Na Masanja Mabula -Zanzibar.
…………………………………………………………….
Balozi wa Ireland nchini
Tanzania, Fionnuala Gilsenan amevihimiza vyama vikuu vya siasa Zanzibar
kuendeleza utamaduni wa kuzungumza na kuzipatia ufumbuzi kasoro
zinazojitokeza ili Zanzibar iendelee kubaki katika hali ya amani, umoja
na mshikamano.
Ametoa ushauri huo alipofanya
mazungumzo na Makamu wa Kwanza was Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif
Sharif Hamad yaliyofanyika nyumbani kwake Mbweni, nje kidogo ya mji wa
Zanzibar.
Balozi Gilsenan amesema Zanzibar
imejipatia sifa kubwa kutokana na maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa na
vyama viwili hivyo vya CCM na CUF na baadaye kuweza kuundwa Serikali ya
Umoja wa Kitaifa.
Amesema Serikali ya Umoja wa
Kitaifa imeipatia sifa kubwa Zanzibar kutokana na mafanikio makubwa
yaliyojitokeza ikiwemo hali ya utulivu na kusababisha wananchi wa
Zanzibar kuwa wamoja na kuelekeza nguvu zao katika kujiletea maendeleo.
Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesifu mahusiano mema yaliyopo
baina ya Zanzibar na Ireland ambayo yamewawezesha wananchi kunufaika na
miradi mbali mbali ya maendeleo, kiuchumi na kijamii, ikiwemo ufugaji
wa ng’ombe wa kisasa kisiwani Pemba.
Maalim Seif amesema ipo haja
mahusiano hayo yaendelezwe katika nyanja nyengine, ikiwemo sekta za
biashara, kilimo, utalii na viwanda vidogo vidogo, maeneo ambayo amesema
yana mchango mkubwa katika kuinua uchunmi wa Serikali na wananchi mmoja
mmoja.
Akizungumzia Serikali ya Umoja
wa Kitaifa, Maalim Seif amesema utaratibu huo ni mzuri na umeonesha
mafanikio makubwa Zanzibar na hauna budi kuendelezwa katika ngazi zote.
Maalim Seif amesema
kinachohitajika hivi sasa ni elimu zaidi kwa viongozi hasa wa ngazi za
chini, kuanzia mikoa, Wilaya na Shehia ili waelewe umuhimu wa Serikali
ya Umoaj wa Kitaifa na waweze kutekeleza majukumu yao bila ya upendeleo
miongoni mwa wananchi wote.
Maalim Seif amesema miongoni mwa
kasoro zinazolalamikiwa sana ni baadhi ya wananchi wa Zanzibar wenye
sifa kunyimwa haki yao ya kupata vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi,
licha ya juhudi kubwa wanazozichukua kuviomba katika mamlaka husika.
Amesema kasoro kama hizo hazina
budi kushughulikiwa kwa haraka kuepusha dhana kuwa baadhi ya watu
wanabaguliwa kwa misingi ya itikadi za kisiasa.
Kuhusu hali ya uchumi Maalim
Seif amesema Zanzibar inapiga hatua licha ya kuwa sekta zake za kiuchumi
zikiwemo Utalii na zao la karafuu zimekuwa zikipata mabadiliko
kulingana na mabadiliko ya misimu.
“Unajua uchumi wetu unategemea
zaidi sekta za utalii na zao la karafuu, lakini sekta hizi hutegemea
misimu. Kwa mfano msimu huu wa karafuu tunaweza kupata mavuno mazuri
lakini misimu miwili inayofuata mavuno hupungua, na hivyo hivyo kwenye
sekta ya utalii”, Maalim Seif alimueleza balozi huyo.
Hata hivyo amesema wananchi
wamehamasika katika sekta hizo hasa zao la karafuu, baada ya kuona kuwa
zinawaletea tija, na kwamba jumla ya miche milioni moja ya mikarafuu
hutolewa kwa wakulima kila mwaka ili kuliendeleza zao hilo.
No comments:
Post a Comment