Na Masanja Mabula -Pemba .
Mgogoro wa shamba kati ya Mwekezaji na wananchi wa Shehia ya
Makangale umemalizika ambapo pande hizo zimefikia makubaliano na
kuahidi kushirikiana kulinda na kudumisha amani pamoja na kukuza kipato
chao kupitia sekta ya Utalii .
Makubaliano hayo yamefikiwa mbele
ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Omar Khamis Othman ambapo Mwekezaji
Amit Ladwa amekubali kulipa fidia ya miti aina ya mivinje ambayo
imepandwa na wananchi katika shamba hilo .
Akizungumza kwenye kikao hicho
kilichofanyika kwenye ufukwe wa Vumawimbi liliko shamba , Mkuu wa Mkoa
wa Kaskazini Pemba Omar Khamis Othman ameiagiza Idara ya Misitu na
Maliasili zisizorejesheka Pemba kuharakisha kufanya tathmini na miti
hiyo ili wananchi walipwe fidia na Mradi huo uanze kutekelezwa .
Amesema kuwa ni jukumu la Idara
hiyo kuhakikisha kwamba inavifanyia tathmini vitu vyote vilivyomo katika
shamba hilo haraka iwezekanavyo ili mwekezaji alipe fidia inayostahili
kwa wananchi jambo ambalo litatoa fursa kwa ujenzi wa hoteli .
“Leo hii tumeshughudia
makubaliano yakifikiwa hapa , kilichobaki ni kwa Idara ya Misitu na
Maliasili zisizorejesheka kufanya tathmini ya vitu vyote vilivyomo ndani
ya shamba hili ili mwekezaji aweze kuwalipa wananchi fidia zao na
ujenzi wa mradi uanze kutekelezwa ” alisisitiza Mkuu wa Mkoa .
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa
amewataka wananchi wa shehia hiyo kumpa ushirikiano wa kila hali
mwekezaji huyo wakati wote wa utekelezaji wa mradi huo ikiwa ni pamoja
na ulinzi wa mali zake .
Mapema Mkuu wa Wilaya ya
Micheweni Jabu Khamis Mbwana amefahamisha kwamba makubaliano hayo
yamefikiwa kutokana na wananchi wa shehia hiyo kutambua umuhimu na faida
za sekta ya Utalii katika kukuza uchumi wao na Taifa kwa Ujumla .
Amesema kuwa kufikiwa kwa
makubaliano hayo ni ishara ya kuwepo na amani katika shehia hiyo na
kuwataka wananchi kumpokea mwekezaji huyo na kisha kushirikiana naye ili
aweze kusaidia klutatua baahi ya kero za kijamii .
“Makubaliano haya yamefikiwa
kutokana na wananchi wa shehia hii kutambua umuhimu na faida ya Sekta ya
Utalii katika kukuza uchumi wao na Taifa kwa ujumla lakini nawaomba
wananchi mpokeeni huyu mwekezaji na shirikianeni naye ” alitilia mkazo
Mkuu wa Wilaya .
Awali wananchi hao wameitaka
Serikali kutokuwa na hofu juu ya usalama wa mwekezaji huyo na kwamba
watashirikiana naye kuanzia mwanzo hadi mwisho wa utekelezaji wa mradi
huo .
“Kwa hili tunaiomba Serikali
kuondoa hofu juu ya usalama wa maisha ya mwekezaji pamoja na mali zake
sisi tupo pamoja naye na tutashirikiana muda wote wa utekelezaji wa
mradi huu ” alisema Kombo Ali Kombo kwa niaba ya wananchi wenzake .
Kwa Upande wake mwekezaji Amit
Ladwa ameelezea kwamba kipaombele cha kwanza cha ajira atakitoa kwa
wakaazi wa shehia hiyo na kuongeza kwamba atatoa mafunzo ya lugha mbali
mbali kwa vijana watakaokuwa tayari kufanya kazi hoteli hiyo ..
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa
ametembelea maeneo ambayo yanamigogoro ya ardhi likiwemo shamba la Mzee
Ali Said Ramadhaman (80) ambalo linadaiwa kupimwa bila ya mwenyewe
kushirikishwa na kisha kukabidhiwa Samiya Suluhu Hassan.
No comments:
Post a Comment