Na Mwandishi Wetu
WAKATI zikiwa zimebaki siku
chache kuelekea Tamasha la Krismasi linalotarajia kuanza Desemba 25
kwenye mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, wadau na waumini wa dini
mbalimbali hapa nchini wanatarajia kupokea neno la Mungu kupitia
waimbaji wenye mvuto wa aina yake katika muziki huo ambao unafanikisha
ukaribu baina ya Binaadamu na Mungu.
Ukaribu huo baina ya binaadam na
Mungu pia unafanikishwa kupitia Wachungaji na Maaskofu mbalimbali
watakaojitokeza katika tamasha hilo ambalo litafanyika kwenye mikoa ya
Mbeya, Iringa na Ruvuma katika Wilaya ya Songea.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa
Msama Promotions ambayo inaandaa tamasha hilo, Alex Msama maandalizi ya
tamasha hilo yamefanyika kwa asilimia kubwa kama viwanja na maeneo
mengine muhimu yamekamilika.
“Maandalizi ya Tamasha la
Krismasi mwaka huu yamefanyika kwa kiasi kikubwa, hivyo wadau wa muziki
huo wajiandae kupokea injili kutoka kwa waimbaji na maaskofu mbalimbali
watakaohudhuria,” alisema Msama.
Tamasha la Krismasi lina lengo
la kudumisha amani kwa Tanzania kwani mwaka huu Kauli mbiu ya tamasha
hilo ni “Tanzania ni ya Kwetu, Tuilinde na Tuipenda,” alisema Msama.
Kupitia Tamasha la Krismasi na
Pasaka, vituo mbalimbali vya kulelea watoto wenye uhitaji maalum
wanapata mahitaji muhimu kupitia viingilio vinavyopatikana.
Kampuni ya Msama Promotions
haikuishia hapo imeenda mbali zaidi kwa kuelekeza nguvu zake zaidi kwa
kujipanga kwa lengo la kujenga kituo cha Kimataifa katika eneo la Pugu
nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam kitakachojulikana kama Jakaya
Kikwete Rafiki wa Wasiojiweza.
Anasema Tamasha la Krismasi ni
zao la Tamasha la Pasaka ambalo limeshika hatamu ya muziki wa Injili
Afrika Mashariki na Kati, ambako waimbaji mbalimbali kutoka katika nchi
hizo wanashiriki kutoa huduma.
Aidha Msama anawataja waimbaji
watakaopanda jukwaani kwenye tamasha hilo ni pamoja na Rose Muhando,
Upendo Nkone, Bonny Mwaitege, Emmanuel Mgogo, Fraja Ntaboba, Solomon
Mukubwa, Edson Mwasabwite, Upendo Kilahiro, Joshua Mlelwa, Tumaini Njole
na Martha Mwaipaja.
No comments:
Post a Comment