SERIKALI
Serikali imepata mkopo wa sh. bilioni 15 ambazo zitatumika kulipa kiasi
cha madeni ya mazao ya nafaka ambayo wakulima wanaidai kupitia Wakala
wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).
Hayo yamesemwa na Waziri
Mkuu Mizengo Pinda kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi
wa Mkoa wa Iringa akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo
katika mkoa huo.
Akizungumza na wananchi
mara baada ya kukagua Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo (SACCOS)
cha Mazombe kilichopo Ilula wilayani Kilolo, mwishoni mwa wiki, Waziri
Mkuu alisema katika kipindi cha mwezi huu, Serikali imepata mkopo huo
kutoka benki ya CRDB ambazo zimesambazwa kwenye mikoa mbalimbali ili
kuwalipa wakulima hao.
Alisema hadi kufikia
Machi mwaka huu, Serikali itahakikisha inamaliza kulipa madeni kwa
wakulima ambao waliuza mazao yao kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA).
Akifafanua kuhusu mgao
wa fedha hizo, Waziri Mkuu alisema kanda ya Arusha wamepata sh. bilioni
1.72/-; kanda ya Dodoma sh. bilioni 2.02/-; kanda ya Kipawa sh. milioni
632.3/-; kanda ya Makambako sh. bilioni 4.58/-; kanda ya Shinyanga sh.
milioni 238.85/-; kanda ya Songea sh. bilioni 1.97/- na kanda ya
Sumbawanga sh. bilioni 3.82/-.
Alisema fedha hizo
zimegawanywa kwenye vituo, vikundi na mawakala na kuongeza kuwa Serikali
kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika itatoa sh. bilioni 15
nyingine ili zigawanywe katika kanda na kumaliza kabisa madeni ya
wakulima.
Alitoa ufafanuzi huo
baada kutolewa malalamiko kuwa ucheleweshwaji wa malipo hayo kwa
wakulima umewafanya baadhi yao washindwe kurejesha mikopo kwenye taasisi
za fedha kwa wakati.
Alisema ucheleweshwaji
wa malipo hayo ulitokana na ziada ya chakula kwenye msimu wa kilimo wa
mwaka 2014 kuongezeka kwa kufikia zaidi ya tani milioni 1.3,
ukilinganisha na ziada ya tani 300,000 za msimu uliopita. “Serikali
ililazimika kununua mazao ya wakulima zaidi ya malengo yake… matokeo
hayo mazuri ya kilimo, yalitokana na msisitizo wa Serikali kuwekeza
kwenye pembejeo, mbegu bora pamoja na kuingiza nchini matrekta zaidi ya
1600.
Mapema, akisoma taarifa
ya chama hicho mbele ya Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa Mazombe SACCOS, Bw.
Yohanes Mwemtsi, alisema kucheleweshwa kwa marejesho ya mikopo
iliyochukuliwa na wakulima kunazorotesha maendeleo ya SACCOS hiyo kwa
kushindwa kujiimarisha kimtaji.
Alisema licha ya
changamoto hiyo, chama hicho kimeshatoa mikopo yenye thamani ya sh.
bilioni 4.3 kwa wanachama wake zaidi ya 1,300 huku kukiwa na ongezeko la
wanachama wapya kwa wastani wa asilimia 10 kila mwaka.
No comments:
Post a Comment