Ametoa wito huo leo mchana
(Jumanne, Februari 24, 2015) wakati akizungumza na viongozi mbalimbali
na wananchi waliofika kushuhudia uzinduzi huo uliofanyika kwenye kata ya
Lumumba, Halmashauri ya Mji wa Makambako, mkoani Njombe.
“Ninawasihi viongozi wa siasa
tuwahimize wanachama wetu waende kujiandikisha kwa wingi. Tuache kauli
za kukatisha tamaa, tuache kauli za kejeli sababu zoezi hili ni jema na
lina nia ya kuwawezesha Watanzania wote kutumia haki yao ya kupiga
kura,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo
kuwaomba Watanzania wenye vitambulisho vya uchaguzi vya zamani na wale
wasio na vitambulisho wajitokeze kwa wingi kushiriki zoezi hilo.
“Wale waliokwishafikisha miaka 18,
na wale ambao watatimiza miaka 18 ifikapo Oktoba, mwaka huu wajitokeze
kwa wingi kujiandikisha kwa sababu wasipofanya hivyo hawataweza kupiga
kura kama hawatajiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,”
aliongeza.
Akiwa uwanjani hapo, Waziri Mkuu
alishuhudia uandikishaji wa wakazi watatu wa kata hiyo ambapo zoezi zima
lilidumu kati ya dakika tatu na dakika tano. Kisha alikabidhi kadi kwa
mpigakura wa kwanza kuandikishwa ambaye alitumia dakika tatu kamili.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amesema amefurahishwa na taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi, Jaji Damian Lubuva kwamba zoezi la uandikishaji
lililoanza jana katika mji wa Makambako lilizidi matarajio ya Tume ya
kuandikisha wapigakura 1,850.
“Nimefarijika sana na taarifa ya
Mwenyekiti… Mlianza na kata tisa zenye vituo 54 na mlitarajia
kuandikisha watu 1,850 lakini badala yake mmepata watu 3,014. Hili
limenipa faraja sana. Ninawapongeza sana kwa hatua hiyo,” alisema.
Mapema, akitoa taarifa kabla ya
kumkaribisha Waziri Mkuu kufanya uzinduzi huo, Jaji Lubuva alisema ana
imani wadau mbalimbali wataendelea kuhamasisha wananchi washiriki zoezi
la uboreshaji daftari la wapiga kura.
Alisema uboreshaji wa daftari hilo
utafanyika kikanda na kwamba wamepanga kutumia siku saba kwa kila kituo
huku akisisitiza kwamba hakuna mtu atakayebakizwa bila kuandikishwa
wakati ameshafika kituoni.
Aliwataka watu wanaokwenda
kujiandikisha wawe na vitambulisho vyao vya zamani vilivyotolewa na Tume
ya taifa ya Uchaguzi kwani tayari vina taarifa zao kwa hiyo vitapunguza
muda wa mtu kuandikishwa. “Kadi za Tume (NEC) au za NIDA kwa wale
wachache ambao wanazo, wakija nazo zitapunguza muda wa uandikishai
sababu zina taarifa kwenye kanzidata,” alisema.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mfumo wa
uandikishaji wa BVR, Jaji Lubuva alisema mfumo huo siyo sawa na mfumo wa
upigaji kura wa kielektroniki (e-voting) kama ambavyo wengi wanadai
bali mfumo huo unafanya kazi kwa kutumia alama muhimu za mpigakura.
“Mfumo huu unatumia alama zaidi
kwanza ikiwa ni picha na zaidi ni macho ya mhusika, pili ni alama za
vidole na tatu ni saini ya mhusika. Mfumo huu unaweza pia kuchukua alama
za mtu mwenye ulemavu wa kuona ama ulemavu wa mikono,” alisema.
Alisema uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapigakura ni hatua ya kisheria na kwamba Tume itajitahidi
kuhakikisha inafuata hatua zote wakati wa zoezi hilo.
Waziri Mkuu ameondoka Makambako na
anaelekea Mbeya kuanza ziara ya kikazi ya siku sita kukagua shughuli za
maendeleo katika mkoa huo.
No comments:
Post a Comment