Na Oyuke Phostine – Shinyanga
Serikali imetoa wito kwa Ofisi za
wakuu wa mikoa kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda kwenye
mikoa yao ili kuweza kukuza uchumi wa mikoa husika na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Bw. Paul
Sangawe, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, anayeshughulikia
Biashara za Kimataifa wakati akiongoza timu ya wataalam kutoka ofisi
hiyo iliyokuwa ikifanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa
na Serikali na sekta binafsi katika mikoa ya Shinyanga, Mara, Simiyu, na
Mwanza.
Bw. Sangawe, alisema kuwa Wajibu
wa Serikali ni kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuwekeza.
Alifafanua kuwa, moja ya vipaumbele katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka
Mitano ambao utekelezaji wake unaishia 2015/16, ni miundombinu ili
kufungulia fursa za ukuaji wa uchumi.
Aidha, Mpango wa Maendeleo wa
Miaka Mitano unaofuata kuanzia 2016/17 utalenga katika kuendeleza
viwanda. Hivyo, alitoa rai kwa viongozi katika ngazi za mikoa kuratibu
masuala ya uwekezaji hususan katika viwanda ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha kuwa uwekezaji huo unawanufaisha wananchi wa maeneo husika
kwa kuongeza fursa za ajira na masoko ya bidhaa za kilimo.
“Uwepo wa viwanda hivi unaonyesha
mwenendo na mwelekeo mzuri wa taifa katika kufungua fursa za maendeleo
na kiuchumi kupitia sekta ya viwanda, hivyo basi iwapo jitihada za
kuhamasisha uwekezaji wa viwanda katika kila mkoa zitatiliwa maanani ni
dhahiri kuwa fursa za ajira zitaongezeka na kasi ya ukuaji uchumi
itaongezeka” alisema Bw. Sangawe.
Akizungumza na timu hiyo ya
ukaguzi wa miradi ya maendeleo ilipotembelea na kukagua kiwanda cha
kusindika mafuta kwa kutumia alizeti na mbegu za pamba cha Jielong
Holdings Mkoani Shinyanga, Kaimu Meneja Utawala Bw. Atanas William
alisema kuwa mpaka sasa kiwanda hicho kinaweza kusindika na kuhifadhi
lita milioni 2.4 kwa mwezi.
“Kwa sasa upatikanaji wa mali
ghafi ni wakuridhisha kwa sababu bado tunanunua alizeti kutoka kwa
wakulima, na mbegu za pamba katika vinu vya kuchambua pamba (Ginneries).
Tuna mpango wa kuhamasisha na kuwafundisha wakulima njia bora za kilimo
na utunzaji wa mazao ili kujihakikishia upatikanaji wa mali ghafi yenye
ubora zaidi” alisema Bw. Atanas.
Viwanda vingine vilivyotembelewa
ni kiwanda cha Dahong kinachotengeneza nyuzi za pamba na kiwanda cha
Xinghua cha kusindika ngozi mkoani Shinyanga na kiwanda cha nguo cha
Mwatex Mkoani Mwanza. Kiwanda cha Dahong kina uwezo wa kununua tani
12,000 za pamba kwa mwaka na kuzalisha tani 7 za nyuzi za pamba kwa
siku. Kiwanda hiki kimeanza uzalishaji mwezi Septemba 2014, na nyuzi
zote zinazozalishwa zitauzwa nchini China.
Kwa mujibu wa bwana Luke Li,
ambaye ni afisa fedha wa kiwanda hicho, mipango ya baadae ya kiwanda
hicho ni kutengeneza nguo. Bwana Li pia alisema kuwa kuna mpango wa
kujenga kinu cha kuchambua pamba na kutoa mafunzo kwa wakulima ili
kuwezesha upatikanaji wa pamba yenye ubora unaotakiwa.
Kwa upande wake, Meneja wa kiwanda
cha Xinghua, Bw. Wang, alisema kuwa usindikaji wa ngozi unasuasua
kutokana na upatikanaji hafifu wa malighafi. Wafugaji wanapowekea alama
mifugo na kutoboa ngozi wakati wa kuchinja, wanaathiri sana ubora wa
ngozi alisema meneja huyo. Katika kukabiliana na changamoto hii,
mwekezaji huyo ana mpango wa kujenga machinjio ya kisasa ambayo pia
itahusisha usindikaji wa nyama.
Aidha Bw. Sangawe alitoa rai kwa
viongozi wa mikoa inayotoa ngozi kwa wingi kuongeza jitihada za kutoa
elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa ubora wa ngozi ili kuhakikisha
ngozi inayopatikana Tanzania inakuwa na thamani ya hali ya juu.
No comments:
Post a Comment