MAANDALIZI
kwa ajili ya Tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania, zinazotolewa na Chama
cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) yamekamilika.
Tuzo hizo zitatolewa kesho Ijumaa
kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee Dar es Salaam, kuanzia saa 12 jioni,
ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein.
Wanamichezo mbalimbali
wanatarajiwa kupewa tuzo hizo kutokana na kufanya vizuri katika michezo
yao kwa kipindi cha Juni 2013 hadi Juni 2014, ambapo bendi ya Kalunde ya
Dar es Salaam itatumbuiza.
Washindi wa kila mchezo watawania
nafasi ya Mwanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2013/2014 na mshindi
atatangazwa ukumbini na Dk. Shein, ambaye pia atamkabidhi tuzo yake.
Baahi ya waliopata kutwaa tuzo ya
Mwanamichezo Bora Tanzania ni Samson Ramadhani (2006), Martin Sulle
(2007) na Mary Naali (2008) wote wanariadha.
Mwaka 209 tuzo ilienda kwa mcheza
netiboli Mwanaid Hassan, ambaye pia alitwaa tuzo hiyo mwaka 2010, wakati
mwaka 2011, ambapo tuzo yake ilitolewa mwaka 2012 mshindi alikuwa
mwanasoka Shomari Kapombe.
Tuzo ya mwaka 2012 iliyokuwa
itolewe mwaka 2013 haikufanyika kutokana na wadhamini kujitoa dakika za
mwisho. Kwa kawaida tuzo ya mwaka husika hutolewa kati ya Juni hadi
Agosti mwaka unaofuata.
Wanamichezo wengine watakaoshinda
kwenye michezo yao kesho watakabidhiwa tuzo zao na wageni mbalimbali
walioalikwa wakiwemo wanamichezo wa zamani, viongozi wa serikali na wa
kisiasa.
Tuzo za mwaka huu zimedhaminiwa na
Selcom Wireless, Said Salim Bakhresa & Co Ltd – Bakhresa Group,
IPTL, A to Z, mifuko ya hifadhi ya jamii, PSPF na NSSF.
Pia kutatolewa tuzo ya Heshima, ambayo itatangazwa na mgeni rasmi na ndiye atakayekabidhi zawadi kwa mshindi huyo.
Tuzo ya Heshima inatolewa kwa mdau
yeyote ambaye TASWA inaona anastahili kutokana na mchango wake katika
masuala mbalimbali ya michezo.
TASWA imewahi kutoa Tuzo ya
Heshima kwa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, pia imewahi
kutoa Tuzo ya Heshima kwa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa
Stars’ iliyokuwa ikicheza mechi za kufuzu fainali za mataifa ya Afrika
mwaka 1980 zilizofanyika Lagos, Nigeria.
No comments:
Post a Comment