WAZIRI MKUU Mizengo
Pinda amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Bw. Ahmed Sawa akae
pamoja na Afisa Elimu wake na kuwapunguza walimu 230 waliozidi mahitaji
ya walimu kwenye manispaa hiyo na badala yake wawapangie kwenda
vijijini.
Ametoa agizo hilo jana
jioni (Jumapili, Februari 22, 2015) wakati akizungumza na mamia ya
wakazi wa kata ya Ipogolo waliofika kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Ipogolo, nje kidogo ya
Manispaa ya Iringa.
“Manispaa inahitaji
walimu 534 lakini waliopo ni 764. Hapa kuna ziada ya walimu 230 tena kw
shuke za msingi… Mkurugenzi kaa na Afisa elimu wako muwaondoe walimu
waliozidi na kuwapangia waende vijijini ambako kuna mahitaji zaidi,”
alisema.
“Kwa upande wa shule
binafsi nako pia tatizo ni lile lile. Walimu wamezidi. Mahitaji ni
walimu 75 waliopo ni walimu 142 … wanaozidi ni walimu 67,” alisema
Waziri Mkuu.
“Sina tatizo na walimu
wa shule binafsi kwa sababu wao wana mfumo wao wa ajira lakini hawa wa
shule za Serikali ni lazima muwaondoe tena haraka sana. Waondoeni waende
vijijini kwenye mahitaji makubwa sababu ualimu ni ualimu tu, siyo
lazima mtu awe mjini ndiyo afundishe vizuri,” alisema.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu aliupongeza uongozi wa mkoa wa Iringa kwa kuwa na ufaulu wa
juu kwenye shule za msingi lakini akawataka wajiulize ni kwa nini ufaulu
huo umeanza kushuka tangu mwaka 2013.
“Mwaka 2010 kiwango cha
ufaulu kilikuwa asilimia 77; mwaka 2011 kilikuwa asilimia 87; mwaka 2012
kilipanda na kufikia asilimia 97. Lakini mwaka 2013 kilishuka hadi
asilimia 82 na mwaka jana ni kama kipo palepale kwani kilikuwa asilimia
82.5. Kaeni mjiulize kumetokea nini na mtafanya nini ili kurudi tena
kwenye asilimia 97 au zaidi.”
Akizungumzia suala la
afya, aliwaeleza wananchi hao kwamba ameuagiza uongozi wa mkoa kupitia
watoa tiba wake waweke utaratibu wa kutoa elimu walau kila baada ya
miezi miwili au mitatu ili wananchi wapate ufahamu wa magonjwa makuu
yanayosumbua hivi sasa.
Akifafanua magonjwa ya
akinamama, Waziri Mkuu aliyataja magonjwa hayo kuwa ni saratani ya
matiti, saratani ya shingo ya uzazi na tatizo la fistula wakati kwa
upande wa akinababa alisema wao wanahitaji kupatiwa elimu zaidi kuhusu
ugonjwa wa tezi dume.
“Matatizo haya
yanatibika lakini ni lazima watu waeleweshwe kwamba wakiwahi kwenda
hospitali matatizo haya yanatibika lakini wakichelewa inakuwa tatizo
zaidi,” alisema.
No comments:
Post a Comment