WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amesema anakubaliana na ombi la wakazi wa Nyanzwa na
Igunda wilayani Kilolo, mkoani Iringa kuhusu ujenzi wa bwawa la
kuhifadhia maji yatakayovunwa msimu wa mvua ili yasaidie kuongeza eneo
la mradi wa umwagiliaji.
Ametoa kauli hiyo
mwishoni mwa wiki wakati akiwahutubia wakazi wa vijiji vya Nyanzwa na
Igunda, mara baada ya kukagua mradi wa umwagiliaji wa Nyanzwa ambao ni
maarufu kwa kilimo cha vitunguu.
“Huu mradi ni wa siku
nyingi. Nimewauliza wataalamu niliokwenda nao wakasema ujenzi wa bwawa
ndiyo suluhisho pekee la kuokoa mradi huu na kwamba ni jambo
linalowezekana kama fedha zipo.”
Aliutaka uongozi wa mkoa
uandae mpango kazi na wauweke kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha ili
mradi huo uweze kuombewa fedha kwenye bajeti kuu ya Serikali. ia
aliwataka wakazi wa eneo hilo wakitunze chanzo cha maji kwa kuweka
mipaka ili watu wasikivamie na hatimaye kukiharibu.
“Tengeni eneo kwa kuweka
mipaka. Mkurugenzi simamia uwekaji wa mipaka kwenye chanzo hiki ili
tukilinde kwani uharibifu wa mazingira utakiharibu kabisa,” alisisitiza.
Akiwa katika ukaguzi wa
eneo la mradi, Waziri Mkuu alikutana na mkulima mmoja wa vitunguu Bw.
Furaha Ngalali (32) ambaye alimweleza kwamba mwaka jana alifanikiwa
kulima ekari tatu za vitunguu ambazo zilimpatia kiasi cha milioni 6/-
huku kila gunia akiwa ameliuza kwa sh. 70,000/-.
“Gharama kwa kila ekari
ni karibu sh. 600,000/- kwa hiyo kwa ekari tatu ni sh. milioni 1.8/-.
Tukivuna vitunguu tunaandaa bustani ya mbegu na pia humu tunapanda
maharage,” alisema Bw. Ngalali alpoulizwa Waziri Mkuu analima eneo hilo
mara ngapi kwa mwaka.
Alipoulizwa soko la
vitunguu wanapata wapi, Bw. Ngalali alisema wanunuzi huwa wanavifuata
huko huko Nyanzwa na kwamba wengi wao hutoka Dar es Salaam, Mbeya na
Songea. Kijiji cha Nyanzwa kipo umbali wa kilometa 36 kutoka Ruaha
Mbuyuni ilipo barabara kuu ya kuelekea Dar es Salaam na Mbeya.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amewataka wakazi wa vijiji vya Nyanzwa na Igunda wajikite
kwenye ufugaji wa nyuki kwani hauna gharama kubwa na unawawezesha
wananchi kuinua kipato chao kwa haraka.
“Wakati mkisubiri ujenzi
wa bwawa ili muongeze uzalishaji wa mbogamboga ni vema mkaangalia suala
la ufugaji nyuki… licha ya kutumika kama sehemu ya kujiingizia kipato,
pia ufugaji nyuki ni njia mojawapo ya utunzaji wa misitu,” alisema.
“Hapa mlipo kuna msitu
mkubwa wenye migunga na mibuyu mingi tu. Yote hii imechanua maua mengi
mno. Lazima tutumie uwepo wa misitu hii kama fursa ya kipekee ya
kujiingizia kipato kwa kuweka mizinga ya nyuki. Unaweza usipate mahindi
au vitunguu lakini asali ikawasaidia kuwapa kipato. Hivi sasa lita moja
ya asali imefikia sh. 15,000/- hadi sh. 20,000/- na tena mtapata nta
ambayo pia ina bei nzuri tu,” alisema.
Alisema kwa sasa asali
inauzwa kwa bei ghali kwenye nchi mbalimbali baada ya kuongezeka kwa
mahitaji yake na hasa ikizingatiwa kwamba inatumika kama dawa ya kutibu
magonjwa mbalimbali na pia kwenye baadhi ya vipodozi.
Mapema, akisoma taarifa
mbele ya Waziri Mkuu, Mtendaji wa Kijiji cha Nyanzwa, Bw. Hekima
Masanula alisema skimu ya umwagiliaji ya Nyanzwa ilijengwa mwaka 1960
wakati huo kwa kutumia banio la miti na magunia ya mchanga. Ilikuja
kuboreshwa miaka ya 90 kwa ufadhili kutoka Jumuiya ya Ulaya na Serikali
ya Sweden.
“Hata hivyo, skimu hii
ambayo inahudumia wakulima 3,469 wakiwemo wanaume 1,662 na wanawake
1,807; inakabiliwa na uhaba wa maji kwani ni hekta 256 tu ambazo
zinamwagiliwa kwa sasa wakati eneo lote la mradi ni hekta 940,” alisema
Bw. Masanula.
Alisisitiza ombi la
kujengewa bwawa kama njia pekee ya kuwakwamua wakazi hao kutokanana
shida ya maji inayowapata hasa wakati wa kiangazi.
No comments:
Post a Comment