashara.
“Benki yangu itaendelea kuangalia
ni namna gani tunaweza kuweka wataalam watakaotoa ushauri mzuri kwa
wajasiriamali ili kupunguza mlolongo mrefu wa nenda rudi kwa mkopaji.
Hii ni katika jitihada za kuhakikisha kuwa mkopaji anapata mkopo kwa
wakati ili kuwahi fursa iliyojitokeza,”.
Akiongea kwa niaba ya
wajasiriamali hao, Bi. Joyce Mkongo, aliishukuru sana benki ya Posta kwa
kutoa mafunzo hayo kwao,ambayo yamewafungua macho na kuwaondolewa woga
wa kutumia huduma za kibenki. Alisema wajasiriamali wengi wanasita
kuchukua mikopo kwa hofu kuwa mali zao zitataifishwa pindi
watakaposhindwa kulipa mkopo.
No comments:
Post a Comment