CHAMA Cha Mapinduzi (CCM)
kimejigamba kuwa kinaingia kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa kesho,
kikiwa kimeshajizolea maelfu ya nafasi ambazo wagombea wake wamepita
bila kupingwa.
Akizungumza juzi wakati wa mkutano wa kufunga kampeni za
uchaguzi huo, jijini Dar es Salaam Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Nape
Nnauye alisema, kulingana na takwimu CCM imepita bila kupingwa katika
vijiji 2708, mitaa 644, na vitongoji zaidi ya 26,300.
Alisema, CCM imeweza kupita bila kupigwa baada ya vyama vya
upinzani kushindwa kusimamisha kabisa wagombea na maeneo mengine kuweka
wagombea ambao walionekana kukosa sifa za kugombea baada ya kuwekewa
pingamizi.
Nape alisema, hatua hiyo ya CCM kuingia kwenye uchaguzi huo
ikiwa na mtaji mkubwa wa nafasi ambazo wagombea wake amepita bila
kupingwa ni dalili tosha kwamba chama kitavibwaga vibaya vyama vya
upinzani kuliko uchaguzi uliopita mwaka 2009.
“Uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa CCM iliibuka na ushindi
wa asilimia 96, sasa kutokana na dalili za mapema, uchaguzi wa safari
hii sina shaka kabisa kwamba wapinzani tutawapiga kwa ushindi wa
asilimia mia moja”, alisema Nape.
Nape aliupongeza uongozi wa CCM katika jimbo la Ilala, baada ya
kumthibitibishia kwamba katika kipindi chote cha kampeni jimbo hilo
wamekuwa wakifanya kampeni za kistaarabu na wanao uhakika wa
kuibuka na ushindi kwa asilimia mia moja baada ya uchaguzi.
“Sina shaka kabisa kwamba hapa Ilala tutashinda kwa kishindo,
mnastahili kupata pongezi kutoka makao makuu kutokana na mlivyoendesha
kampeni, hongereni sana.”. alisema Nape.
Alisema, pamoja na CCM kuwa na uhakika wa kushinda lakini
itafanya kazi ya ziada ya kuhakikisha wapigakura waliojiandikisha
wanapata fursa ya kwenda kupiga kura bila kubughudhiwa na watu ambao
huandaliwa na vyama vya upinzani kufanya fujo ili kuzuia watu
wasijitokeze kupiga kura.
“Nasema bila kificho, vijana wa CCM kama mtamuona mtu yeyote
anajaribu kufanya fujo wakati wa upigaji kura mshughulikieni kidogo
kabla ya kumpeleka polisi, maana watu wa aina hii wanabaka demokrasia,
lazima waadabishwe”. alisema Nape na kuongeza.
“Vijana wa CCM lazima tuwe shupavu, maana kujifanya wanyonge
unyonge huu hautatusaidia chochote, na hili mimi sihamasishi fujo na si
wa kwanza kulisema hata Mwenyekiti wetu wa CCM alishasema kwamba unyonge
basi. Sasa mimi hapa napigilia msumari tu”.
Nape aliwataka wananchi wa Ilala na Watanzania kwa jumla
kuchagua wagombea wa CCM, kwa kuwa ana uhakika ndio watakao watumikia
vizuri.
Aliwataka viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huo wa
serikali za mitaa kuhakikisha wanawatumikia wananchi, hasa kwa kusimamia
kuondoa kero zao na kusimamia misingi ya kuboresha mazingira ya
shughuli mbalimbali zikiwemo za biashara kama za mamalishe na machinga.
Nape alisema, CCM, itaendelea kusimamia na kutetea haki za
wananchi hasa walio wanyonge na si kwa sababu ya kutaka kura ila kwa
sababu ni wajibu wake kama chama kilichopewa ridhaa ya kutawala nchi.
Katika mkutano huo, Nape aliwanadi wagombea wa nafasi mbalimbali
katika Mtaa huo wa Mtambani B, akiwemo mgombea wa nafsi ya Ueneyekiti
wa mtaa huo, Gungu Tambaza.
No comments:
Post a Comment