Kwa miaka mingi sasa tangu taifa
letu liingie katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 kumekuwa na
mabadiliko yaliyoletwa na taratibu na kanuni za uendeshaji wa mfumo huu
wa vyama vingi vya kisiasa. Mfumo wa Vyama vingi katika nchi umekuwa
ukitoa fursa ya kidemokrasia kwa kila mwananchi aliefikisha umri wa
miaka 18 kushiriki katika uchaguzi wa viongozi wa serikali kwa mujibu wa
sheria.
Kutokana na mabadiliko haya katika nchi yetu, kwa sasa tumekuwa
na vyama vingi vya siasa kama vile CCM, Chadema, CUF, NCCR Mageuzi, TLP
na vingine vingi. Vyama hivi vimekuwa vikitoa wagombea katika nafasi
mbalimbali kama vile Wenyeviti wa serikali za mitaa, madiwani, wabunge
na urais. Sanjali na hilo, vyama hivi vimekuwa na kipindi cha kufanya
kampeni kwa lengo la kutoa ushawishi kwa Wananchi ili wawachague
viongozi wa vyama vyao.
Kwa mwaka huu 2014 taifa lipo katika mchakato wa kufanya
uchaguzi wa viongozi wa serikali katika ngazi ya Vitongoji, Vijiji na
Mitaa Tarehe 14.12.2014. Katika kuhakikisha zoezi hili linafanyika kwa
mafanikio ikiwa na maana linafanyika kwa amani na utulivu, idara na
taasisi mbalimbali ushirikiana kwa pamoja katika kusimamia na kuratibu
shughuli mbalimbali za uchaguzi kuanzia uandikishwaji wapiga kura,
kampeni, upigaji kura na hatimaye zoezi zima la utangazaji wa matokeo
yenyewe.
Suala la msingi la kujiuliza, je ni nani mwenye wajibu wa
kuhakikisha shughuli za uchaguzi zinafanyika kwa amani na utulivu bila
kuwepo kwa vitendo vitakavyo pelekea uvunjifu wa amani? Ni wajibu wetu
sote kwa nafasi tuliyonayo kutambua sheria, kanuni na taratibu za
mchakato wa uchaguzi kwani vitendo vyovyote vya uvunjwaji wa sheria
kabla na baada ya uchaguzi, ni uhalifu. Sheria haina udhuru, inachukua
mkondo wake mara moja endapo tu ukiukwaji umefanyika.
Katika mchakato huu kuelekea uchaguzi mara kwa mara tumekuwa
tukishuhudia vitendo vya uvunjifu wa amani na utulivu hasa katika
Kampeni na siku ya uchaguzi. Imekuwa ni kawaida kwa baadhi ya watu
kujiona wenye nguvu na kusababisha kuchochea vitendo visivyo vya
kiungwana. Katika kipindi kama hiki tumeona idara, tume na taasisi
zikifanya jitihada za kutoa elimu kwa wananchi kwa njia mbalimbali ikiwa
ni pamoja na kutoa vipeperushi, maandiko, vipindi maalum vya redio
pamoja na mikutano.
Kwa kuelewa vizuri taratibu, kanuni na sheria za uchaguzi ni
hakika kila mmoja atashiriki zoezi la upigaji kura bila kuwepo vitendo
vya uvunjifu wa amani. Miongoni mwa idara zilizopewa jukumu la kulinda
amani na usalama wa raia ni Jeshi la Polisi. Polisi kama chombo cha
umma, hakitumikii chama chochote cha siasa bali ni chombo
kinachowajibika kutenda kwa haki na usawa bila upendeleo katika mchakato
mzima wa uchaguzi.
Polisi pamoja na wajibu wa kulinda amani na usalama wa raia
wote, katika kipindi cha uchaguzi utekelezaji wa majukumu unaweka mkazo
katika yafuatayo, kuhakikisha mikutano ya kampeni inafanyika na
kumalizika salama, kuhakikisha kwamba zoezi la upigaji kura linaenda
sawa, bila vikwazo au bughudha, kuhakikisha kwamba vifaa vya kupigia
kura viko salama yaani haviibiwi, havitekwi wala kughushiwa na watu
wenye nia mbaya, kuhakikisha mchakato wa kupiga kura, kuhesabu na
kutangazwa matokeo unakuwa huru na haki pamoja na kuhakikisha amani,
usalama na utulivu vinadumu kabla na baada ya matokeo kutangazwa.
Ieleweke kuwa, kupiga kura ni haki ya msingi ya kila Mtanzania
aliyetimiza umri unaokubalika Kisheria. Haki ya kupiga kura inaambatana
na wajibu mbalimbali ikiwemo umuhimu wa kujielimisha mambo ya sheria na
taratibu zinazohusu mchakato mzima wa uchaguzi kwani kisingizio cha
kutokujua sheria iliyovunjwa siyo sababu ya kutokamatwa na kushitakiwa.
Hivyo kutii sheria na taratibu za uchaguzi ni wajibu.
Ni wajibu wetu sote kuendelea kuelimishana kwa kupeana elimu ya
uchaguzi ili kuepuka makosa hama uhalifu kabla na baada ya uchaguzi.
Wagombea, Viongozi wa Serikali, Viongozi wa Dini na waandishi wa habari
kwa pamoja na kwa nafasi zao wanayo nafasi ya kuwaelimisha wananchi
kanuni, taratibu na sheria za uchaguzi ili kujiepusha na vitendo vya
uvunjifu wa amani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa
Polisi Ahmed Z. Msangi anasema “Ulinzi na Usalama wetu siku zote unaanza
na mimi, wewe na sisi sote” kwa ushirikiano, nguvu na nia ya pamoja ni
hakika uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa utafanyika kwa amani na
utulivu, kila mmoja atimize wajibu wake kwa kufuata sheria,kananu na
taratibu za uchaguzi.
Imetolewa na:
[Ahmed Z.Msangi – SACP]
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya.
No comments:
Post a Comment