Mbunge
wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete, wa kwanza kulia alipotembelea
ujenzi wa vyoo vya kisasa vinavyojengwa katika shule ya msingi
Changalikwa,wa pili kushoto mwalimu mkuu wa shule hiyo Juma Paulo na wa
kwanza kushoto ni mwalimu mkuu shule ya sekondari Lugoba Abdalaah
Sakasa.(Picha na Mwamvua Mwinyi)
………………………………………………………………………………
Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
WANAFUNZI wa shule ya msingi ya Changalikwa
,kata ya Mbwewe,chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wanatarajia
kuondokana na kero ya vyoo chakavu na kujisaidia maporini baada ya
halmashauri ya wilaya hiyo kuanza ujenzi wa matundu 6 ya vyoo .
Ujenzi huo umelengwa kugharimu kiasi cha sh.mil 10 zilizotolewa kupitia fedha za mradi wa usafi na mazingira huku ukitarajiwa kukamilika baada ya miezi miwili ijayo.
Vyoo
hivyo vitakapokamilika kutawezesha wanafunzi wa shule hiyo kuondokana na
adha ya kwenda kujisaidia maporini kama ilivyo kwasasa.
Akizungumzia
ujenzi wa vyoo hivyo juzi wakati mbunge wa jimbo hilo Ridhiwani kikwete
alipokwenda kutembelea ujenzi huo,mwalimu mkuu wa shule ya msingi
changalikwa Juma Paulo amesema kuwa vyoo vya awali vimechakaa
miundombinu yake hivyo haifai kwasasa kutumiwa na wanafunzi kwa kuhofia
kudondokewa na kuta ama madahara mengine.
Aidha
Paulo amesema, kutokana na uchakavu uliokithiri wa vyoo hivyo, baadhi
ya wanafunzi walikua wakilazimika kujisaidia porini hali ambayo inaweza
kusababisha magonjwa ya mlipuko.
Nae
mbunge wa jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete aliyetembelea ujenzi huo
alieleza kuwa shule hiyo ilipata msaada huo kutokana vikao mbalimbali
vya halmashauri kutambua tatizo lililopo ili kuwajengea wanafunzi
mazingira bora.
Amesema
kijumla tatizo la vyoo mashuleni si zuri kwa afya za wanafunzi sanjali
na walimu kwani linatishia afya za binadamu hivyo haina budi kutatua
hali ya uchakavu wa vyoo uliopo katika shule hiyo.
Ridhiwani
ameeleza kuwa yeye kama mbunge atasaidia kuweka tanki la kuhifadhia
maji ambalo litatumika kuvuna maji kwa ajili ya wanafunzi na walimu wa
shule hiyo ya msingi Changalikwa..
Shule ya msingi Changalikwa ina jumla ya wanafunzi 405,walimu 6.
No comments:
Post a Comment