…………………………………………………………………………..
Na Asteria Muhozya, Nzega
Mgodi wa Resolute uliopo Wilayani Nzega Mkoani Tabora jana
tarehe 12 Desemba, 2014, ulikabidhi eneo la Mgodi kwa Chuo cha Madini
Dodoma katika hafla fupi iliyofanyika na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, anayeshughulikia madini Stephen Masele aliyekuwa
mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Nzega aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa huo,
Mhe. Bituni Msangi, Viongozi Waandamizi wa Wilaya ya Nzega, Kaimu
Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje, Kamati ya Kitaifa ya
uchimbaji, Uongozi wa Juu wa kampuni ya Resolute na wananchi.
Akihutubia katika hafla hiyo, Naibu Waziri Masele alieleza kuwa,
tukio la kukabidhiwa eneo hilo la Mgodi kwa Chuo ni tukio ambalo
limefungua ukurasa mwingine kutokana na kwamba Chuo cha Madini Dodoma
kitaiwezesha Tanzania kuzalisha wataalamu zaidi waliobobea katika tasnia
hiyo ambao mchango wao kwa taifa unahitajika katika kuendeleza sekta ya
madini.
“Tunataka wanafunzi wasome kwa vitendo, hii itawezesha kupata
wataalamu waliobobea. Ni nafasi kwa wanafunzi na Chuo cha Madini
kuitumia fursa hii vizuri. Najua kuna mawazo mchanganyiko ya kupoteza
mapato kwa Halmashauri na mengine ya kupata Chuo lakini, kufunga mgodi
ni sehemu ya Sheria ya madini”, aliongeza Masele.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nzega Bintuni Msangi,
akizungumza katika halfa hiyo, alieleza kuwa, Mgodi wa Resolute una
historia ya kuwa mgodi wa kwanza nchini kuzalisha madini ya dhahabu na
kuogeza kuwa, ndani ya kipindi cha miaka 12 cha uhai wa mgodi huo
umeweza kuchangia kiasi cha shilingi bilioni 290 za Kitanzania ikiwa ni
kodi mbalimbali zilizotolewa na mgodi huo kama mrahaba.
Aliongeza kuwa, Halmashauri iliweza kupata kiasi cha shilingi
bilioni 6 ikiwa ni kodi na kiasi cha Tsh bilioni 6 kilitumiwa na mgodi
huo kuwezesha za kijamii ikiwemo ujenzi wa zahanati, shule, upatikanaji
wa huduma safi ya maji katika eneo linalozunguka mgodi huo.
Pamoja na eneo la mgodi huo kukabidhiwa kwa Chuo cha Madini
Dodoma, vilevile mgodi umekabidhi majengo, mitambo, maabara ambapo, kwa
mujibu wa Mkuu wa Chuo cha Madinini Dodoma, Mjiolojia Mwandamizi Subian
Chiragwile alieleza kuwa, eneo hilo litatumiwa na wanafunzi wa mwaka wa
pili kwa ajili ya masomo ya vitendo.
Mgodi wa Resolute umefunga rasmi shughuli zake za uchimbaji
madini ya dhahabu katika eneo hilo, ambapo ulianza kazi zake mwaka 1998.
Kabla ya makabidhiano hayo, mgodi huo umefanya ukarabati, ujenzi wa
madarasa, na uhifadhi wa mazingira.
No comments:
Post a Comment