KAMPUNI ya Simu nchini Tanzania
(TTCL) sasa imerahisisha upatikanaji wa vocha zake baada ya kuingia
makubaliano kuishirikiano na benki 13 nchini zinazotoa huduma zake pia
kwa kupitia simu za mkononi (Mobile Banking) ambapo sasa mteja wa TTCL
ataweza kuongeza salio kupitia simu yake ya mkononi (TTCL top-up).
Akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam, Meneja Mipango na Mauzo wa TTCL, Benjamin
Bizere alisema huduma hiyo ya kununua salio kwa njia ya simu kupitia
mabenki 13 imeanza kufanya kazi hivi sasa hivyo mteja wa TTCL anaweza
kununua salio lake popote alipo kwa kutumia simu yake.
Alisema TTCL imeingia makubaliano
ya kiushirikiano katika uuzaji wa muda wa maongezi kwa benki za Standard
Chartered, Akiba Commercial (ACB), Tanzania Postal Bank (TPB), Exim
Bank, Dar Es Salaam Community Bank (DCB), Mkombozi Bank, KCB Bank pamoja
na Bank of Africa ambazo wateja wa beki hizo wanaweza kununua salio
kupitia simu zao popote walipo kwenye akaunti zao.
“…Jumla ya benki 13 zimeingia ubia
wa kibiashara na TTCL kwa ajili ya kuuza vocha za TTCL kupitia benki
zao…hapo juu nimetaja majina ya benki zote ambazo zinatumika kwa ajili
ya kufanya miamala mbalimbali ikiwemo TTCL TOP-UP,” alisema Bw. Bizere.
Akifafanua zaidi juu ya huduma
hiyo Mkuu wa Mauzo wa TTCL, William Chamla alisema huduma ya TTCL TOP-UP
na Mobile banking ni njia ambayo TTCL imeanzisha kwa wateja wake kwa
ajili ya kuongeza salio la muda wa maongezi kwa simu za mezani, mkononi
na kununua vifurushi vya intaneti hivyo mteja ataweza kununua salio lake
muda wowote na popote.
“…Mteja atakayenufaika na huduma
hii ni yule mwenye akaunti ya benki, na amejisajili katika huduma ya
kibenki kupitia simu ya mkononi yaani ‘mobile banking’. Hata hivyo
alisema ili kuwarahisishia upatikanaji wa huduma kwa wateja wa wao vocha
za TTCL pia zinapatikana katika vituo vya Maxmalipo na Selcom ‘wireless
Point’ na kwenye Ofisi za TTCL, pamoja na vituo vya huduma kwa wateja
ambako viko katika kila mkoa na wilaya.
No comments:
Post a Comment