WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda ameupongeza uongozi wa mkoa wa Mbeya kwa kuvuka
lengo la wastani wa pato la mwananchi kitaifa na kuwataka waendeleze
kasi ya kupambana na umaskini kwa wakazi wa mkoa huo.
Ametoa pongezi hizo jana usiku
(Jumanne, Februari 24, 2015) wakati akizungumza na viongozi wa mkoa huo
na wilaya zote wakiwemo wadau mbalimbali na viongozi wa dini mara baada
ya kupokea taarifa ya Mkoa wa Mbeya.
Alisema katika mipango yake,
Serikali ililenga kwamba pato la mtu kwa mwaka liwe sh. 1,186, 200,
lakini kwa sababu ya jitihada mbalimbali mkoa huo umelivuka. “Katika
taarifa aliyonisomea, Kaimu Mkuu wa Mkoa amesema wastani wa pato la
mwananchi umeongezeka kutoka sh. 711,201/- mwaka 2008 hadi kufikia sh
1,420,427/- mwaka 2013 na kwamba mkoa unachangia asilimia 7.43 ya Pato
la Taifa,” alisema.
Alisema kipato cha mtu mmoja kwa
siku ni sh. 3,891/- ambazo ni zaidi ya Dola mbili za Marekani (sh.
3,400/-). “Wakubwa hawa wanatupima kwa kuangalia kipato cha mtu kwa
siku. Wanasema nchi ni maskini iwapo watu wake wanaishi chini ya dola
moja kwa siku (sawa na sh. 1,700/-).”
“Mbeya imeendelea kushika nafasi
ya tatu kwa kuchangia vizuri Pato la Taifa ikiwa imetanguliwa na Dar es
Salaam na Iringa. Ninawapongeza kwa sababu mmevuka malengo ya Taifa
katika eneo la pato la mtu mmoja mmoja,” alisema Waziri Mkuu.
Mapema, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya, Bw. Deodatus Kinawilo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Chunya,
alisema pato la mkoa limeongezeka kutoka sh. trilioni 1.779 mwaka 2008
na kufikia sh. trilioni 3.951 mwaka 2013.
“Uchumi wa mkoa huu unategemea
kilimo, ufugaji, uchimbaji madini, uvunaji mazao ya maliasili, biashara,
uzalishaji viwandani na ajira katika taasisi za serikali na sekta
binafsi,” alisema.
Wakati huohuo, uongozi wa mkoa wa
Mbeya umetakiwa kuongeza bidii ili uweze kuinua kiwango cha ufaulu wa
elimu ya kwa sababu umekuwa ukiendelea kushuka na kuwa chini ya kiwango
cha asilimia 60 kilichowekwa na Serikali.
Waziri Mkuu aliutaka uongozi huo
ubuni mbinu za kisomi zitakazowawezesha wanafunzi wa shule za msingi
kuelewa wanachofundishwa, hivyo, kufaulu mitihani yao vizuri. ”Ufaulu
wenu kwa shule za msingi ni asilimia 46.6, uko chini ya kiwango cha
kitaifa cha ufaulu kwa asilimia 13.4. Ni matokeo yasiyoridhisha, fanyeni
utaratibu maalum ili yapande,” alisema.
No comments:
Post a Comment