Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Matokeo ya utekelezaji wa utoaji wa ruzuku kwa wachimbaji Madini
wadogo nchini Awamu ya Pili yanatarajiwa kufanyiwa tathmini na
ufuatiliaji kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Hayo yamebainishwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na
Madini, Mhandisi Ngosi Mwihava wakati akiongea katika Kipindi cha Jambo
Tanzania kinachorushwa kupitia Televisheni ya Taifa TBC1 mapema leo,
ambapo amefafanua kuhusu taratibu za maombi ya namna ya kupata ruzuku
kwa wachimbaji wadogo wa madini Awamu ya Pili.
Mhandisi Mwihava ameeleza kuwa, ili kupata matokeo bora ya namna
ruzuku hiyo itakavyotumiwa na wachimbaji wadogo watakaokidhi vigezo vya
maombi na kunufaika na ruzuku hiyo, mpango wa BRN utatumika ipasavyo
kuhakikisha kwamba fedha hizo zinatumika kama ilivyopangwa.
“BRN itatumika kufuatilia utekelezaji wa ruzuku. Wizarani tuna
Sehemu ya Ukaguzi wa Migodi, lakini pia tuna Shirika la Madini la Taifa
(STAMICO), hawa wote watashirikiana kufanya tathmini yenye matokeo
tunayotarajia,” amesisitiza Mhandisi Mwihava.
Ameongeza kuwa, kiwango cha ruzuku kwa wachimbaji wadogo Awamu ya Pili kimeongezwa kufikia Dola za Marekani 100,000/-, ruzuku ambayo inalenga katika kuendeleza uchimbaji mdogo ili uwe na tija; kuwakwamua wachimbaji wadogo kiuchumi na kuongeza pato la taifa. Aidha, ameeleza kuwa malengo mengine ya ruzuku hiyo kwa wachimbaji wadogo wa Madini kuwa ni kuendeleza mkakati wa kurasimisha shughuli za uchimbaji mdogo wa madini na kutoa mitaji ili kusaidia ukuaji wa tasnia ya uchimbaji mdogo wa madini. Malengo mengine ni pamoja na uongezaji thamani ya madini wenye Matokeo Makubwa Sasa. Ameongeza kuwa, Serikali imedhamiria kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini kuwawezesha kuwa wachimbaji wa kati, jambo ambalo limefanya Serikali kuzifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika utoaji ruzuku na mikopo awamu ya kwanza. “Tunataka kuwasaidia mitaji, kuwapatia vifaa na kuhakikisha wanapata uelewa wa namna ya kufanikisha shughuli zao kupitia wataalamu wetu. Tunalenga kuwafanya wakue hadi kuwa wachimbaji wakubwa”, ameongeza Mwihava. Aidha, Mhandisi Mwihava ametumia fursa hiyo kuwataka wachimbaji wadogo kuzitumia ofisi za madini zilizoko mikoani kwa ajili ya kuchukua fomu za maombi kuanzia tarehe 2 Machi na kuwataka kuzirejesha fomu hizo katika ofisi hizo ifikapo tarehe 27 Machi, 2015, zikiwa na viambatanisho vyake. Katika hatua nyingine, Mhandisi Mwihava amesema kuwa, migodi inayoshirikisha watoto wadogo katika shughuli za uchimbaji madini watanyanga’nywa leseni zao endapo itabainika kuwa, migodi hiyo inawashirikisha watoto, na hivyo kuwataka wachimbaji kufuata sheria na taratibu. “Watoto kushiriki katika shughuli za uchimbaji ni makosa. Watakaobainika watanyang’anywa leseni zao. Wizara inapinga si haki kwa watoto kufanya shughuli za uchimbaji madini”, alisisitiza Mwihava. Awamu ya pili ya utoaji ruzuku kwa wachimbaji wadogo nchini, inatekelezwa kupitia Wizara ya Nishati na Madini, chini ya Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini (SMMRP), unaopata fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia.
No comments:
Post a Comment