Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akimshauri Ndugu Peter Charles,28, baba
mzazi wa binti Irene mwenye umri wa miezi 3 na mkazi wa Mikocheni
kupunguza baadhi ya nguo alizomfunika mtoto wakati hali ya hewa ni ya
joto. Mama Salma alimpongeza Ndugu Peter kwa kuambatana na mke wake
kwenda kliniki.
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na Bibi Mariam Omar aliyemshika
mtoto wake Jane Winston aliyekuwa akisubirim kupata huduma hospitalini
hapo wakati Mama Salma alipotembelea sehemu mbalimbali za Kitengo cha
Uzazi na Mtoto mara baada ya kukabidhi mashine ya kupimia saratani ya
matiti kwa akina mama tarehe 27.2.2015.
………………………………………………………..
Na Anna Nkinda – Maelezo
27/2/2015
Wanaume nchini wametakiwa kuwaunga mkono wake zao kupima saratani za
matiti na shingo ya kizazi na pale watakapokutwa na maradhi hayo
wasiwanyanyapae bali wawafariji kwani magonjwa hayo yanatibika kama
yatagundulika mapema.
Rai
hiyo imetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa hafla
fupi ya makabidhiano ya mashine ya kisasa ya upimaji wa saratani ya
matiti (Mammography) katika Hospitali kuu ya Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo, kliniki ya Mama na Mtoto iliyopo
Mwenge jijini Dar es Salaam.
Mama
Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)
alisema unyanyapaa wa wanaume huwakwaza wanawake na kuwafanya baadhi yao
kusita kujitokeza kupima na kupata tiba dhidi ya saratani.
“Nanyi
wanawake msisubiri mpaka msikie maumivu ndipo mkapime maana wakati huo
saratani itakuwa imeenea, jengeni tabia ya kupima saratani za matiti na
shingo ya kizazi mara kwa mara wataalamu wanasema unapima mara moja
kila baada ya miaka mitatu”.
Bahati
nzuri saratani ya shingo ya kizazi ina kinga kwa njia ya chanjo hivyo
basi wazazi tuchangamkie kuwapeleka watoto wetu wa kike kupata chanjo
hiyo, tutawapatia kinga ya kudumu ya maradhi haya hatari”, alisisitiza
Mama Kikwete.
Alisema
ugonjwa wa saratani ya matiti unaathiri wanawake wengi nchini na
wataalam wa afya wanasema saratani ya matiti ni ya pili kwa ukubwa
nchini ikifuatiwa na ya shingo ya kizazi.
Mama
Kikwete alisema, “Niliamua kukabidhi mashine hii katika Hospitali hii
baada ya kubaini kuwa wananchi wengi wanatibiwa hapa pia huduma ya mama
na mtoto hutolewa hapa.Hospitali kuu ya Jeshi ya Lugalo ni Hospitali ya
Rufaa ya Kanda ya Mashariki hivyo inastahili kuwa na mashine ya aina hii
ambayo itawanufaisha wanawake wengi wanaokuja hapa kuhudumiwa”.
Kwa
upande wa saratani ya tezi dume aliwahimiza wanaume wenye umri wa zaidi
ya miaka 45 wajitokeze kupima kwani ikigundulika mapema inatibika.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA alisema, “Wanawake nasi tunao wajibu wa kuwahamasisha
waume zetu kupima saratani ya tezi dume na kuwafariji wakiwa wakiwa
kwenye tiba. Tushirikiane kwa pamoja kuleta mabadiliko”.
Naye
Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Samuel Ndomba alimpongeza Mama
Kikwete kwa kazi anayoifanya ya kuiongoza Taasisi ya WAMA yenye lengo la
kuinua ustawi wa watoto na akina mama hususani katika nyanja za afya,
elimu na huduma za maji safi na salama.
Alisema,
“Juhudi kubwa unazozionyesha za kuboresha na kuendeleza huduma za afya
ya mama na mtoto zinadhihirisha upendo wa dhati ulionao kwa umma wa
watanzania”.
Luteni
Jenerali Ndomba alisema tukio hilo la kukabidhiwa mashine ya kupimia
saratani ya matiti kwa Jeshi hilo ni la kihistoria na la kipekee na
kumshukuru Mama Kikwete kwa kutambua umuhimu, kujali na kuthamini afya
za wanajeshi, familia zao na akina mama wote.
“Ni
dhahiri kuwa ulinzi imara wa taifa letu unategemea wanajeshi na wananchi
wenye afya nzuri. Tunakuhakikishia kuwa mashine hii haitatumika kwa
wanajeshi na familia zao tu bali itatumika kutoa huduma kwa wananchi wa
Tanzania kwa kufuata kanuni na taratibu za huduma ya tiba Jeshini”,
alisema Luteni Jenerali Ndomba .
Alimalizia
kwa kusema Jeshi hilo litaweka kipaumbele katika mafunzo kwa wataalam
ambao wataweza kuitumia na kuitunza vizuri mashine hiyo ili utoaji wa
huduma kwa akina mama uwe endelevu.
Mashine
hiyo imetolewa na kikundi cha wanawake wajasiriamali wa Tanzania
waishio nchini Washington, nchini Marekani cha Wanawake watano (Tano
Ladies) kwa kushirikiana na Chama cha Wanawake wa Afrika na Uelewa wa
Saratani (African Women Cancer Awareness Assossiation – AWCAA).
Wanawake
hao walimkabidhi Mama Kikwete mashine hiyo ya kupimia saratani ya
matiti mwishoni mwa mwaka jana alipokuwa nchini Marekani katika shughuli
za kikazi ili iweze kusaidia na kuokoa maisha ya wanawake hapa
nchini.
No comments:
Post a Comment