Ni Mnara wa kurushia matangazo wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) ulioko Bungi Wilaya ya Kati Unguja.
Ni chumba chenye mitambo ya kurushia matangazo (Transmitter) kilichopo katika Kituo cha Bungi Unguja.
Wa kwanza kulia ni fundi mkuu wa
kituo hicho Nd. Ali Aboud Talib akitoa maelezo ya kiufundi kwa Waziri wa
Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Mhe. Said Ali Mbarouk wa
kushoto.
Aliyenyoosha mkono ni Mkurenzi
Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) Nd. Hassan Abdalla Mitawi
akitoa maelezo kwa Waziri wa Habari Zanzibar.
Waziri wa Habari, Utamaduni,
Utalii na Michezo Zanzibar Mhe. Said Ali Mbarouk akikagua Jenereta
linalotarajiwa kutumika pindi umeme utakapokosekana kituoni hapo.
Waziri wa Habari, Utamaduni,
Utalii na Michezo Zanzibar Mhe. Said Ali Mbarouk akizungumza na
waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali mara baada ya kumaliza ziara
yake kituoni hapo.
…………………………………………………………………………..
Na Abdulla Ali Maelezo-Zanzibar
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Zanzibar Mhe.
Said Ali Mbarouk amesema zaidi ya shilingi milioni 100 za Kitanzania
zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa kituo kipya cha kurushia
matangazo cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC).
Hayo ameyasema wakati wa ziara yake ya kutembelea kituo hicho kilichopo Bungi Wilaya ya Kati Unguja.
Amesema lengo la ziara hiyo ni
kuangalia ufanisi wa kazi kwa watendaji wa kituo hicho na kusisitiza
kuwa ni jukumu la Wizara kufanya hivyo ili kuimarisha dhana ya
uwajibikaji kwa watendaji wake.
Amesema kwa sasa Serikali inaweza
kuendesha mitambo ya kurushia matangazo iliyopo kituoni hapo bila ya
kutegemea mafundi kutoka nje ya Nchi kama vile China kwani ina mafundi
wa kutosha wenye uweledi katika fani ya uhandisi wa mitambo ya Redio na
Televisheni.
Aidha ametanabahisha kuwa Serikali
ina jukumu la kuwaongezea ujuzi baadhi ya mafundi hao kwa kuwapeleka
kusoma nje ya Nchi ili waende sambamba na mabadiliko ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano ya Umma.
Waziri huyo amewataka mafundi wa
kituo hicho kurekebisha matatizo madogo madogo yaliyopo kituoni hapo
ikiwemo kufunga mafeni pamoja na viyoyozi (Air Condition) ili kuzifanya
mashine hizo zidumu kwa muda mrefu na kupunguza hasara ya kuungua mara
kwa mara kutokana na joto kali linakuwemo katika vyumba hivyo vya
kurushia matangazo.
Waziri Mbarouk amewataka
wafanyakazi kuwa wabunifu katika utendaji wao wa kazi na kutekeleza
majukumu yao ipasavyo kwa lengo la kuliimarisha shirika hilo kwani
matangazo yake ni muhimu ndani na nje ya Nchi ikiwemo mwambao wa Kenya
ambao wanategemea kwa kiasi kikubwa matangazo ya ZBC.
Nae fundi mkuu wa kituo hicho Nd.
Ali Aboud Talib amesema wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo
uchakavu wa nyaya za kurushia matangazo (Cable) kutokana na kutumika kwa
muda mrefu, kuwepo kwa msitu mkubwa kutokana na kukosekana kwa
wafanyakazi wa kusafisha eneo hilo.
Vilevile amesema tatizo la usafiri
ni usumbufu mkubwa kwao kwani hadi sasa kituo hicho kina gari moja
ambayo haitoshelezi kwa kazi za kila siku pamoja na Taa za Mnara wa
kurushia matangazo kuwa haziwaki.
Aidha amesema mashine za kurushia
matangazo (Transmitter) hazina uwezo mkubwa ukilinganisha na vyomo
vyengine vya habari vilivyopo Nchini kwani hadi sasa ZBC inatumia
mashine yenye uwezo wa masafa ya 1 kilowatts ambapo vyombo vyengine
vinatumia mashine zenye uwezo wa masafa hadi 4 kilowatts.
Fundi huyo amewataka wananchi kuwa
wazalendo kwa kuangalia Televisheni yao ya nyumbani (ZBC) ili kuipa
thamani ndani na nje ya Nchi jirani kwa kuwa na watazamaji wengi.
No comments:
Post a Comment