Na Anna Nkinda – aliyekuwa Pemba
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete
amehani msiba wa muasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bibi Ashura
Abeid Faraji aliyefariki mwishoni mwa mwaka jana katika kijiji cha
Tibirizi wilaya ya Chakechake mkoa wa Kusini Pemba.
Akiwa nyumbani kwa marehemu Mama
Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliwapa pole
wafiwa na viongozi wa Chama na Serikali na kusema kwamba alitambua
mchango wa Bibi Ashura katika kukijenga chama na kuisaidia jamii
inayomzunguka.
Alisema ingawa marehemu Bibi
Ashura alikuwa na umri wa utu uzima lakini hakuchoka kufanya kazi za
kukitetea chama chake na kuisaidia jamii inayomzunguka, kwa yale
aliyoyafanya anastahili kuigwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya
Chakechake Hanuna Ibrahim Masoud alisema marehemu alikuwa mshauri wa
chama na jamii kwa hiyo wamempoteza mtu wa muhimu sana.
“Licha ya kufanya kazi za chama
marehemu pia alikuwa anafanya kazi za kijamii ikiwa ni pamoja na kuwa
msuluhishi wa matatizo mbalimbali na kutoa ushauri hivyo basi kutokana
na utendaji wake alikuwa anakubalika na vyama vyote vya siasa kikiwemo
Chama Cha Wananchi (CUF)”, alisema Hanuna.
Mwaka 1954 Bibi Ashura alianza
kufanya kazi na chama cha Afro Shirazi Party (ASP) na baadaye CCM hadi
mauti yanamkuta alikuwa mjumbe wa baraza la wazee wa CCM na mjumbe wa
halmashauri kuu ya mkoa wa Kusini Pemba.
Baadhi ya nyadhifa alizozishika
wakati wa uhai wake katika chama na Serikali ni Naibu Katibu Mkuu wa
kinamama wa ASP mwaka 1974, mjumbe wa baraza kuu la umoja wa wanawake wa
Tanzania mwaka 1966-2012 na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa kupitia
mkoa wa Kusini Pemba.
Mbunge wa mwanzo wa kuteuliwa wa
Zanzibar aliteuliwa na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1981 – 1995 na mjumbe wa
baraza la wawakilishi viti maalum vya wanawake kutoka mkoa wa Kusini
Pemba mwaka 2005-2010.
Bibi Ashura alizaliwa mwaka 1938
na hadi mauti yanamkuta Novemba 27,2014 nyumbani kwake Tibirizi aliacha
watoto watatu wawili wa kike na mmoja wa kiume, wajukuu 25 na vitukuu
27.
Mama Kikwete alikuwa kisiwani
Pemba kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za Maulid ya kuadhimisha kuzaliwa
kwa Mtume Muhammad (S.A.W) zilizofanyika katika viwanja vya shule ya
Sekondari Utaani Kaskazini Pemba.
No comments:
Post a Comment