Na. Aron Msigwa –
MAELEZO.
Jamii imetakiwa
kuendelea kuunga mkono juhudi za
Serikali za ujenzi wa mabweni katika shule
za Sekondari zilizoko pembezoni
mwa miji hasa maeneo ya vijijini ili kukabiliana na tatizo la msongamano wa
wanafunzi mijini linalosababishwa na baadhi ya wanafunzi kushindwa kujaza
nafasi wanazopangiwa maeneo ya
pembezoni mwa miji kutokana na umbali.
Kauli hiyo ilitolewa
juzi jijini Dar es salaam na Katibu Tawala wa mkoa wa Dar es salaam Bi.
Theresia Mmbando wakati akizungumza na viongozi wa Elimu wa mkoa na walimu
wakuu wa Shule za Sekondari za mkoa wa Dar es salaam wakati wa kikao cha Kamati
ya Uchaguzi wa wanafunzi wa watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2015.
Alisema mwaka huu mkoa wa Dar es salaam umekuwa na kiwango cha
juu cha ufaulu kitaifa kwa kuwa na wanafunzi
wanaokidhi vigezo vya kuendelea na masomo ya sekondari kwa kiwango cha asilimia
78 ukifuatiwa na mkoa wa Kilimanjaro ambao umepata asilimia 69.
Alifafanua kuwa kati ya
wanafunzi 60,709 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi
mwaka huu , wanafunzi 59,577 ambao ni sawa na asilimia 98.14 waliofanya mtihani huo, wavulana wakiwa 28,419
na wasichana 31,158.
Bi. Mmbando alibainisha
kuwa kati ya hao watahiniwa 1,132 sawa na asilimia 1.86 katika mkoa wa Dar es
salaam hawawakuweza kufanya mtihani huo kutokana sababu mbalimbali zikiwemo
utoro, vifo, ugonjwa na sababu nyinginezo.
Akizungumzia kuhusu ufaulu wa wanafunzi hao kimkoa alisema wanafunzi
46,434 sawa na asilimia 78 walifaulu mtihani huo na kuufanya mkoa wa Dar es
salaam kuongoza kwa kuwa na ufaulu wa juu kitaifa wavulana 22,389 na wasichana
24,086.
Alibainisha kuwa
wanafunzi 36,610 walichaguliwa katika chaguo la kwanza kujiunga na shule
mbalimbali za Sekondari za ndani na nje ya mkoa wa Dar es salaam na kufafanua
kuwa wanafunzi 9824 waliobaki sawa na asilimia 21 ambao nao wamefaulu watachaguliwa
katika chaguo la pili kufuatia baadhi ya wanafunzi waliochaguliwa katika chaguo
la kwanza kujiunga na shule zisizokuwa za serikali na nafasi zao kubaki wazi.
Katika kufanikisha
zoezi hilo Bi. Mmbando alieleza kuwa mkoa tayari umeunda timu tatu
zitakazofuatilia idadi ya wanafunzi watakaoshindwa kufika katika shule walizopangiwa kuanzia Januari 14, 2015 katika halimashauri
za Temeke, Ilala na Kinondoni ili nafasi zao zijazwe na wanafunzi wengine.
Kwa upande wake Afisa
Elimu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Raymond Mapunda akitoa tathmini ya mtihani
wa kumaliza Elimu ya Msingi uliofanyika nchi nzima mwezi Septemba mwaka huu alisema
mkoa wake ulifanya vizuri kutokana na juhudi za walimu pamoja na wanafunzi
kuuelewa vizuri mfumo wa ufanyaji mitihani uliotumika wa Optical Mark Reader
(OMR).
Alisema kuwa wanafunzi
wa shule 506 za jiji la Dar es salaam walifanya mtihani walitumia mfumo huo kwa
ufanisi mwanafunzi 1 alifutiwa matokeo yake kwa sababu za udanganyifu, 2
walipata alama 0 huku wavulana 10 na wasichana 10 kutoka wilaya ya
Ilala na Kinondoni waliibuka washindi wa nafasi 10 bora kitaifa.
No comments:
Post a Comment