Ofisa
Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la Kimataifa la
Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini, Al Amin Yusuph,
akiwasilisha mada ya mchanganuo wa ufumbi wa changamoto mbalimbali
katika utekelezaji wa mradi wa kijiji cha kidigitali.
Na Mwandishi wetu, Bagamoyo
WADAU
mbalimbali wa elimu, afya, Tehama na masuala ya utamaduni na uchumi
ambao wamo katika mradi wa kijiji cha dijiti cha Ololosokwan kilichopo
wilayani Monduli Arusha wanakutana kwa warsha ya wiki moja ikiwa ni
sehemu ya mandalizi ya uwapo wa kijiji hicho nchini Tanzania.
Kwa
mujibu wa Ofisa Miradi ya Mawasiliano, Habari na Tehama wa Shirika la
Kimataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO) nchini Al Amin Yusuph
warsha hiyo imelenga kuangalia changamoto na namna ya kuzitatua ili
mradi kuwa na tija kwa wananchi wake.
Yusuph
alisema kwamba wadau hao wanapanga mkakati kuangalia vipaumbele na
changamoto katika utekelezaji wa mradi huo wa miaka mitatu.
Alisisitiza
kwamba kwa kuwa mradi huo utakuwa na mawasiliano ya kisasa, masomo kwa
njia ya Tehama, tiba kwa kutumia mtandao wadau wamekusanyika mjini
Bagamoyo kuangalia namna bora ya kuufanya mradi huo uwe endelevu hata
kama UNESCO na mbia wake Samsung watajiondoa huko mbeleni.
Aliwataja
baadhi ya wadau kuwa ni kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Wizara ya Afya na ustawi wa jamii, Samsung, Unesco, wanakijiji wa
Ololosokwan, waganga wa jadi wakunga, Taasisi ya elimu na Chuo cha
Ufundi cha DIT.
Alisema
changamoto ambazo zinaonekana ni lazima ziangaliwe ni pamoja na
matumizi ya lugha hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa wengi wa wananchi wa
Kimasai hawazungumzi Kiswahili fasaha.
“tunategemea
sana Tehama kufanikisha mradi huu, na lugha inayoweza kutumiwa ni
Kiswahili, sasa hili ni changamoto ni lazima kuangalia mawasiliano”
alisema Yusuph na kuongeza kuwa kuwapo kwa radio ya jamii kutachangia
kwa kiasi kikubwa kutoa nafasi ya wananchi wengi kujifunza Kiswahili.
Aidha
alisema kwamba mambo mengine ambayo yanaangaliwa katika warsha hiyo ni
matumizi ya Tehama (intaneti) na kutoa mafunzo ya namna ya kuhudumia na
kufanyia matengenezo mitambo mbalimbali iliyomo katika mradi huo.
Alisema
nia kubwa ya kukusanya wadau mbalimbali ni kuangalia utekelezaji wa nia
ya mradi ya kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo kwa jamii ya
kimasaii ambayo kwa sasa utamaduni na uchumi wake unatishiwa na
mabadiliko ya tabia nchi.
“Tunataka maendeleo haya yasaidiwe na mawasiliano. Tunaangalia jinsi ya kutumia mawasiliano kuleta maendeleo” alisema Yusuph.
Alisema
ni matumaini yao kwamba wabia wengine wa mradi huu ambao ni kampuni ya
simu ya Airtel watatumia uwezo wao kuhakikisha kwamba kijiji hicho
kinakuwa hewani muda wote kwa lengo la kurahisisha huduma zinazopatikana
kwa njia ya mtandao hasa tiba.
Aidha
alisema kwamba pamoja na kuleta maendeleo mradi huo unakusudiwa
kuhamasisha amani kati ya koo na makabila mbalimbali yaliyopo wilayani
Ngorongoro.
Katika
warsha hiyo ambapo wadau wamegawanyika makundi mbalimbali ili
kutengeneza hoja za kufanyia kazi kwa ajili ya kufanikisha masuala ya
elimu na afya.
Katika elimu wameangalia vikwazo ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni na watoto kuacha shule kwenda kuchunga mifugo.
Ili
kukabiliana na kiwango kikubwa cha kutojua kusoma na kuandika kipaumbele
kinachofikiriwa ni kuwafikia vijana hao wakiwa machungani kwa
kuwapelekea mafunzo kwa njia ya mtandao.
Afisa
Mipango wa Elimu wa Unesco, Jennifer Kotta alisema changamoto ya elimu
katika kijiji hicho na majirani ni kubwa na kwamba wanachofikiria ni
kutumia Tehama ambapo sasa watawafikia vijana kule waliko.
Aidha
wamepanga kufunza lugha ya Kiswahili na Kiingereza ili kutanua wigo wa
majadiliano wa wakazi wa eneo hilo na watalii wanaofika na kupenda
kununua kazi zao.
Warsha
hiyo iliyofunguliwa na Mkurugenzi Mkazi wa Unesco nchini inafanyika
wakati vifaa vya kutengeneza kijiji hicho vikiwa vimeshaondoka katika
bandari ya Dar es salaam.
Katika masuala ya Afya wadau wameangalia vipaumbele vinavyostahili sasa ikiwa ni pamoja na utunzaji wa mimba na mtoto.
Wamesema
wanawake wa kimasai wanafanya shughuli nyingi kuanzia ujenzi wa makazi
na ukamuaji wa maziwa hadi ulezi wa watoto na kusema katika mazingira
hayo wanahitaji sana elimu ya uzazi salama.
No comments:
Post a Comment