Kutua Februari, apania kuzalisha akina Mayweather kibao nchini
NDONDI ni miongoni mwa michezo maarufu mno hapa Tanzania na duniani kwa ujumla.
Wapo wanamichezo waliojipatia heshima kubwa duniani kutokana na kufanikiwa kupitia mchezo wa ndondi.
Miongoni mwa wanamichezo hao ni nguli Mohammed Ali, Mike ‘Iron’ Tyson, Evender Holyfield, Floyd Mayweather, Manny Pacquiao na wengineo wengi.
Kwa hapa nchini, wapo
mabondia waliojitengenezea majina wakiwamo Emmanuel Mlundwa, Habibu
Kinyogoli ‘Masta’ Michael Yombayomba, Stanley Mabesi ‘Ninja’ Rashid
Matumla, Ibrahimu Class ‘King Class Mawe’ na wengineo wengi.
Lakini ikumbukwe kuwa ndondi
ndio mchezo uliotoa mwanamichezo anayelipwa zaidi duniani kwa sasa
ambaye si mwingine bali ni Mayweather, akifuatiwa na mwanasoka raia wa
Ureno anayekipiga katika klabu ya Real Madrid ya Hispania, Cristiano
Ronaldo.
Anayeshika nafasi ya tatu ni
mchezaji wa mpira wa kikapu LeBron James, wakati mwanasoka anayechezea
Barcelona ya Hispania, Muargentina Lionel Messi akishika nafasi ya nne,
huku wa tano akiwa ni mkali wa mpira wa kikapu, Kobe Bryant.
Pamoja na mafanikio hayo
katika ndondi, Tanzania imeonekana kuzidi kulala usingizi wa pono katika
suala zima la kuvumbua na kuendeleza vipaji vya mchezo huo kama sehemu
ya kutatua tatizo sugu la ajira linaloitesa nchi yetu kwa sasa.
Unapopita huko mitaani,
unaweza kukutana na vijana wadogo wakiwa wanafanya mazoezi ya ngumi kwa
kutumia vifaa visivyo rasmi ambavyo mwisho wa siku, huishia kuwadumaza
badala ya kuwajenga kama walivyotarajiwa.
Hali hiyo imetokana na
kukosekana kwa vifaa vya kujifunzia mchezo huo, zikiwamo kumbi na hata
wataalam wa kuwapa ujuzi wa kuwawezesha kufikia mafanikioi ya akina
Mayweather.
Ni kwa kufahamu hilo, wapo
wadau wa ndondi ambao wamekuwa wakijitoa kusaidia vipaji vya ndondi hapa
nchini, miongoni mwao akiwa ni Kocha wa Kimataifa wa Ndondi nchini,
Rajabu Mhamila ‘Super D’.
Bondia huyu wa zamani,
ameshawahi kufanya jitihada kadha wa kadha kuendeleza ndondi hapa
nchini, ikiwamo kutoa mafunzo kwa vijana chini ya klabu yake ya Ashanti
Boxing Club na kupitia DVD zake zenye mapambano makali yaliyowahi
kufanyika hapa nchini na duniani kwa ujumla, yakiwahusisha mabondia
nyota.
Katika kuonyesha jinsi
anavyoguswa na ndondi, Februari mwaka huu Super D atakuwa na ugeni
mkubwa wa bondia Mtanzania anayefanya kazi zake nchini Deer Park, Victoria, Australia, Omari Kimweri ambaye anatua nchini kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wanamasumbwi wa Tanzania.
Akizungumza Dar es salaam
jana, Super D anasema kuwa ujio wa Kimweri ni fursa nyingine adimu kwa
mabondia wa Tanzania katika kuona ni vipi wanaweza kutimiza ndoto zao za
kutoka kimaisha kupitia mchezo huo.
Anasema kuwa Kimweri atatua
akiwa na vifaa mbalimbali vya masumbwi ambapo pia atatoa mafunzo na
mbinu mpya zinazotumiwa na mabondia wa nje kwa mabondia pamoja na
kushuhudia mapambano kadhaa yatakayofanyika kwa kipindi atakachokuwapo
hapa nchini.
“Kimweri anakuja akiwa na
msafara wa watu kadhaa, akiwamo mwanasoka wa kike, Melanie Gines ambaye
ni raia wa Hispania. Akiwa hapa nchini, Melanie atapata fursa ya
kukutana na wanasoka wa kike wa hapa , kwani amechezea timu nyingi za
Ulaya, Hispania,” anasema Super D.
Anasema kuwa ujio wa Kimweri
umewezeshwa kwa kiasi kikubwa na promota wake, Brian Amatruda ambaye ni
miongoni mwa mapromota maarufu nchini kwao Australia, akiwa amekubali
kutoa baadhi ya vifaa vya kisasa kutoka Hispania na Marekani kwa ajili
ya ziara hiyo.
Super D anasema kuwa Kimweri
ambaye ni bingwa wa WBO, atatua nchini akiwa na mikanda yake yote
aliyowahi kutwaa, ukiwamo wa ubingwa wa Australia, lengo likiwa ni
kuwahamasisha vijana wa kitanzania kujikita zaidi katika ndondi.
“Nimezungumza na Kimweri na
ameonyesha kuwa na uchungu wa kuwainua mabondia wa hapa nchini ili
waweze kutimiza ndoto zao na anafanya hivyo chini ya mradi wake wa
‘Kimweri Project’ na atakuwa hapa nchini kwa wiki moja,” anasema.
Anasema kuwa ujio wa bondia
huyo uliochagizwa na Super D Boxing Coach and Promotion, umelenga
kuwahamasiaha mabondia kucheza mara kwa mara ili kupandisha viwango vyao
kwani hiyo ndio siri ya mafanikio ya wanamasumbwi wengi duniani.
Mbali ya mafunzo kutoka
kwa Kimweri, pia katika ziara zake zote sehemu mbalimbali nchini,
kutakuwa na uuzwaji wa DVD za Super D zenye lengo la kutoa mafunzo
kupitia mapambano ya mabondia maarufu duniani, akiwamo Floyd
Mayweather,Manny Paquaio, Mohamerd Alli, na wa hapa nchini kama Mbwana
Matumla, FrancisMiyeyusho,Ibrahimu Class’ King Class Mawe’ ambaye ni bingwa
wa WPBF Africa na wengineo.
No comments:
Post a Comment