WAZIRI MKUU Mizengo
Pinda amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bibi Amina Masenza aandae orodha
ya watumishi wa mkoa huo ambao wamekaa kwenye nafasi za ajira kwa zaidi
ya miaka 10 na kumpelekea ili wafanyiwe utaraibu wa kuhamishiwa vituo
vingine.
Ametoa agizo hilo jana
jioni (Jumatatu, Februari 23, 2015) wakati akizungumza na viongozi
mbalimbali wa mkoa wa Iringa waliofika kusikiliza majumuisho ya ziara ya
siku sita ya Waziri Mkuu kwenye mkoa huo. Mkutano huo ulifanyika kwenye
ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ulioko Mafinga, wilayani
Mufindi.
“Tafuta wote waliokaa zaidi ya miaka 10. Ni lazima tuwabadilishe… niletee orodha mapema iwezekanavyo,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema nia ya zoezi
hilo ni kuongeza ufanisi kwani watumishi wakikaa sehemu moja kwa muda
mrefu wanakuwa butu kwa kukosa ubunifu kwenye kazi zao, wanaota mizizi
na kugeuka kuwa chanzo cha matatizo katika baadhi ya sehemu.
Alimtaka pia Mkuu huyo
wa mkoa pamoja na timu yake wasimamie vizuri ukusanyaji wa mapato ili
kuongeza kiwango cha mapato cha mkoa huo. “Na siyo hilo tu, simamieni
vizuri matumizi ya fedha zilizopangwa kwenye miradi mbalimbali ili
kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi mnaowaongoza,” alisisitiza.
Alisema mkoa wa Iringa
ni wa pili kwa kuwa na kiwango cha juu cha pato la mwanachi wa kawaida
baada ya Dar es Salaam ambao ndiyo unaongoza nchini. “Katika taarifa ya
Mkuu wa Mkoa, tulielezwa kwamba pato la mwananchi wa Iringa katika mwaka
2013 lilikuwa ni wastani wa shilingi 1,660,532/- ambazo ni sawa na
shilingi 138,377/- kwa mwezi au shilingi 4,612/- kwa siku”.
Alisema pato la
mwananchi wa Iringa linakua vizuri ikilinganishwa na mwaka 2006 ambapo
pato hilo lilikuwa shilingi 589,607/- na limeongezeka hadi kufikia
shilingi 1,660,532/- mwaka 2013. Alivitaja viashiria vya kukua kwa
uchumi kuwa ni pamoja na ujenzi wa nyumba za kisasa zenye umeme, elimu
bora, afya bora na upatikanaji wa vifaa vya mawasiliano kwenye ngazi ya
kaya.
Alisema kulingana na
taarifa ya Shirika la Fedha Duniani (IMF), Tanzania imeondolewa kutoka
miongoni mwa nchi 10 barani Afrika zenye umaskini mkubwa na kwamba sasa
Tanzania ni miongoni mwa nchi 20 duniani ambazo uchumi wake unakua kwa
kasi kubwa.
“Kukua kwa pato la mkoa
kumechangiwa hasa na kuwepo kwa mashamba makubwa ya tumbaku, chai,
viwanda vya chai, misitu na viwanda vya mbao. Tukitumia vizuri fursa
hizi, na tukijipanga vizuri tutaweza kuongeza pato la mkoa kuzidi hapa
tulipo,” alisema.
Aliwataka watendaji wote
katika ngazi zote, wawe na dhamira ya kuwaletea wananchi maendeleo na
hivyo kuwaondolea umaskini na kuongeza pato lao kwa kila mmoja.
“Ninawasihi sana viongozi wa mkoa tutangulize maslahi ya wananchi na
siyo maslahi yetu binafsi. Tukifanya hivyo, wananchi wataona kweli
tunawasaidia na tunastahili kuwaongoza,” aliongeza.
Waziri Mkuu amemaliza
ziara ya siku sita katika mkoa wa Iringa na leo anakwenda Makambako,
Njombe kuzindua uandikishaji wa Daftari la Mpiga Kura. Baadaye mchana,
ataelekea Mbeya kuanza ziara ya kikazi ya siku sita kukagua shughuli za
maendeleo katika mkoa huo.
No comments:
Post a Comment