Na. Aron Msigwa –
MAELEZO.
Ofisi ya Taifa ya
Takwimu imesema kuwa Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Novemba, 2014 umepungua
hadi kufikia asilimia 5.8 kutoka 5.9 iliyokuwepo mwezi Oktoba ,2014 kutokana na
kupungua kwa kasi ya bei ya bidhaa na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa taarifa ya
mfumuko wa bei kwa waandishi wa habari
leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa kupungu kwa mfumuko wa Bei nchini
kumesababishwa na kupungua kwa bei za bidhaa za vyakula na zile zisizo za vyakula.
Amezitaja bidhaa za
vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei nchini kuwa ni pamoja na Unga
wa mahindi , unga wa ngano, tambi na vyakula vya lishe kwa watoto.
Bidhaa nyingine ni mavazi ya
wanaume zikiwemo suti, suruali, sare za shule na viatu vya wanaume huku bidhaa
za gesi, mafuta ya taa, mkaa, mazulia, vyandarua pamoja na simu na saa za mkononi
zikichangia kwa asilimia 17.2.
Kuhusu Fahirisi za bei
kwa maana ya kiwango cha badiliko la kasi ya bei za makundi ya bidhaa na huduma zote
zinazotumiwa na Kaya binafsi kwa kuzingatia kipimo cha mwezi amesema
kuwa zimeongezeka hadi kufikia 150.54 mwezi Novemba kutoka 149.70 za mwezi Oktoba,
2014.
Amefafanua kuwa
kuongezeka kwa Fahirisi hizo kumechangiwa na ongezeko la bei ya bidhaa za
vyakula hususan mchele, vitafunwa vinavyotokana na unga wa ngano,samaki,
matunda,mbogamboka,viazi mviringo, mihogo na viazi vitamu.
Akizungumzia uwezo wa
shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za mlaji kwa mwezi
Novemba , 2014 amesema kuwa umefikia shilingi 66 na senti 43.
“Uwezo wa shilingi 100
ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma kwa mlaji umepungua ,hii inamaanisha mtu anahitaji kuongeza ziada ya shilingi 33 ili aweze kununua bidhaa na
huduma zilezile anazozihitaji”
Kwa upande wa mfumuko
wa Bei wa mwezi Novemba 2014 katika nchi za Afrika Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana , Kenya
ukipungua kwa asilimia 6.04 kutoka
asilimia 6.43 za mwezi Oktoba, Uganda
mfumuko wa bei ukiongezeka hadi asilimia 2.1 kutoka asilimia 1.8 za
mwezi Oktoba.
No comments:
Post a Comment