………………………………………………………………..
Na: Genofeva Matemu – Maelezo
Tarehe: 09/01/2015
Vijana wa Mkoa wa Kilimanjaro wamewataka vijana wenzao kutokuwa
na mtazamo hafifu unaowafanya kujenga fikra mbaya kati yao hivyo
kushindwa kushirikiana katika kuendeleza mafanikio ya vijana katika mkoa
wa Kilimanjaro.
Rai hiyo imetolewa leo na vijana walioshiriki semina
inayoendeshwa na wawezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo kuwaelimisha vijana kuhusu Mfuko wa Maendeleo ya Vijana,
ujuzi pamoja na stadi za maisha.
Akizungumza wakati wa semina hiyo kijana Musa Mchomvu kutoka
kikundi cha Umoja ni Nguvu amesema kuwa mtazamo wa vijana kuhusu Mfuko
wa Maendeleo ya Vijana ulikua ni mdogo sana kutokana na vijana kutokuwa
na elimu na uelewa wa kutosha hivyo kuwashukuru wawezeshaji waliotoa
mafunzo juu ya mfuko huo na kuwataka vijana wazidi kushiriki semina
zinazotolewa kwa vijana ili waweze kupata mwanga utakaowawezesha
kujiendeleza.
Kwa upande wake Bibi. Salome Sichalwe amewataka vijana wa Mwanga
kuweka siasa pembeni kwa kuachana na ahadi zinazotolewa na wanasiasa
wanaowasababishia vijana kubweteka bali wajiwekee malengo
yatakayowawezesha kuunda Saccoss imara ya Wilaya na kujiunga katika
vikundi vya ujasiliamari kwa maendeleo ya Wilaya na Mkoa wa Kilimanjaro
kwa ujumla.
Naye Bw. Idrisa Bajah wa kikundi cha Mwanga Youth Employment
Fund amesema kuwa Wilaya ya Mwanga imekua na changamoto ya ajira kwa
vijana lakini kutokana na semina waliyoipata itawasaidia vijana
walioudhuria kuwanusuru vijana wenzao walioko mitaani kwa kuwapatia njia
mbadala za kiujasiriamali.
Aidha mwezeshaji kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo Bibi. Ester Riwa amesema kuwa vijana wengi wamekata tamaa
kwasababu hawajitambui, hawatambui fursa zinazowazunguka na kukosa
ubunifu kitu ambacho kinachowafanya kushindwa kutumia rasilimali ndogo
zilizopo kujiendeleza.
Bibi. Riwa amezitaka Halmashauri kutekeleza mwongozo wa
kuwasaidia vijana kupata mkopo unaotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya
Vijana kwa kuunda Saccoss za Wilaya, kusimamia utengenezaji wa vikundi
hai vya vijana na kuwaongoza vijana kuandika miradi iliyo na mashiko ili
kufanikisha zoezi la kupatiwa mikopo inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo
ya Vijana na kurejesha mikopo hiyo katika mfuko kwa ajili ya kupatiwa
vijana wengine wanaohitaji mkopo
No comments:
Post a Comment